Dk. Slaa
Na Daniel Mbega
WASWAHILI
wanasema, ‘Msemea sikioni, siyo majinuni’!
Maana yake ni kwamba, yeyote anayekunong’oneza kuhusu jambo fulani, katu siyo
mjinga.
Septemba
Mosi, 2015, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, aliibuka
baada ya ukimya wa mwezi mmoja na kueleza msimamo wake katika siasa na mambo
yaliyomfanya akimbie.
Katika
mkutano huo uliofanyika kwa muda wa saa 1:30 kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar
es Salaam, Dk. Slaa, pamoja na mambo mengine, alieleza namna mchakato wa
kumkaribisha Edward Lowassa ndani ya Chadema na hatimaye Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) ulivyogubikwa na hila kutoka kwa viongozi wa chama chake.
Aliwatuhumu
viongozi wake hao kuuchakachua mchakato na hata hoja alizozitoa, ikiwemo kupewa
orodha ya watu ambao Lowassa aliokuwa anakwenda nao Chadema, ilizimwa huku
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Profesa Abdallah Safari,
akiichana barua yake ya kujiuzulu aliyomkabidhi.
Kubwa
zaidi lililoleta mtikisiko ni maelezo ya Dk. Slaa kwamba, kumbe mchakato wote
huo ulifanywa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ambaye
Slaa mwenyewe anamwita ‘mshenga’.
Alimnukuu
Gwajima akimshawishi amkubali Lowassa kwa vile anakubalika na Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na kwamba maaskofu 30 kati ya 34 wa
Kanisa Katoliki walikuwa wamelambishwa sukari guru na wanamkubali.
Hali hiyo
ndiyo iliyozusha mtafakaruku mkubwa wa kisiasa ambao wapinzani waliuelezea
kwamba una lengo la kuligawa taifa.
Slaa
hakuwa majinuni alipotoa tuhuma hizo. Alikuwa sober, hakuwa amekunywa kileo wala hakuwa anaumwa, tena
hakulazimishwa na yeyote… alimaanisha alichokuwa anakisema.
Hata
hivyo, Septemba 8, 2015 Askofu Gwajima naye aliibuka kujibu mapigo ya tuhuma za
Dk. Slaa, akisema kwamba Paroko huyo mstaafu wa Kanisa Katoliki hana hoja kwa
sababu ‘ametekwa na mkewe’ ambaye alitamani sana kuwa ‘Mke Namba Moja wa
Tanzania’ (First Lady).
Akasema,
siku Lowassa alipopokelewa Chadema, Dk. Slaa alitupiwa nguo nje na mkewe na
kwamba alilala kwenye gari huku kitendo hicho kikishuhudiwa na walinzi, ambao
yeye Gwajima ndiye aliyempatia Slaa ingawa walikuwa wanalipwa na Chadema.
Gwajima
ameruka futi 100 kwamba hajawahi kumweleza Dk. Slaa kwamba kuna maaskofu 30
waliohongwa, hivyo maneno hayo ni ya kutungwa.
“Dk Slaa
anasingizia kuwa maaskofu 30 wamehongwa na Lowassa, hii ni kuwaondolea maaskofu
kuaminika (credibility) ili waonekane
kuwa hawafai,” alisema Gwajima na kuongeza kuwa; “Maaskofu Wakatoliki
hawakupewa rushwa, maaskofu wa KKKT hawakupewa rushwa, mimi sikupewa rushwa.”
Ukiangalia
mambo yanayoendelea unaweza kusema hizi ni ngonjera ama malumbano na majigambo,
sanaa ambazo zimetoweka nchini mwetu kwa vile mitaala imebumundwa na wajanja na
Kiswahili kinaelekea kupoteza misingi hata shuleni.
Dk. Slaa
alikwishasema kwamba alikuwa anamsubiri kwanza Gwajima ajibu, halafu atarejea
kumwaga mboga na kulivunja kabisa jungu.
