Wanajeshi wa Nigeria wamekuwa wakikabiliana vikali na wapiganaji wa Boko Haram
Wapiganaji 200 wa kundi la Kiislamu la Boko Haram wamejisalimisha, jeshi la Nigeria limesema.
Wapiganaji hao wanadaiwa kujisalimisha kwa vikosi vya serikali katika mji wa Banki karibu na mpaka wan chi hiyo na Cameroon.
Jeshi lilikuwa awali limesema kuwa mji huyo umekombolewa kutoka kwa wapiganaji hao lakini habari hizo hazikuweza kuthibitishwa.
Watu 17,000 wanadaiwa kuuawa na wapiganaji hao katika kipindi cha miaka sita, wengi kaskazini mwa Nigeria.
Mwandishi wa BBC nchini Nigeria Will Ross anasema wapiganaji wengi wa Boko Haram wamekuwa wakijisalimisha wiki za hivi karibuni lakini kundi lililojisalimisha leo ndio kubwa kuwahi kujisalimisha wakati mmoja.
Operesheni ya wanajeshi imefanikiwa kuwadhoofisha wapiganaji hao lakini wengi wa raia wa Nigeria wanataka ushahidi wa kuthibitisha madai hayo ya jeshi, na thibitisho kwamba hao ni wapiganaji na wala si raia walionaswa mjini, mwandishi wetu anasema.
Mwaka huu, wanajeshi wamefanikiwa kukomboa karibu maeneo yote yaliyokuwa yametekwa na Boko Haram.
Jeshi pia limekomboa watu kadha waliotekwa nyara na kundi hilo na wiki hii lilitangaza kuokolewa kwa wanawake 241 na watoto karibu na mpaka wa Nigeria na Cameroon.
Mashambulio yanayotekelezewa na kundi hilo yameongezeka tangu Muhammadu Buhari aapishwe kuwa rais mwezi Mei, baada yake kushinda uchaguzi.
CREDIT: BBC
No comments:
Post a Comment