Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday 24 September 2015

UTAFITI TWAWEZA WAIBUA MASWALI 14

Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli
Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli (kushoto) na mgombea urais wa Chadema Edward Lowassa (kulia), wakiwa katika mikutano ya kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu. 

Dar es Salaam. Siku moja baada ya taasisi ya Twaweza kutoa ripoti ya maoni ya wananchi kuhusu uchaguzi wa Oktoba 25, maswali yameibuka kwenye mijadala mbalimbali miongoni mwa wananchi, yakihoji jinsi maoni hayo yalivyokusanywa, wafadhili wa utafiti na namna maamuzi kadhaa yalivyofikiwa.
Kadhalika maswali mengine yaliyozua utata kuhusu utafiti huo ni sababu za maoni hayo kuanza kukusanywa siku mbili kabla ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupitisha wagombea urais, na iwapo uamuzi huo haungeweza kuathiri matokeo. Baadhi ya maswali hayo yamejibiwa na Twaweza.

Hata hivyo, baadhi ya maswali yamejibiwa na Twaweza wakati ikiwasilisha utafiti wake na jana wakati gazeti hili lilipowasiliana na taasisi hiyo, ikisema maswali hayo hayashangazi kwa kuwa hii si mara ya kwanza kwake kufanya utafiti kwa kukusanya maoni.

Kuhusu aliyefadhili utafiti huo, Mshauri Mkuu na Meneja wa Mawasiliano wa Twaweza, Risha Chande alisema kwa kawaida taasisi hiyo inatumia fedha zake kufanya utafiti.

Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo mpya yaliyotangazwa juzi, asilimia 65 ya wananchi wa Tanzania Bara wangempigia kura mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli iwapo uchaguzi ungefanyika kati ya Agosti 19 na Septemba 7.

NEC ilipitisha majina ya wagombea nane wa urais Agosti 21 na kampeni kuruhusiwa kuanza Agosti 22, lakini utafiti huo umetaja majina ya wagombea wawili, licha ya kipindi cha utafiti kudumu kwa takriban mwezi mmoja baada ya kampeni kuanza.

Utafiti huo unaonyesha kuwa asilimia 25 wangempigia kura mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, iwapo uchaguzi ungefanyika kipindi hicho.

Katika utafiti wa taasisi hiyo wa mwezi Novemba mwaka jana, Lowassa akiwa ndani ya CCM alikuwa akiongoza kwa mbali wakati Dk Magufuli hakuwamo kwenye tano bora.

Huu ni utafiti wa kwanza mkubwa wa kisiasa uliofanywa tangu kipenga cha kampeni kilipopulizwa Agosti 23, mwaka huu.

Katika maelezo ya methodolojia ya utafiti, Twaweza imeeleza kuwa ilikusanya maoni hayo bila kuwauliza wahojiwa jina la mgombea na kwamba watu waliohojiwa ndio waliotaja jina la mgombea ambaye walimtaka, lakini ripoti ya utafiti huo haikutaja baadhi ya majina yaliyojitokeza zaidi ya Dk Magufuli na Lowassa.

Kadhalika, Twaweza ilisema haikutaka kukusanya maoni kwa kuangalia wingi wa watu katika mikutano ya kisiasa au vichwa vya habari vya magazeti bali waliona kura ya maoni ya wananchi ndiyo inayoweza kueleza ukweli kisayansi.

Kwa mujibu wa Twaweza, utafiti huo ulitumia mawasiliano ya simu kukusanya maoni, ikieleza kuwa huo ni utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa uliotumia simu za mkononi walizogawiwa wahojiwa.

“Ili kuhakikisha kwamba uchaguzi nasibu unawakilisha vilivyo Tanzania Bara, simu za mkononi na chaja zinazotumia mwanga wa jua ziligawiwa kwa kaya zilizoshiriki. Kaya zisizowakilishwa ni zile tu zilizopo katika maeneo ambayo hayafikiwi na mitandao ya simu,” ilisema ripoti ya Twaweza.

Ajenda 9 zilizotumika kukusanya maoni

Ripoti ya Twaweza inaeleza kuwa maoni hayo yalikusanywa kwa kujikita katika mambo tisa yaliyojenga ajenda. Mambo hayo ni pamoja na matatizo makuu yanayowakera wengi nchini (elimu, afya, kipato, ajira na ugumu wa maisha).

Mengine ni utekelezaji wa ahadi za wabunge, idadi ya wanaodhamiria kupiga kura mwaka huu, changamoto ya uandikishaji katika BVR, kama Watanzania wanaijua tarehe ya kupiga kura, chama kinachopendwa, nafasi ya urais ya Ukawa na sababu za kumpigia kura Lowassa au Magufuli.

Awamu za utafiti

Chande alifafanua kuwa hii si mara ya kwanza kwa Twaweza kufanya utafiti unaofanana na huu, akitoa mfano utafiti wa awali wa Sauti za Wananchi wa mwaka 2012 ambao ulihusisha watu 2,000, Sauti za Wananchi Awamu ya 10 kutoka Oktoba 2013, Sauti za Wananchi Awamu ya 24 kutoka Septemba 2014 na Sauti za Wananchi Awamu za utafiti Aprili na Julai 2015.

