Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday 17 September 2015

UCHAGUZI MKUU TANZANIA NA VITA YA MAFUTA NA GESI


Na Daniel Mbega
WIKI iliyopita nilikuwa napitia – kwa mara nyingine – kitabu cha Confession of an Economic Hit Man (Ushuhuda wa Mharibifu wa Kiuchumi) ambamo John Perkins, Mmarekani ambaye alitumia sehemu kubwa ya maisha yake kufanya ulaghai wa kijasusi kuhujumu uchumi wa mataifa mbalimbali, hasa ya Dunia ya Tatu.
Perkins anasema katika Dibaji: “Waharibifu ama wapigaji wa kiuchumi ni wataalamu wanaolipwa fedha nyingi kuzihadaa nchi mbalimbali ulimwenguni na kuvuna matrilioni ya dola. Wanachukua fedha nyingi kutoka Benki ya Dunia, Shirika la Kimataifa la Misaada la Marekani (USAID), na mashirika mengine ya ‘misaada’ ya kimataifa na kuyaingiza taasisi kubwa na mifuko ya matajiri wanaomiliki rasilimali za dunia hii. Silaha zao ni kuangalia ripoti za kifisadi za fedha, chaguzi zenye utata, malipo yasiyo rasmi, utesaji, ngono, na mauaji. Wanacheza mchezo wa kale ambao umekuwa kama himaya, lakini ambao umegeuka kuwa wa kutisha hasa katika kipindi cha utandawazi.”
Yapo mengi ambayo anayazungumza, lakini kubwa ni mbinu wanazotumia kuzirubuni nchi zinazoendelea (hii ikiwa na maana na Tanzania) ili kuchota rasilimali zilizopo.
Perkins, ambaye alikuwa jasusi wa Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA), anasema mara nyingi wanachokifanya ni kwenda kutoa misaada na mikopo kwa nchi hizo kwa kujenga miundombinu ya barabara, viwanda, nishati na maeneo ya maegesho.
Mara nyingi, anasema, mambo wanayoyafanya yanakuwa yale ambayo yatawasaidia matajiri wachache na siyo wananchi walio wengi ambao hawapati umeme wala miundombinu mingine, kwa kifupi misaada hiyo haiwasaidii wananchi walio wengi.
Anasema, misaada na mikopo hiyo 'yenye masharti nafuu' kwa nchi hasa zenye utajiri wa rasilimali mbalimbali ikiwemo mafuta, inakuwa mikubwa na madeni yanazidi kiasi kwamba nchi husika inashindwa kulipa.
Ikishafikia hatua hiyo, anasema, wanarudi hapo na kuwashawishi viongozi wakisema: "Tazama, deni hili ni kubwa, hamuwezi kulilipa, tuachieni tuchimbe mafuta, madini au rasilimali nyingine muhimu kufidia deni hilo kwa malipo madogo sana".
huwezi kuwatambua waharibifu hao wa kiuchumi, kwa sababu ama wanaweza kuja kwa mgongo mwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ama maofisa waubalozi wanaofahamika kama Mwambata wa Kiuchumi (Economic Attache).
Katika baadhi ya mataifa, wanaposhindwa kufanikisha malengo yao kutokana na ugumu wa viongozi, wanaweza kuwatumia harakati za vyombo vya habari kueneza propaganda kwamba serikali fulani haifai, au la wanaweza ‘kuwapoteza’ (kuwaua) viongozi wanaoonekana kikwazo kwa kuwatumia wauaji ambao wanafahamika kwa jina la ‘mbweha’ (jackals) ambao nao huwa ubalozini kama maofisa wa usalama. Ikishindikana kabisa, basi hupeleka majeshi katika mataifa hayo.
Mbinu hizi hazitumiwi na na CIA peke yake, bali mataifa mengi yanafanya ujasusi wa aina hii wa kiuchumi kwa nia na madhubuni ya kukomba rasilimali za mataifa yanayoendelea huku wakija na kisingizio la misaada na mikopo kwa shughuli za maendeleo ya kijamii, mara nyingi fedha hizo huwa hazitolewi taslimu.
Nilikuwa napitia mistari mbalimbali kwenye kitabu hiki ndipo nikakumbuka kwamba deni la taifa hadi kufikia Desemba 2014 ni Shs. 27.04 trilioni (Shs. 20.23 trilioni ni deni la nje na Shs. 6.81 trilioni ni deni la ndani) ambapo kwa hesabu ya haraka, kila Mtanzania kati ya watu milioni 45, haijalishi kama ni mtoto au mzee, anadaiwa Shs. 600,000/-.
Japokuwa serikali inajipa moyo kwamba deni hilo asilimia 28, hivyo bado inakopesheka kwa kuwa kiwango cha ukomo wa kukopa ni asilimia 50, bado inatia mashaka kama linaweza kulipwa leo au kesho.
Tanzania ni moja ya mataifa yanayoendelea na yenye rasilimali nyingi ambazo kwa miaka mingi zinachotwa na kupelekwa nje huku Watanzania wakiwa hawanufaiki na wakiendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini.
Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) nayo ni mengi mno Tanzania, yapo yanayojishughulisha moja kwa moja na jamii, lakini yapo mengine ambayo kazi zao ni za kiharakati zaidi na hutegea kama kuna hoja yenye kutatiza na kutoa matamko ama kuhamasisha wananchi wapinge.
