Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday 24 September 2015

SABABU 10 ZA UKAWA KUSHINDA OKTOBA 25



Na Daniel Mbega
Kampeni za urais zinaendelea na zimebaki takriban siku 30 tu kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015.
Kuna mtikisiko mkubwa wa kisiasa nchini baada ya Edward Lowassa kuhamia upinzani, kama ule wa mwaka 1995 (miaka 20 iliyopita) wakati Augustine Lyatonga Mrema alipokaribishwa NCCR-Mageuzi.
Pamoja na uzoefu na ukongwe wa CCM, lakini mtikisiko wa sasa umekifanya chama hicho tawala kianze kufikiria ‘Plan B’ kukabiliana na wimbi kubwa la mageuzi linalotokana, siyo tu na Ukawa, bali ujio wa Lowassa upande wa pili.
Wachambuzi wengi wa siasa wanaielezea hali hiyo kama ni ushindi wa mapema kabisa wa Ukawa ikiwa CCM itabeza na kupuuza kasi ya mabadiliko ya sasa na nguvu ya Lowassa.
Blogu ya www.brotherdanny.com inajaribu kuchambua sababu ambazo zinaweza kuufanya upinzani kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kushinda uchaguzi huu.
Zipo sababu nyingi, lakini kubwa ni 10 ambazo zinatajwa kwamba zinaweza kuipa Ukawa ushindi asubuhi tu. Sababu hizo ni hizi zifuatazo:

1. Nguvu za Lowassa
Kuwepo kwa Lowassa kama mgombea urais kupitia Ukawa ni turufu mojawapo ya umoja huo kutokana na umaarufu wa mwanasiasa huyo ambaye ndani ya wiki moja tayari amebadilisha hali ya hewa nchini.
Lowassa ni maarufu, mashuhuri na anakubalika kila kona, kwani tayari alikwipandikiza ‘mbegu’ kwenye mioyo ya wananchi ambao wanamwamini kwa asilimia kubwa kwamba ndiye hasa anayeweza kuleta mabadiliko. Kama walivyomwamini wanaCCM wenzake, ndivyo ambavyo wataendelea kumwamini akiwa upande wa pili.
Lowassa ni taasisi imara, ambayo haitegemei chama, na kigezo cha kuwa na wafuasi wengi kila kona ndicho kilichowashawishi wapinzani kumchukua, wakiwa na nia thabiti ya kuing’oa CCM madarakani. Anakidhi vigezo vyao walivyokuwa wameviweka awali.
Lowassa ni maarufu kuliko mgombea wa CCM, lakini pia anao uwezo wa rasilimali (watu na fedha) za kutosha kuendesha harakati hizo.

2. Mabadiliko ya uongozi
Kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakiishi katika hali ya umaskini mkubwa huku viongozi wachache wakineemeka kwa kujilimbikizia mali kupitia nyadhifa zao. Japo Lowassa ni mmoja wa waliokuwa kwenye kundi hilo, lakini baadhi wanaona kwamba ni afadhali amehamia upande wa pili ili kwa nguvu zake awezeshe upinzani uchukue Dola.
Mfumo wa ufisadi unatajwa kuota mizizi ndani ya CCM na Serikali yake naimekuwa vigumu kupambana na mtu mmoja mmoja kwa sababu kila anayeingia, hata kama atakuwa na msimamo imara, lazima mfumo utamnyumbisha na kufanya yale yanayokera.
Ni uongozi mpya, wa upinzani, ambao wengi wanaamini kwamba unaweza kuufumua mfumo huo na kuimarisha maadili ya utendaji ili haki sawa ipatikane na wananchi wapate maendeleo.
Vyamavya upinzani vilikwishaifanya kazi hiyo kwa miaka kadhaa sasa, na kuwepo kwa Lowassa mwenye wafuasi wengi kutakamilisha kiu ya wengi ya mabadiliko ya uongozi.

3. Uwezo wa kujenga hoja
Ukawa wana hazina ya viongozi wanaoweza kujenga hoja na kuifafanua vyema. Kwa kuchanganya na uwezo wa Lowassa ambaye anaweza kubeba agenda na kuisimamia, kuna kila dalili kwamba kazi ya kampeni itakuwa rahisi kuliko ilivyotegemewa na wengi.
Lakini ni vyema wapinzani wakabeba agenda chache ambazo watazifafanua kwa wananchi badala ya kubeba agenda nyingi, ambazo badala ya kuwavutia wananchi, huwachanganya. Lazima wawe na agenda bora kuliko za CCM ili kufanikisha kazi hiyo na si kuzungumzia mambo ya kufikirika.
Lowassa anatajwa kwamba ni mtu mwenye kuweka vipaumbele na kuvisimamia ipasavyo, hivyo hata agenda watakaoziweka Ukawa zina matumaini ya kusimamiwa na kufanikiwa.

4. Mgawanyiko wa CCM
Wapinzani wanaweza kutumia mgawanyiko wandani ya CCM kama talanta yao katika kushinda uchaguzi. CCM imeparaganyika tangu Lowassa alipoenguliwa na Kamati Kuu Julai 10, 2015, ambapo makada wengi wameamua kuhama naye kwenda upinzani, hatua ambayo inakidhoofisha chama hicho tawala.
Wimbi la makada wengi kujiunga na upinzani kabla, wakati na baada ya Lowassa kuhama CCM linaonyesha dhahiri kwamba chama tawala kitakuwa na kazi ya ziada kuwaaminisha wananchi kwamba bado kinastahili kupewa dhamana ya uongozi, na kwa bahati mbaya muda hautoshi.