Lakini
naye Gwajima, wakati alijibu tuhuma hizo, akasema Dk. Slaa anatumiwa na kuonya
kwamba kama atajibu hayo, basin aye atarejea tena kueleza kila kitu ambacho Dk.
Slaa alikifanya akiwa Afrika Kusini na vijana wa Usalama wa Taifa kabla
hajarejea na kushusha tuhuma.
Wakati
alipojitokeza kwa mara ya kwanza baada ya ukimya mkubwa Agosti 3, 2015, Dk.
Slaa alisema kwamba, ujio wa Lowassa kwenye Chadema na Ukawa bado una harufu ya
ufisadi, kwani fedha zinazotumika, ambazo zimeingizwa huko ni za mafisadi wale
wale waliokuwa kwenye Orodha ya Mafisadi, lakini akakanusha kwamba hafanyi
hivyo kwa kukosa nafasi ya kugombea urais.
“Kwangu mimi kuingia Ikulu ni tunda la lengo
kuu ambalo ni kurudisha maadili ndani ya nchi hii. Nani hajaona matumizi ya
rushwa kwenye mchakato wa Lowassa kutafuta wadhamini? Leo fedha zinazotumika ni
za kina Rostam Aziz – wale wale ambao tukisimama jukwaani tumekuwa tukiwaita
mafisadi. Nimeheshimu na kutii dhamira yangu kwa kuwa naamini Mungu huzungumza
nasi kupitia dhamira zetu,” alisema Dk. Slaa.
Kauli inayofanana na hiyo ilitolewa pia na
aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Agosti 6, 2015 wakati
akijiuzulu: “Nawaomba radhi sana wanachama na wananchi walioniamini na
kuonyesha mapenzi makubwa kwangu na uongozi wangu. Nimeshiriki vikao vya Ukawa
vilivyotufikisha hapa. Hata hivyo, dhamira na nafsi yangu inanisuta kuwa katika
uamuzi wetu tumeshindwa kuenzi na kuzingatia tunu za Taifa za utu, uzalendo,
uadilifu, umoja, uwazi na uwajibikaji.”
Binafsi
naona hapa bado kuna hoja muhimu zinazohitaji kujadiliwa, kwa kina. Gwajima na
Dk. Slaa wanatuchezesha shere tu kutuchelewesha, na wanaweza wakayumbisha
mawazo ya Watanzania wasisikilize Sera zinazotolewa na wanasiasa kwa
mustakabali wa taifa letu wabaki wakijadili vitendawili ambavyo haviteguliki.
Kwa
kuzingatia maelezo ya Gwajima, naamini Dk. Slaa atakuwa ‘amepewa mji’ kwani
inaonekana Gwajima hakujibu hoja zilizotolewa, na inawezekana hajui siri ambazo
Dk. Slaa alisema anazo kuhusiana, kwanza na Lowassa na ushiriki wake kwenye
Richmond, lakini pia kuhusiana na Frederick Sumaye, Meneja wa Kampeni wa
Lowassa ambaye naye amejiunga Chadema hivi karibuni.
Dk. Slaa
umelipasua jipu, lakini kwa nini linakushinda kulikamua? Unadhani kwa kutoa
tuhuma na kuziacha zinaelea bila kueleza kwa undani utakuwa unawatendea haki
unaowatuhumu ama hata Watanzania kwa ujumla wao ambao pengine hawajui kilicho
nyuma ya pazia?
Gwajima
ameshindwa kutegua kitendawili chako, sasa rudi kutoka huko Marekani uje
utupatie jibu, kwani ulisema kwamba, ulikuwa unamsubiri ajibu zile za awali
ndipo ushuke.
Shuka sasa
na ‘silaha zako za maangamizi’ ili Watanzania wapime, watafakari na waamue
lililo la haki.
Kukaa
kimya kunazidi kuzalisha maswali mengi, hivyo njoo upesi utupe jibu la
kitendawili… na ulikamua jipu ulilolipasua, maana bado linauma!
Wasalaam.
0656-331974
NB: Makala haya yalichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la WAJIBIKA la Septemba 14, 2015.
No comments:
Post a Comment