Ndege aina ya Hustlers Jet ambayo Ruto aliitumia.
Na Daniel Mbega
JUMANNE ya Agosti 4, 2015
wabunge wa Jubilee nchini Kenya waliamua kwa ‘nia moja’ kumsafisha na kumtakasa
Makamu wa Rais William Kipchirchir
Samoei arap Ruto baada ya kuitupilia mbali ripoti
ya uchunguzi kuhusu ubadhirifu wa fedha za umma kuhusiana na ndege aliyotumia kiongozi
huyo kutembelea mataifa kadhaa mnamo 2013.
Uchunguzi huo ulikuwa unafanywa
dhidi ya kashfa ya ukodishaji wa ndege hiyo maarufu kama “Hustler’s Jet”
ambapo mamilioni ya fedha za umma yalitumika.
Uamuzi wa kuitupilia mbali
ripoti hiyo ukawaacha midomo wazi wabunge wa upinzani na baadhi ya wanachama wa
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ambayo kwa mujibu wa ratiba ya
Bunge, ripoti hiyo ilikuwa miongoni mwa miswada kadhaa ambayo ilipaswa kupigiwa
kura baada ya mjadala kuihusu kukamilika Julai 30, 2015.
Lakini kwa mshangao mkubwa,
ripoti hiyo ilijadiliwa haraka haraka kabla ya kutupiliwa mbali, licha ya
kuwasilishwa bungeni tangu Aprili 2014. Ripoti hiyo ilikuwa ikimlaumu Rais Uhuru
Kenyatta kwa kumwagiza Ruto kusafiri katika mataifa manne, mwezi mmoja tu baada
ya serikali yake kuingia madarakani.
Mbunge wa Suba John Mbadi,
ambaye pia ni mwenyekiti wa ODM alisema kulikuwa na njama za siri kuhusu jinsi
ripoti hiyo ilivyojadiliwa. “Haiwezekani ripoti iliyokaa katika Bunge kwa
karibu mwaka mmoja kutupiliwa mbali huku mjadala wake ukionekana kutotiliwa
maanani. Ni kana kwamba kuna mtu anayelengwa kulindwa na ripoti hii.”
Ruto alisafiri katika mataifa
ya Congo Brazaville, Ghana, Nigeria na Gabon kati ya Mei 16 na 19, 2013. Uchunguzi
wa ripoti hiyo ulionyesha kuwa jumla ya Shilingi za Kenya 18.9 milioni (takriban
TShs. 369.6 milioni) zilitumika katika ziara hiyo, wakati ambapo stakabadhi
zilionyesha kuwa zilizotumika ni KShs. 100 milioni (TShs. 1.9 bilioni).
Wanasiasa wa Kenya wanasema,
hatua hiyo ni njama za kumsafisha Ruto katika kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa
mwaka 2017 nchini Kenya.
Ruto amekuwa na kashfa nyingi
huko Kenya. Mwaka 2009 akiwa Waziri wa Kilimo alikumbwa na kashfa ya ubadhirifu
wa mahindi kiasi cha maguni milioni moja kati ya milioni 2.6 ambayo yalipaswa
kutolewa kama msaada kutokana na baa la njaa. Yeye akasema alikuwa anachafuliwa
kisiasa.
Agosti 24, 2011 ‘alitimuliwa’
kazi akiwa Waziri wa Elimu ya Juu, katika kipindi ambacho alikuwa amejiuzulu kupisha
uchunguzi kuhusu kashfa iliyokuwa inamkabili ya kununua jengo la ubalozi wa
Kenya mjini Tokyo.
Oktoba 2012 alitajwa katika
kashfa ya kuuza sehemu ya Msitu wa Ngong kwa kampuni ya Kenya Pipelines Limited
(KPC) kwa kiasi cha KShs. 272 milioni (takriban TShs. 5.3 bilioni) na kwamba
alikuwa akipokea kiasi cha KShs. 96 milioni (TShs. 1.9 bilioni) kwa vipindi
tofauti.
Lakini pamoja na yote hayo,
alichaguliwa kuwa makamu wa rais katika uchaguzi wa mwaka 2013! Kweli Wabantu wanaugua
ugonjwa wa Epodomia kama Mchungaji Christopher Mtikila anavyosema.