5. Uwezo wa kubadili mfumo
Tatizo kubwa la mfumo mbovu ndilo limeifanya CCM ionekane imeshindwa kazi licha ya kuongoza nchi kwa miaka mingi. Rais Jakaya Kikwete anatajwa kwamba si mtu wa maamuzi magumu ndiyo maana ufisadi na rushwa vimetamalaki.
Hali hiyo imewafanya wengi kutamani kwamba rasi ajaye awe walau dikteta na mwenye uwezo wa kuubadili mfumo. Maoni hayo ya kutaka rais dikteta yametolewa na wengi wakiwemo Waziri Mkuumstaafu Cleopa David Msuya, Kamanda wa Polisi mstaafu Alfred Tibaigana, wasomi na watu mbalimbali.
Lowassa ndiye kwa kiasi ametajwa kwamba anazo sifa hizo za udikteta, japokuwa maamuzi yake yamewahi kuleta athari kwa upande mwingine, lakini pia ana maono na hapotezi mwelekeo. Ubadilishaji wa mifumo ukifanywa haraka na kwa pupa, utaingilia na kuvunja hata mifumo ambayo ilikuwa imeanza kukua na kukomaa kwa upande chanya.

6. Msimamo kuhusu Katiba
Ukawa ulianzishwa baada ya wajumbe wa upinzani kususia vikao vya Bunge Maalum la Katiba mwaka 2014, hivyo wanaamini agenda hiyoitakuwa fimbo yao ya kuichapa CCM ambayo ilifanya hila kuichakachua Rasimu ya Pili ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba.
Mgombea wa Ukawa, Lowassa, alikuwa mmoja wa wajumbe wa Bunge hilo, na kwa vyovyo te vile atalazimika – hata kama alikuwa anaunga mkono Serikali Mbili – kunadi maono ya upinzani kuhusiana na katiba hiyo mpya ili kujenga imani kwa wananchi. Lakini msimamo wowote kuhusiana na suala la Katiba Mpya unaweza kuwa na ukinzani kulingana na jinsi wananchi watakavyolitazama.

7. Kuinua uchumi
Kilio cha Watanzania wengi ni umaskini. Ukawa wanapigia kelele hali duni ya maisha ya wananchi, hasa vijijini, huku ahadi za CCM za kuwapa maisha bora kila Mtanzania zikiwa ndoto zilizoyeyuka kabla ya kupambazuka.
Agenda ya Lowassa ya kuuchukia umaskinina kutamani walau kila Mtanzania awe na utajiri kama walivyo akina Bakhressana wengineo inaweza kuwashawishi Watanzania wakaleta mabadiliko kwenye kura, kwani walio wengi ahadi kama hizo – hata kama hazitimiliki – kwao huwa na mvuto wa aina yake.
Lowassa amekuwa Waziri wa Tamisemi, anazijua halmashauri zinavyojiendesha, anayafahamu maisha ya vijijini yalivyo, kwa hiyo kwake itakuwa rahisi kuinadi agenda hiyo kwa nguvu zote. Lakini bila kusahau kwamba ana uzoefu katika masuala ya kimataifa.

8. Uchapaji kazi na maendeleo
Vyama vyote vya upinzani umekuwa vikihimiza uchapaji kazi na kukemea uzembe ambao umesababisha rasilimali za taifa kuporwa na wachache, hivyo Ukawa wanaweza kusimamia agenda hiyo na kutoa mifano hai ambayo imezalisha mafisadi wengi.
Kumsimamisha Lowassa ni faida kwao kwani mbali ya udhaifu alionao, bado alijiwekea rekodi bora ya uchapakazi katika wizara zote alizopitia tangu serikali ya awamu ya pilihadi ya nne. Wananchi wanapenda mtu mchapakazi siyo longolongo na Lowassa anauzika kirahisi kwa wananchi.

9. Kashfa ya Escrow
Kashfa ya ufisadi wa akaunti ya Benki Kuu ya Escrow badoiko vichwani mwa wananchi hasa baada ya kuiyumbisha serikali kiasi cha kubadilishwa kwa Baraza la Mawaziri huku wahusika wakishindwa kuchukuliwa hatua.
Ukawa wataifukua kashfa hiyo na kuijengea hoja nzito kwenye kampeni na huenda ikazusha mijadala mingi kama ilivyokuwa mwanzoni.

10. Kupambana na rushwa
Japokuwa Lowassa si msafi kivile, lakini agenda ya kupambana na mafisadi inaweza kuwapa kura nyingi Ukawa, kwa vile wamekuwa wakipigia kelele vitendo vya rushwa kwa miaka mingi. Ukawa wanapaswa kuwa mipango ya kuziba haraka mifumo inayoleta mianya ya rushwa ndani ya nchi na wao wenyewe wajitakase.
Udhaifu wa Lowassa uko pia katika eneo la mapambano dhidi ya rushwa na ikumbukwe kwamba alipokuwa Waziri Mkuu hakuonyesha makeke yake kwenye mapambano dhidi ya rushwa na hakutaka kujihusisha wala kujionyesha kuwa anawachukia wala rushwa. Pamoja na kuonyesha utendaji mzuri akiwa Waziri Mkuu, kipengele hiki kilimuangusha na hadi leo hii kokote kule anakokwenda hapendi kuzungumzia rushwa na wala rushwa. Huu ni udhaifu wake mkubwa.

Kesho nitaeleza sababu 10 za CCM kushinda uchaguzi huo licha ya mihemko ya vijana...
0656-331974

No comments:

Post a Comment