Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 18 September 2015

NYERERE ALISEMA...HAKUNA TAJIRI MZURI WALA MBAYA, MATAJIRI WOTE NI WEZI!

 
Mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe, lakini mtaji wa tajiri ni jasho la maskini!



Na Daniel Mbega
“Siku zote tajiri ndiye atakayeamua huyu alipwe mshahara kiasi gani, huyu apate kiasi gani. Na itaendelea kuwa hivyo mpaka wafanyakazi tena wamgomee, waje juu waseme; “Wewe siyo tajiri mzuri!” Sijui kama kuna tajiri mzuri na tajiri mbaya, na hivyo nawaambieni kwamba hakuna tajiri mzuri, tajiri wote ni wezi!”
Hii ni sehemu ya hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere akihutubia wafanyakazi katika sherehe za Mei Mosi. Sikumbuki ni lini.
Hata hivyo, maneno haya yamenifanya nitafakari sana mambo yanayoendelea katika siasa za nchi yetu, hususan za vyama vingi, tangu mfumo huo ulipoanza Julai Mosi, 1992.
Nakumbuka mwaka 1995 wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi kulikuwa na wagombea urais wanne. Kila mgombea alikuja na kauli mbiu yake: Benjamin Mkapa wa CCM alikuja na kauli mbiu ya ‘Ukweli na Uwazi’; Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF (Haki Sawa Kwa Wote); Augustine Mrema wa NCCR (Mageuzi); na John Cheyo wa UDP (Kuwajaza Wananchi Mapesa) kauli mbiu ambayo ilimfanya apachikwe jina la ‘Bwana Mapesa’.
Ni kauli mbiu ya Cheyo ya ‘kuwajaza watu mapesa’ ambayo ilikuwa imewavutia wananchi wengi na kumpatia umaarufu mkubwa kiasi kwamba wananchi wa kawaida walihisi huyo ndiye mkombozi wao.
Pengine kwa sababu tu hakuwahi kuchaguliwa ndiyo maana ‘mapesa’ hayo hayakuweza kupatikana, lakini Cheyo kwa miaka 10 aliyokaa Bungeni tangu mwaka 2005 hadi 2015 ameshindwa hata kuwajaza mapesa wananchi wa Jimbo la Bariadi Mashariki (sasa Itilima).
Kauli ya Cheyo haina tofauti na ile ya mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.
Mimi si mwanasiasa, ingawa ninapenda siasa. Hakuna mwanasiasa anayependa siasa, wote wanapenda madaraka! Najaribu tu kuchambua kwa kutumia taaluma yangu.
Tangu alipotangaza nia yake ya kuwania urais kupitia CCM, kauli kubwa ya Lowassa imekuwa kuuchukia umaskini na kutamani kila Mtanzania awe tajiri kama walivyo akina Said Bakhressa, Reginald Mengi, Nazir Karamagi na wengineo, kwa kuwataja wachache.
I hate (nachukia) umaskini. Nataka uongozi ili kuwaondoa Watanzania katika umaskini. Kama mtu amepata utajiri kwa njia za uhalali, amejinyima, ni nzuri sana. Nachukia watu wanaopata fedha na kuishia katika ulevi na wanawake. Kina mama mnisamehe. Sitaki kupata uongozi kwa kudanganya, nachukia umaskini.”
Hata alipokwenda Chadema, Lowassa ameendelea kuinadi Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho kwa kurejea kauli yake ya kuuchukia umaskini. Hili ni jambo jema sana kwa kiongozi, maana kwa kuuchukia kwake umaskini, hawezi kuona jamii ikiwa maskini.