Kadhalika Twaweza inabainisha kuwa waliohojiwa ni watu wa mikoa yote ya Tanzania Bara. Hata hivyo haikueleza sababu za kutoihusisha Zanzibar hata katika tafiti zao za nyuma.

Chande alisema waliohojiwa walichaguliwa bila kulenga kundi maalumu na kufafanua kuwa mbinu hiyo inatumika kukadiria wastani wa mgawanyo wa tabia, mtazamo au maoni ya wananchi wote kwa ujumla.

“Hii ni njia inayokubalika kisayansi na kura za maoni za siasa kote duniani,” alieleza Chande.

Hata hivyo, Twaweza ilisema hawawezi kutabiri matokeo ya uchaguzi kwa uhakika lakini takwimu hizo ni picha inayoakisi kupendwa kwa wanasiasa tangu kampeni za uchaguzi zilipoanza.

CCM yaponda wanaopinga

Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba amewaponda na kuelezea kushangazwa na baadhi ya wasomi wanaopinga matokeo ya utafiti huo.

Wakati akiwashangaa wasomi hao, ameelezea sababu tano za kuukubali na kuunga mkono utafiti huo wa Twaweza.

January aliwataka wasomi wanaoupinga utafiti huo watambue kuwa umefanywa kisayansi na kwamba wasomi ambao ni werevu hupinga matokeo ya utafiti kwa utafiti mwingine na si kuponda kwa kejeli, kashfa, matusi wala vitisho.

“Ni vyema tukajifunza kupokea habari mbaya na nzuri bila taharuki. Ikumbukwe Agosti mwaka 2010, taasisi ya utafiti ya kimataifa ya Synovate ilitoa utafiti ulioonyesha CCM ingeshinda uchaguzi mwa mwaka 2010 kwa asilimia 61 na ikashinda.

Maswali 14 yaliyoibuliwa na tafiti ya Twaweza

1. Kwa mara ya kwanza Twaweza walisoma ripoti ya utafiti na kuonyeshwa moja kwa moja na TV. Nani alidhamini utafiti, matangazo hayo na kwa madhumuni gani?

2. Kwa nini waliamua kutoa matokeo ya utafiti wao katikati ya kampeni zenye ushindani mkali na mhemko mkubwa wa kisiasa?

3. Je, ni jinsi gani watu waliohojiwa walichaguliwa?

4. Je, watu waliohojiwa ni wa kutoka maeneo gani, makundi gani ya watu, ukiacha jinsia?

5. Je, waliohojiwa wamejiandikisha kupiga kura, mashabiki tu au mchanganyiko?

6. Twaweza wanajua kwamba kampeni za wagombea urais huanza baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuidhinisha wagombea waliopendekezwa na vyama. Kwa nini shirika hilo lilianza kufanya utafiti siku mbili kabla ya hapo?

7. Twaweza wanasema wahojiwa hawakupatiwa orodha ya majibu ya kuchagua. Je, ni kweli hawakuwa wanawajua wagombea wengine waliotajwa zaidi ya Dk John Magufuli na Edward Lowassa wakabaki kusema “mwingine?”

8. Katika nafasi ya ubunge na udiwani, wahojiwa wameonyesha kuwajua na kuwapigia kura wagombea wa ACT-Wazalendo. Inakuwaje watu hao hao washindwe kumtaja mgombea urais wa chama hicho badala yake Twaweza ikamweka katika kundi la “mwingine?”

9. Takwimu zote asilimia huwa ni 100 iliwezekanaje mgawanyo wa takwimu katika ripoti ya Twaweza katika baadhi ya maeneo asilimia zilizidi na au kupungua 100?

10. Tafiti zilizopita za Twaweza zilikuwa zinajumuisha watu wengi na zilikuwa zinaonyesha mtu aliyeshika nafasi ya kwanza pengine hadi 10. Kwa nini katika utafiti huu waliwalenga wawili tu Lowassa na Magufuli?

11. Ripoti inasema kwamba dodoso la utafiti huu liliandaliwa kabla ya uteuzi wa wagombea urais wa vyama vingine (nje ya mseto wa Ukawa), kikiwamo ACT-Wazalendo. Je, dodoso hilo lilikuwa na maelekezo gani kiasi kwamba ikawa vigumu kuwaingiza wagombea wengine?

12. Kwanini matokeo ya utafiti na kinachoonekana nje ni picha mbili tofauti?

13. Matokeo ya awali ya Twaweza yalionyesha Lowassa alipokuwa CCM aliongoza kwa ushawishi, iweje ndani ya wiki mbili baada ya kuhamia upande wa pili aporomoke hivyo?

14. Kwanini Twaweza hawakushirikisha Zanzibar katika utafiti wakati urais ni wa Muungano?

http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Utafiti-Twaweza-waibua-maswali-14/-/1597296/2883392/-/5mskirz/-/index.html

No comments:

Post a Comment