
Meru: VYOMBO vya habari vimetakiwa kutumia fursa na wajibu wake kutangaza matatizo mbalimbali yanayowakabili wanafunzi, vijana wa kwenye vituo na wale wa mtaani.
Mpaka sasa bado changamoto ambazo zinawakumba vijana ni nyingi sana na wenyewe pamoja na wazazi wao kamwe hawataweza kutatua ila kwa kutumia vyombo vya habari wataweza kusaidika.
Hayo yameelezwa na mratibu wa shirika la FARM RADIO Goodlove Nderingo wakati wa uzinduzi wa kampeni shirikishi kwa radio ambapo uzinduzi huo ulifanyika hivi karibuni kwenye shule ya sekondari Singisi iliopo Meru mkoani hapa.
Nderingo alisema kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa sana ya kusaidia vijana hasa kwa nyakati kama hizi ambazo kuna changamoto mbalimbali ambazo zinaanzia kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.
Alidai kuwa kama waandishi wa habari wataweza kuwatembelea vijana na kisha kubainisha changamoto ambazo wanazo basi vijana wataendelea kupata mambo mbalimbali yakiwemo elimu ambayo itawasaidia kwenye maisha yao ya kila siku.
“Kwa mfano kama sisi hapa huwa tunashirikiana na vyombo vya habari vingi sana hapa nchini na tunataka watanzania waweze kuelimika kupitia elimu ambazo tunazitoa sasa ni jukumu hata kwa wale ambao hatushirikiani nao basi na wao waweze kuangalia namna ambayo watawasaidia vijana," aliongeza Nderingo.
Alidai kuwa kwa sasa ili kuweza kuwasaidia vijana wa mkoa wa Arusha wanatoa elimu mbalimbali kupitia katika kituo cha matangazo cha Radio Five kilichopo jijini hapa ambapo elimu hiyo inatolewa chini ya mradi huo unalenga kusaidia vijana kutambua afya ya akili pamoja na madhara yake.
Akiongelea mradi huo ambao umezinduliwa alisema kuwa tayari umeanza kutoka mwezi Septemba na utaweza kunufaisha shule 35 za Wilaya ya Arusha Vijijini lakini pia Meru huku vijana 10,000 watapata elimu ya afya ya akili.
Naye mwakilishi wa walimu ambaye ni Slyvester Paul aliongeza kuwa pamoja na kuwa vyombo vya habari hapa nchini vina mchango sana kwenye kutatua changamoto za vijana lakini pia mpango huo wakuwelimisha jamii kuhusiana na afya ya akili pamoja na walengwa wenyewe ambao ni vijana na wanafunzi wa shule kutaweza kupunguza matatizo mbalimbali ambayo yamo kwenye jamii.
Paul alibainisha kuwa hata kwa upande wa walimu nao wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanajijengea tabia ya kuwasoma wanafunzi wao hasa wanapobadilika kwani wakati mwingine yapo baadhi ya matatizo ambayo yanasababisha hata wanafunzi hao kubadilika.
“Kama tunavyojua sisi walimu ni kama wazazi na sisi ndio tunatumia muda mwingi kukaa na hawa watoto kwaiyo ni lazima tutambue sasa umuhimu wa afya ya akili ili mtoto anapopata matatizo au anapobadilika basi tuweze kumsaidia," aliongeza Paul.
No comments:
Post a Comment