Arusha: UPUNGUFU wa watumishi wa afya katika Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha umesababisha Daktari mmoja kuhudumia wagonjwa zaidi ya 10,000 kinyume na na viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO) vinavyoelekeza daktari mmoja kuhudumia wagonjwa 7,500.
Hayo yamebainika wakati wa mjadala ulioandaliwa na Taasisi ya Idadi ya Watu Duniani (DSW) kupitia mradi wake wa Health Action kwa kushirikiana na mashirika mengine ya kijamii kwa lengo la kuibua matatizo na kero katika sekta ya afya katika kata ya Leguruki Wilayani ya Arumeru.
"Tumetoa kilio cha tatizo hili la huduma za afya katika vijiji vyetu lakini hakuna hatua zilizochukuliwa kurekebisha mambo ili tupate huduma ya afya kama watanzania wengine hususan waishio mijini” alisema Ndeniengwasinga Joseph kutoka kijiji cha Shishtoni.
Alisema kuwa wananchi wa vijiji hivyo wamekuwa wakikosa huduma za afya pindi daktari huyo anapokuwa na dharura ya kutokuwepo kazini.
“Imekuwa ni kazi kubwa sana kwa daktari huyu wa hapa katika zahanati yetu ya Nkoasenga ,kuhudumia vijiji vitano vyenye watu wengi, ni jambo la muhimu kuletwa kwa daktari mmoja angalau wawe wawili,” alisema Anderson Sikawa Mkazi wa Leguruki.
Aidha Sikawa alieleza kuwa zahanati yao ya Nkoasenga haina majengo ya kutosha ikiwemo chumba cha kuhifadhi nmaiti na pia haitoi huduma zote na hivyo itakuwa bora ipandishwe hadhi na kuwa kituo cha afya ili kiweze kutoa huduma za kulaza wagonjwa.
Aliongeza kuwa wananchi wa vijiji hivyo wanalazimika kusafiri zaidi ya kilomita sitini kufuata huduma za afya katika hospitali ya Wilaya iliyopo Tengeru jambo ambalo limekuwa likiwagharimu fedha nyingi.
Wakizungumzia masuala ya afya ya uzazi baadhi ya wananchi hao walisema kuwa ufahamu mdogo kuhusu elimu ya afya ya uzazi na kwamba wao wanaishi kwa kufuata mila na desturi katika mambo ya uzazi.
“Mimi kama Mama naelewa umuhimu wa elimu ya afya ya uzazi na mpango wa uzazi lakini wakina mama wenzangu hapa kijijini hawafahamu na wala hakuna uelimishaji wowote unaofanyika kuhusu suala hilo," anasema Ndekirwa Sooi.
Alifahamaisha kuwa elimu ya uzazi ikitolewa katika jamii wanaume wengi watabadili mawazo na matendo yao,pia ushiriki wao utaondoa dhana potofu kuwa elimu ya afya ya uzazi na mpango wa uzazi huwahusu wanawake.
“Kutokana na Wanaume wengi kutopata elimu ya afya ya uzazi kumekuwa na ongezeko kubw ala watu katika kijiji chetu hivyo elimu hiyo ni muhimu ikatolewa kusaidia kupunguza kasi ya ongezeko la watu hapa,” alisema Sooi.
Meneja utetezi wa DSW-Tanzania, Manka Martin Kway,alisema kuwa mradi huu unatekelezwa kwa kushirikiana na wadau wengine ambao ni Women in Development for Science and Technology(WODSTA), Walio katika Mapambano na AIDs (WAMATA), Evangelical Lutheran Church of Tanzania-Selian (ELCT-Selian), Women and Child Vision (WOCHIVI), Pathfinder International (PI), Support for International Change (SIC) na Tumaini Positive (TUPO) chini ya Mradi ujulikanao kama Health Action unaolenga kuwajengea uwezo mashirika yasiyo ya kiserikali kufanya utetezi na ushawishi katika masuala ya afya.
No comments:
Post a Comment