Hata hivyo, kauli hiyo inatia mashaka kutokana na ukweli kwamba, hizo ni ndoto za mchana na maneno matamu ya wanasiasa ili tu wapate madaraka.
Lowassa ni mwanasiasa kama wanasiasa wengine, tena amesomea sanaa za maonyesho (performing arts) Chuo Kikuu. Tunafahamu wasanii ambavyo wanaweza wakafanya ‘accapela’ kwa kumwaga machozi hadharani hata kama hakuna cha kuwaliza!
Kama alivyosema Mwalimu Nyerere katika hotuba yake hiyo, hakuna tajiri mzuri, tajiri wote ni wezi. Tena basi hakuna tajiri ambaye yuko tayari kuona utajiri wake unatishiwa, atafanya kila njia kuulinda – kwa gharama yoyote iwayo.
Matajiri wengi ni wanyonyaji wakubwa. Wanapenda kuwafanyisha watu kazi ngumu kwa ujira mdogo, na ndiyo sababu ya kuanzishwa kwa vyama vya wafanyakazi duniani ili kutetea na kudai maslahi bora zaidi kwa kazi wanazozifanya.
Mwalimu Nyerere alikuwa muumini wa harakati za wafanyakazi na wakulima. Alikuwa mjamaa, siasa ambayo wajanja waliizika kule Zanzibar. Mwalimu alikuwa mpigania ukombozi wa binadamu. Alikuwa anapinga dhuluma na ukandamizwaji. Ujamaa ni imani, ndivyo alivyoamini Mwalimu. Lakini ubepari ni mfumo, si imani.
Matajiri wote, kwa kutafsiri kauli ya Mwalimu Nyerere, ni mabepari na ili mfumo wa ubepari uendelee hakuna budi bepari ajilimbikize mtaji unaotokana na ziada anayonyonya kutoka kwa wafanyakazi ambao ataendelea kuwekeza ili aendelee kuwanyonya wavujajasho.
Viwango vya ubepari vinatofautiana kulingana na nchi yenyewe. Viwango hivyo ni kama vifuatavyo:
Ubepari wa uangalizi: Kwa Kifaransa inajulikana kama Laissez-faire. Huu ni mfumo ambao masuala yote ya uchumi yako mikononi mwa sekta binafsi ambayo haiingiliwi na serikali katika kupanga sheria, taratibu, vipaumbele, kodi na hata mgawanyo wa mapato. Sekta binafsi ndiyo inayosimamia mfumo wote na kazi ya serikali ni kuangalia tu.
Ubepari wa Ustawi (Welfare capitalism): Ni utaratibu wa mabepari kutoa huduma za kijamii kwa wafanyakazi wao na ulikuwa umeanzishwa kwa nchi za viwanda ambako waliajiriwa watu wenye ujuzi tu. Mfumo huu ulikua zaidi katikati ya karne ya 20. Hapa Tanzania ni ndoto kwa mfumo huu kutumika kwa sababu viwanda vyote vimekufa, mashirika ya umma yameuzwa, mabepari wenye viwanda nchini ndio wanaoongoza kwa kulipa ujira mdogo kwa wafanyakazi, tena basi wanapenda zaidi kuwa na vibarua, wenye elimu ndogo. Mtu yeyote mwenye ujuzi hawezi kuajiriwa kwenye viwanda vya mabepari wa Tanzania kwa sababu wanaogopa kwamba hawa ni wasomi, wanajua haki zao na wanaweza kuwasumbua baadaye.
Ubepari wa uswahiba (Crony capitalism): Huu ni mfumo unaoelezea uchumi kwamba kukua kwa biashara kunategemea urafiki wa karibu uliopo baina ya mabepari (wafanyabiashara wakubwa) na viongozi walioko madarakani. Huu unaongozwa na upendeleo zaidi wa maofisa wa serikali kwa mabepari hao ambapo hutoa vibali, ruzuku za serikali, misamaha ya kodi pamoja na upendeleo mwingine. Mfumo huu ndio unaotumika hapa nchini.