Nilikuwa natafakari namna
wabunge wa Jubilee walivyomtakasa Ruto na jinsi ilivyotokea kwa viongozi wa
vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walivyofanya kwa Edward
Lowassa wakati wanampokea akitokea Chama cha Mapinduzi (CCM) alikoenguliwa
kuwania urais.
Ni wapinzani hao hao ambao
tangu Septemba 15, 2007 walimtangaza Lowassa kuwa fisadi miongoni mwa mafisadi
11 wanaoliangamiza taifa. Wakapita kila kona ya Tanzania kwa kutumia
‘Operesheni Sangara’ na baadaye ‘Vuguvugu la Mabadiliko’ (Movement for Change) kunadi
sera yao ya mapambano dhidi ya ufisadi.
Hao hao wapinzani walikuwa
wakiisubiria tu CCM kwenye kona kama ingemsimamisha Lowassa kugombea, ili
wafumue ufisadi wake ulivyo.
Lakini ghafla bin vuu, kwa
kutegemea kwamba mwanasiasa huyo atairahisisha safari yao ya kuingia Magogoni
Oktoba mwaka huu, wakasema Lowassa ni msafi na anafaa kuliongoza taifa hili.
Wamewalisha watu sifongo
inayoonekana tamu mdomoni lakini chungu tumboni, kwa kuwafanya hivi sasa wavae
miwani ya mbao na kuziba masikio kwa gundi wasione wala kusikia kila baya
linalotajwa kumhusu Lowassa.
Kila ninapoandika makala
kuzungumzia hoja mbalimbali za uadilifu wa Lowassa, nimekuwa nikipokea simu za
vitisho na matusi mengi. Sijali, kwa sababu ninaongozwa na uzalendo kwa nchi
yangu pamoja na maadili ya taaluma yangu.
Nikiwahoji hao wanaoshabikia,
hawana hoja yoyote zaidi ya kusema wanataka mabadiliko tu. Hawaitaki CCM kwa
sababu imekaa madarakani kwa miaka mingi.
Huwa napenda kuwaambia watu
kwamba, Hakuna anayemwacha mke kwa sababu
ya mwanamke mwingine, isipokuwa tu ni kwamba hajaweza kuelewana na mkewe
ndiyo maana anamwacha. Huwezi kusema mkeo kwa sababu amekuwa mzee, basi umwache
ukaoe mwingine eti tu kwa sababu huyu umeishi naye miaka mingi, amezeeka.
Nasikitika kusema kwamba huo ni upumbavu na uendawazimu. Hakuna imani ya dini
inayoelekeza hivyo.
Wapinzani wanamtakasa Lowassa
kwa wimbo ule ule usio na kiitikio “CCM imeshindwa kuleta unafuu wa maisha kwa
Watanzania.”
Kila mmoja anapenda mabadiliko
yenye neema, lakini lazima kuwe na sababu. Hawa mashabiki wanaofuata mkumbo
kama panzi kwenye safari ya nzige ni lazima wakae chini watafakari, lakini siyo
kila wanapoona maandiko yanayomgusa Lowassa kwa mtazamo hasi wanaanza kung’aka.
Tafsiri ya neno ‘Mpinzani’ iko
wazi kabisa. Ni mtu anayepinga, anakwenda kinyume na kile kilichopo, kwa nia na
madhumuni ya kutaka afanikishe mambo yake – yawe ya heri au shari!
Siasa za upinzani ni nzuri
zikifanywa kwa kuzingatia ukweli wa mambo. Chadema ilipata nguvu zaidi kutokana
na sera ya kupiga vita ufisadi kwa vitendo, kwa kufichua kashfa nyingi ambazo
zimeiyumbisha serikali mpaka ikafanya mabadiliko ya baraza la mawaziri. Haya ni
mafanikio.
Lakini Chadema ninayoiona sasa
siyo ile ya mwaka 2007 hadi 2010, ni chama kingine tofauti kabisa.
Kumtakasa Lowassa kwa kashfa
moja tu ya Richmond, ambayo hata hivyo inayo maswali mengi ya kujiuliza,
kunawaharibia, kwa sababu zipo kashfa nyingine kadha wa kadha ambazo anastahili
kuzijibu, achilia mbali maelezo yake ya ‘utetezi’ wa Richmond kutotosheleza.
Tanzania ni nchi yetu sote.
Uamuzi wa leo ndio unaoweza kuwa msingi wa taifa la kesho. Tukijenga msingi
mbovu tusijilaumu nyumba itakapoporomoka.
0656-331974
No comments:
Post a Comment