Edward Lowassa wakati alipokuwa akizunguka mikoani kusaka udhamini ili ateuliwe kuwania urais kupitia CCM.
Edward Lowassa wakati akienda kuchukua fomu ya kugombea urais kupitia.
Chadema.
Edward Lowassa akiwa katika mojawapo ya mikutano ya kampeni ya Ukawa.
Na Daniel Mbega
MGOMBEA urais wa Chadema, Kapteni mstaafu Edward Lowassa,
ameendelea kuchanja mbuga kwenye kampeni ambapo licha ya kupata watu wengi
kwenye mikutano yake, bado anaivunia ‘mtaji’ wa kura milioni 2.5, imefahamika.
Idadi hiyo inatokana na watu waliojitokeza kumdhamini
katika mbio zake za kusaka urais, kwanza ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na
baadaye ndani ya Chadema, na wachunguzi wa mambo wanasema, ikiwa watu hao
watakuwa na tafsiri ya kuchagua mtu badala ya chama, basi mgombea huyo anaweza
kujihakikishia kura hizo.
Mbali ya kuja na mbinu na mkakati mpya wa kupita kila
alikokanyaga mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli, lakini Lowassa ameonekana
kupata watu wengi, hasa katika mikoa ambayo alipita kuomba udhamini katika mbio
za kuwania urais.
Kabla ya
kuhamia Chadema, Lowassa alidhaminiwa na wanachama 873,500 wa CCM nchi nzima
ikiwa ni mara 1953 ya idadi iliyotakiwa ya wadhamini 450 tu.
Wakati
anarejesha fomu za kuwania urais ndani ya Chadema Agosti Mosi, 2015, Lowassa
aliweka rekodi kwa kupata wadhamini 1,662,397 katika mikoa yote 32, ikiwa ni zaidi
ya nusu ya kura za urais ambazo chama hicho kilipata kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2010.
Katika
uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, mgombea urais wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alishika
nafasi ya pili baada ya kupata kura 2,271,941 sawa na asilimia 26.34, huku Rais
Jakaya Kikwete akipata kura 5,276,827 sawa na asilimia 61.17.
Mikoa
ambayo Lowassa alidhaminiwa na wanaCCM wengi ni Morogoro (100,438), Dar es
Salaam (95,251), Simiyu (5,000), Kilimanjaro (33,780), Geita (3,000), Shinyanga
(7,114), Tabora (9,516), Tanga (204,125), Arusha (120,335), Mbeya (78,500),
Iringa (58,562), Njombe (10,900), Manyara (42,405), Katavi (3,440), Lindi (3,279),
Singida (22,758), na mingineyo.
Inaelezwa
kwamba, idadi hiyo ya wanaCCM waliomdhamini ni kubwa sana na unaweza kuwa mtaji
wake muhimu ikiwa wataamua kumchagua, hivyo kuongeza idadi ya kura pamoja na
zile za wananchi wengine wanaomuamini kwa nafasi hiyo adhimu.
Hata
hivyo, pamoja na kuwa na mtaji huo, bado mpambano ni mkali kwani mgombea wa
CCM, Dk.Magufuli, naye ameonekana kushika kasi kwenye kampeni zake.
Tayari
Magufuli amefanya kampeni katika mikoa sita ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na
Kanda ya Kusini ambayo ni Katavi, Rukwa, Mbeya, Njombe, Ruvuma na Mtwara
alikofanya mikutano takriban 50 ya hadhara na mikutano midogo 126 ambako
ameinadi Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 na kuzidi kujiimarisha.
Wakati
ambapo Magufuli, ambaye kwa sasa ameigeukia Kanda ya Kaskazini, ametembela
zaidi ya kilometa 7,000 kwa kutumia gari na maeneo mengi akitembea kwa miguu,
tayari Lowassa ameanza kutumia helkopta.
Baadhi ya
tafiti za awali za mashirika ya ndani na nje ya nchi zimeonyesha kwamba CCM
itashinda uchaguzi wa mwaka 2015 kwa zaidi ya asilimia 60, lakini mwa mwendo
ulivyo sasa inaonekana kuwa inaweza kushinda kwa asilimia zaidi ya 80.
Hatua
hivyo, pengine ndiyo iliyomfanya Lowassa, Kapteni mstaafu wa Jeshi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ), kuja na mbinu mpya ya kuhakikisha anakanyaga kila mahali
ambako Magufuli amepita ikiwa ni namna ya kubadilisha upepo.
Lowassa
ametembelea mikoa ya Iringa, Njombe, Rukwa, Katavi, Tabora, Morogoro, Dar es
Salaamna na bado anaendelea kupita katika mikoa ambayo Magufuli amepita, lakini
ile ambayo yeye mwenyewe alipata udhamini wa kutosha akiwa CCM na Chadema.
Hata
hivyo, kuna baadhi ya maeneo ambayo Lowassa ameshindwa kufika licha ya kwamba
tayari yalikuwa kwenye ratiba yake iliyowasilishwa kwenye Tume ya Taifa ya
Uchaguzi.
Maeneo
hayo ni Ludewa mkoani Njombe na Tunduru mkoani Ruvuma, ambako wananchi walikuwa
wakimsubiri lakini hakuonekana, hatu ambayo imeelezwa kwamba huenda mgombea
huyo amechoka na ndiyo sababu ameanza kutumia helkopta.
Wagombea
wote wawili, wakiwemo na wa vyama vingine sita, wanalenga mikoa takriban tisa
ambayo inaonekana kuwa na mtaji mkubwa wa kura, mikoa hiyo ni Dar es Salaam,
Mbeya, Mwanza, Morogoro, Kagera, Tanga, Tabora Dodoma
na Kigoma, ambayo ina karibu asilimia 50 ya wapiga kura wote nchini, huku ikiwa
na wakazi 24,253,541 kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya mwaka 2012.
Waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
linalotumia mfumo wa Kielektroniki (BVR) ni 23,782,558, sawa na asilimia 99.5
ya waliokadiriwa kujiandikisha nchini kore.
Ingawa Tume ya Taifa ya Uchaguzi haijatoa idadi kamili ya
wapiga kura katika kila mkoa, lakini baadhi ya mikoa ambayo idadi yake imetajwa
ni Dar es Salaam iliyoandikisha watu 2,845,256, Tabora (1,083,926), Kagera
(1,039,268), Mara (884,985), Ruvuma (826,779), Kilimanjaro (794,556), Mtwara
(682, 295), Manyara (673,357) na Lindi (569,261).
0656-331974
Makala haya yalichapwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la WAJIBIKA la Septemba 14, 2015.
No comments:
Post a Comment