Kwa sasa Tanzania imekuwa kivutio cha uwekezaji kwa mataifa makubwa kama Marekani, Uingereza, China, India na kadhalika.
Ugomvi mkubwa wa uwekezaji nchini Tanzania ni baina ya Marekani na China, ambayo inakuja kasi sana.
Marekani, ambayo ilikuwa inaongoza kwa uwekezaji, hivi sasa inashika nafasi ya tano nyuma ya Uingereza, China, India na Kenya.
Hadi kufikia mwaka 2012, uwekezaji wa moja kwa moja wa Marekani nchini Tanzania ulikuwa Dola 950 milioni, wakati Uingereza ilikuwa inaongoza kwa kuwekeza jumla ya Dola 4.7 bilioni kutokana na makampuni ya BG Group Plc lililojikita kwenye gesi asilia na mafuta pamoja na kampuni ya SABMiller Plc, India ilikuwa imewekeza Dola 1.8 bilioni, wakati Kenya imewekeza Dola 1.5 na China ilikuwa imewekeza Dola 1.4 bilioni.
Lakini kwa sasa, inaonekana China inakaribia kuipita Uingereza kwenye uwekezaji kutokana na kuingia mikataba mingi hivi karibuni.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania, hadi kufikia Agosti 2013, kulikuwa na kampuni 300 za Kichina zilizowekeza moja kwa moja nchini Tanzania (Foreign Direct Investment) katika maeneo ya miundombinu, kilimo, viwanda na ujasiriamali mdogo na wa kati (SME) zote kwa pamoja zikiwa na mtaji wa zaidi ya Dola 2.1 bilioni.
Kampuni za Kichina zimepata mikataba mingi ya ujenzi ambapo kwa mujibu wa taarifa kutoka Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, kampuni 14 kutoka China zimeingia jumla ya mikataba 58 ya ujenzi wa kilometa 3,140.85 yenye thamani ya Dola 1.75 bilioni.
Kwenye upande wa madini, hasa ya mkaa ya mawe na chuma, China imeingia mkataba wa Dola 3 bilioni (takriban Shs. 6 trilioni) kupitia kampuni yake ya Sichuan Hongda ambao utadumu kwa zaidi ya miaka 100.
Rasilimali kubwa za Tanzania ni madini na maliasili (wanyama mwitu), lakini hivi sasa kuna suala kubwa la ugunduzi wa mafuta na gesi.
Ukiacha madini kama dhahabu, almasi na tanzanite ambayo yamechimbwa na kupelekwa nje kiasi cha kuacha mahandaki tele huku wananchi wakiwa maskini, lakini kuna madini ya uranium ambayo ni muhimu sana kiuchumi na tayari yamekwishaanza kuchimbwa na Serikali ya Urusi huko Mkuju, wilayani Namtumbo.
Suala la mafuta na gesi linanifikirisha sana nikirejea maelezo ya Perkins, kwani tangu mwaka 2013 tumeshuhudia mvutano mkubwa baina ya Serikali na wawekezaji, hasa wa ndani, kuhusiana na suala la vitalu.
Hili bado halijakaa sawa kwa sababu serikali inashikilia msimamo wake wa kuwaalika wawekezai kutoka nje na kusema wazawa hawana uwezo.
Kwa misingi ya mbinu za kijasusi za waharibifu wa kiuchumi (economic hit men), suala la mafuta na gesi lina umuhimu mkubwa kuliangalia kiusalama hasa tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015.
Kama ushuhuda wa Perkins unavyosema, Tanzania haiko salama kwa rasilimali zilizopo kwa sababu tunaamini kabisa kwamba mataifa makubwa yanapigana vikumbo yenyewe kwa yenyewe kutaka kuwekeza hapa.
Ni katika vikumbo hivyo ambamo wanaweza kuwemo akina CIA, KGB na hata MI6 na wote wanapotajwa kuhusishwa na mambo mazito kama haya, kauli mbiu yao inatofautiana kidogo, nayo ni Usikiri Chochote, Kanusha Kila Kitu, Toa Tuhuma Nyingi (Admit Nothing, Deny Everything, Make Counter Accusations).
Mwaka 1982 ilishuhudiwa mabadiliko ya uongozi yaliyofanyika nchini Australia ambayo yalifanikishwa zaidi na Benki ya Nugan Hand. Hadithi yao na jinsi walivyouawa, haina nafasi leo hii hapa.
Lakini kuondolewa madarakani wa Hugo Chavez wa Venezuela tunatambua kwamba ilikuwa ni vita ya mafuta.
Tanzania hatuwezi tukawa salama zaidi hasa kama majasusi wa mataifa mengine watatumia harakati za uchaguzi mkuu wa mwaka huu kutaka kupenyeza ‘watu wao’ watakaolinda maslahi yao ili wawekeze kwenye mafuta na gesi.
Badala ya kushangilia umati mkubwa wa watu kwenye mikutano ya Ukawa na Chama cha Mapinduzi, ni vyema vyombo vya usalama vifanye jitihada za kuchunguza kama kuna chochote ama yeyote nyuma ya uchaguzi huu, iwe kwa vyama ama wagombea mmoja mmoja.
Si mara moja au mara mbili tumewahi kufutiwa madeni yetu ‘yasiyolipika’ na tukaendelea na ushirikiano na nchi husika. Je, kuna chakula cha bure duniani au ndiyo mbinu anazozisema Perkins kwamba wanafanya hivyo ili kuchota maliasili katika nchi zinazoendelea?
Uzalendo kwanza.
0656-331974

NB: Makala haya yalichapwa kwa mara ya kwanza na gazeti la WAJIBIKA la Septemba 14, 2015.

No comments:

Post a Comment