Ubepari wa Dola (State capitalism): Ni mfumo wa uchumi ambamo shughuli zote za biashara zenye tija zinasimamiwa na Dola, ambamo njia za uzalishaji mali zinapangwa na kusimamiwa kama njia za biashara, zikiwemo za ukuzaji wa mitaji, ujira kwa wafanyakazi, na usimamizi. Mfumo huu ni mgumu kutumika hapa Tanzania kwa sababu serikali siyo mwajiri mkubwa tena kama ilivyokuwa zamani, bali sekta binafsi ndiyo iliyoshika hatamu.
Lowassa anaposema anatamani Watanzania wawe matajiri ananishangaza hasa katika kipindi hiki ambacho ubeberu umegeuzwa jina na kuitwa ‘Uliberali mamboleo’ (Neo-Liberalism) au kwa lugha inayofahamika zaidi ni ‘Soko Huria’.
Kwa kuruhusu soko huria, serikali imelegeza masharti ya biashara ya nje na ndani na sasa haiwezi kudhibiti tena biashara. Wafanyabiashara wanajipangia wenyewe bei, serikali haipaswi kuingilia, na madhara yake ndiyo ile migomo ya wafanyabiashara nchini ambayo inaendelea kwa kupinga kodi na mashine za kielektroniki.
Gharama za maisha zimepanda kwa Watanzania siyo kwa sababu serikali ni mbovu, ila ni kwa sababu ya soko huria. Kuilaumu moja kwa moja serikali wakati mwingine tunafanya makosa makubwa, lazima tuangalie nini chanzo.
Sekta za elimu, afya, maji na umeme zimebinafsishwa na sasa zimekuwa bidhaa ambazo wananchi wanapaswa kuzilipia, na siyo huduma za jamii tena zilizopaswa kutolewa bure.
Soko huria limeruhusu ujio wa wawekezaji kutoka nje na ndani, yote haya yakiwa ni masharti ya wafadhili na taasisi za kibeberu. Serikali imepoteza uwezo na haki yake ya kujiamulia mambo muhimu ya sera na mwelekeo wa nchi kwa faida ya watu wake. Hii si Tanzania peke yake, bali nchi zote ambazo zililazimishwa na mabepari hao ambapo hapa Tanzania Sera ya Ubinafsishaji ilianzishwa mwaka 1992. Lowassa analielewa hili vyema kwa sababu alikuwa ndani ya Baraza la Mawaziri, wakati huo akiwa na miaka 39!
Wakati wa utawala wa Mwalimu hakukuwepo na ufisadi, japokuwa kweli rushwa ilikuwepo. Mwalimu aliipigia kelele rushwa.
Tumejifunza tangu shuleni na kama nilivyoeleza hapo awali, ubepari ni mfumo wa uchumi ambamo biashara, viwanda na vitegauchumi vingine vinatawaliwa na watu binafsi kwa kiasi kikubwa na kwa lengo la kupata faida. Nafasi ya serikali ni ndogo, na vilevile lengo la kuhudumia jamii katika mahitaji yake haliongozi mipango.
Kwa kuwa Tanzania imeingia katika soko huria ambalo limeruhusu uliberali mamboleo ambao ndio ubepari wenyewe, pengine Lowassa angetueleza anawezaje kuondoa tabaka la maskini na kuwafanya matajiri halafu aseme ni kwa namna matajiri hao, akiwemo yeye mwenyewe, watakuwa salama.
Lowassa atueleze, kati ya viwango hivi vinne vya ubepari, ni kipi ambacho atakitumia kuwaletea utajiri Watanzania, kwa sababu hakuna ubishi kwamba yeye hawezi kuufuta ubepari kamwe na sifa za ubepari tunazijua.


0656-331974

NB: MAKALA HAYA YALICHAPWA KWA MARA YA KWANZA NA GAZETI LA MWANANCHI SEPTEMBA 16, 2015 INGAWA HAPA IMEREKEBISHWA KIDOGO.

No comments:

Post a Comment