Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli
Na Joseph Mwendapole, Iringa
Wakati zikiwa zimebaki siku 25 kabla ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema hadi sasa anaona mambo yanamuendea vizuri kwenye kampeni zake na hivyo anataka kupata ushindi wa kishindo wa asilimia 99.
Wakati zikiwa zimebaki siku 25 kabla ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema hadi sasa anaona mambo yanamuendea vizuri kwenye kampeni zake na hivyo anataka kupata ushindi wa kishindo wa asilimia 99.
Magufuli aliyasema hayo jana kwenye Uwanja wa Samora uliopo Iringa mjini wakati wa mkutano wake wa kuhitimisha kampeni mkoani hapa.
Alifafanua kuwa matarajio hayo ya ushindi mnono dhidi ya wapinzani yanatokana na idadi kubwa ya watu wanaomuunga mkono katika mikoa mbalimbali ambayo ameshafanya kampeni zake hadi sasa.
Alisema wingi wa watu wanaomuunga mkono umempa matumaini kwamba wapinzani wake wataishia 'kuisoma namba' tu kwani mwishowe hawataambulia kitu.
Mgombea huyo aliahidi kujenga uwanja ndege wa Iringa kuwa wa kisasa ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje pamoja na kujenga kilomita kumi za lami maeneo ya Iringa mjini.
Kadhalika, Dk. Magufuli aliwataka wananchi wa Iringa mjini kumchagua mgombea ubunge wa CCM, Fredrick Mwakalebela, kwani anatosha kuwaletea maendeleo.
Alisema atawashangaa wananchi wa Jimbo hilo kama watamwacha Mwakalebela ambaye ametumia muda mwingi kushughulikia matatizo ya wananchi hao kiasi cha kuacha kazi yake ya ukuu wa wilaya.
Alimtaka mbunge wa sasa wa jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, kuachana na siasa na badala yake kuendelea na kazi ya uchungaji wa kondooo wa Bwana.
“Huyu Mchungaji Msigwa aendelee tu kuchunga Kondoo wa Bwana ili tukifanya dhambi tupate sehemu ya kwenda kutubu... na hii kazi ya ubunge haiwezi, amwachie Mwakalebela,” alisema Magufuli.
Alisema Mwakalebela ni kijana mwadilifu na mchapakazi ambaye hata baada ya kushinda na jina lake kutorudi hakuwahi kuhamia vyama vya upinzani kama ilivyotokea kwa wengine.
AENDELEZA 'PUSHAPU'
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli ameendeleza staili yake ya ‘pushapu’ jana wakati alipomtaka mgombea ubunge wa Jimbo la Kilolo kwa tiketi ya CCM, Venance Mwamoto, kufanya hivyo ili kuwadhihirishia wapiga kura wake kwamba yuko 'fiti' kuwatumikia.
Tukio hilo lilitokea jana mchana kwenye mkutano wake wa kampeni katika jimbo hilo la Kilolo mkoani Iringa, ambalo lilikuwa likiongozwa na mbunge wa chma hicho, Prof. Peter Masolla.
Dk. Magufuli aliwaambia wananchi wa jimbo hilo kwamba anamwamini kwa kiasi kikubwa Mwamoto kutokana na uhodari wake katika kazi na uadilifu hivyo angependa kuona wananchi wa jimbo hilo wanamchagua kwa kishindo.
“Huyu namfahamu siku nyingi ni mtu mchapakazi ambaye ameacha kazi yake ya ukuu wa wilaya kuja kuwatumikia wananchi wa Kilolo na mwamini kwamba atawatumikia kwa moyo wake wote na ili kuwadhihirishia kwamba una nguvu ya kuwafanyia kazi Mwamoto piga ‘push-up’ kidogo hapa jukwaani,” alisema Dk. Magufuli.
Baada ya ombi hilo, Mwamoto aliinama jukwaani na kupiga ‘pushapu’ kumi, hali iliyoibua shangwe na nderemo kwa wananchi waliojitokeza kwa wingi kumsikiliza mgombea huyo wa urais wa CCM.
Tukio hilo ni la pili kutokea kwa Dk. Magufuli kuwaamuru wagombea ubunge kupiga ‘push-up’ kwa niaba yake kuonyesha ukakamavu kwamba wana uwezo wa kuwatumikia watanzania usiku na mchana.
Juzi jioni akiwa katika jimbo la Mafinga mkoani hapa, Dk. Magufuli aliwaamuru wagombea ubunge watatu wa wilaya ya Mufindi mkoani hapa kupiga ‘push-up’ kwa niaba yake ili kuwaonyesha wananchi namna walivyo imara kiafya kuwatumikia.
Dk. Maagufuli alianzisha staili akiwa kwenye mkutano wa kampeni wilayani Karagwe mkoani Kagera ambapo aliinama jukwaani na kupiga ‘pushapu’ saba.
Akiwa katika Jimbo la Kalenga mkoani hapa, Dk. Magufuli alisema anahitaji kura za wanachama wa vyama vya upinzani ili aweze kuingia Ikulu hivyo kamwe hatawatukana wapinzani majukwaani.
Alisema ataendelea kufanya kampeni za kistaarabu kwasababu anajua anahitaji kuungwa mkono na wanachama wa vyama vyote vya siasa, ili kura zake zitoshe kumwingiza Ikulu.
Dk. Magufuli ambaye amekuwa akiepuka kuwarushia vijembe na kashfa wapinzani, alisema ameamua kufanya hivyo kwasababu akiwa rais atakuwa rais wa vyama vyote na kwamba hatabagua.
“Hapa sijamtukana mtu na wala sitarajii kumtukana mtu, maana nahitaji kura zenu wote ili nishinde na nyinyi wa ‘people’s power’ mnipe hiyo ‘power’ niingie Ikulu, uwe Chadema, ADC Maendeleo, Ukawa nahitaji kura yako maana nitakuwa rais wa watanzania wote,” alisema Dk. Magufuli.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Abdalah Bulembo, alisema mabadiliko ya kweli yataletwa na mgombea wa CCM ambaye ni msomi kuliko wagombea wengine.
Alisema CCM haikubahatisha kumpitisha Dk. Magufuli kwenye nafasi hiyo kwasababu wanamwamini kutokana na rekodi ya utendaji na uaminifu wake akiwa mtumishi wa serikali.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment