Ripoti ya mwenendo wa mpira wa miguu Tanzania na mipango yake inayofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imemfurahisha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye hivyo moja kwa moja akaupongeza uongozi wa Rais Jamal Malinzi akisema unafanya kazi kubwa.
Kutokana na ripoti hiyo, Nape ambaye ni Mbunge wa Mtama mkoani Lindi, aliridhia wadau wa mpira wa miguu kusapoti timu za taifa hususani Serengeti Boys – timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ambayo kwa sasa imepiga kambi Shelisheli kujiandaa kuivaa Congo-Brazzaville Jumapili ijayo.
Serengeti Boys inawania kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri katika fainali zitakazofanyika Antananarivo, Madagascar sawa na timu ya taifa ya soka la ufukweni ambayo inatarajiwa kusafiri kwenda Abidjan, Ivory Coast kucheza mchezo wa pili wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mchezo huo.
Timu nyingine ya taifa ni ile ya wanawake ya Tanzania Bara maaarufu kwa jina la ‘Kilimanjaro Queens’ ambayo kwa sasa iko Uganda kuwania taji la Chalenji ikishirikisha timu za taifa za Afrika Mashariki katika michuano ya inayotarajiwa kufanyika jijini Jinja kwa siku tisa kuanzia Septemba 11, mwaka huu.
Nape amefurahishwa na mipango ya TFF baada ya kupeleka timu zote kushiriki michuano mbalimbali kwa vipindi mbalimbali na kwamba Serikali itasapoti lakini hapo baadaye baada ya kufuata taratibu mbalimbali baada ya Rais Malinzi kumfafanualia kuwa gharama za kuendesha mpira kwa mwaka zinafika shilingi bilioni 15, na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) huchangia asilimia tatu (3) tu ya bajeti nzima kwa mwaka.
“Kwa kuanzia msimu huu tu, FIFA imeongeza na sasa itafika asilimia 6 kwa mwaka,” alisema Malinzi jambo ambalo lilimshangaza Nape ambaye leo Septemba 10, 2016 alifanya ziara ya kutembelea TFF kujionea hali halisi na kushangazwa na taarifa za vyanzo mbalimbali zinazotuhumu shirikisho.
Nape alisema: “Serikali inasapoti maendeleo, lakini lazima yafuate taratibu, kanuni na sheria za soka.”
Katika eneo la kufuata taratibu, kanuni na sheria za soka hatua nyingine, Nape alitaka Malinzi na kamati zake kuwa wakali kwa kuwa huwa hawachui hatua mapema, inatokea wadau kutaka kuipanda kichwani TFF.
“Naagiza mchukue hatua mapema kukamua majipu kabla hajajaiva. Sasa ninyi mnasubiri kwa muda mrefu kabla ya kuchukua hatua, ndiyo maana wanawasumbua. Washughulikieni mapema, mkiwabana mapema watakaa kimya, kanuni mnazo, sheria mnazo, wabaneni,” alisema Nape.
Katika hatua nyingine, Nape alisema kwamba kuna mchakato unaendelea kwa sasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhakikisha kwamba wanarejesha mamlaka ya kumiliki baadhi ya viwanja vya soka Makao Makuu ya chama badala mikoa ambako wamegundua kuwa kuna matatizo makubwa katika menejimenti.
NA HIZI NDIZO SALAMU ZA RAIS WA TFF, JAMAL EMIL MALINZI KWA MHESHIMIWA NAPE NNAUYE WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO UWANJA WA KARUME TAREHE 10 SEPTEMBA 2016
Mheshimiwa Waziri,
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutukutanisha hapa leo.
Ni jambo la heshima na furaha kubwa sana kwetu sisi wanafamilia ya mpira wa miguu Tanzania kwa kutembelewa na wewe Mheshimiwa Waziri na ujumbe wako. Mheshimiwa ahsante sana kwa tukio hili adhimu na karibu sana kwenye makazi ya mpira “home of football”.
Mheshimiwa Waziri tunashukuru kwamba umeweza kutembelea eneo letu na kujionea wapi huwa tunafanyia shughuli zetu mbali mbali za kuendeleza michezo.
Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF limesajiliwa chini ya sheria ya baraza ya mwaka 1967 na marekebisho yake ya mwaka 1971 na madhumuni yake makuu ni kuendeleza na kusimamia mpira wa miguu Tanzania. Katika kutekeleza azma hii shughuli zetu tumezigawanya katika maeneo makuu matano:
1. Utawala
Shughuli za kila siku za uendeshaji wa mpira wetu zinasimamiwa na Sekretariet ya TFF inayoongozwa na Katibu Mkuu Ndugu Mwesigwa Selestine. Chini yake ana vitengo vikuu vitano: Ufundi ambacho kinasimamia maendeleo ya mpira, Mashindano ambacho kinasimamia mashindano mbali mbali, Fedha na utawala, Sheria na vyama wanachama na cha tano ni cha biashara na masoko. Vitengo hivi kwa pamoja vinashirikiana kuhakikisha mpira unafundishwa, unachezwa na unasimamiwa vyema. Aidha zipo Kamati mbali mbali zinazotusaidia kutushauri kwenye mambo ya kitaalam na kutoa maamuzi vikiwa vyombo huru. Pia tunacho chombo chetu kinachoitwa Bodi ya Ligi kinachosimamia uendeshaji wa ligi zetu kuu tatu Ligi kuu ya daraja la kwanza na ya daraja la pili. Ligi kuu ya vilabu vya wanawake inaendeshwa na kamati ya mpira wa wanawake.
2. Mashindano
Ili mpira uchezwe inabidi kuwepo na mashindano. Wakati wote TFF inafanya jitihada za kubuni mashindano mapya na kuhakikisha yaliyopo yanafanyika kwa mujibu wa kalenda. Kwa sasa TFF tunaendesha mashindano makuu ya kitaifa saba: Ligi kuu, Ligi daraja la kwanza, Ligi daraja la pili, Ligi ya mikoa, Kombe la Shirikisho, Ligi ya vijana na Ligi ya vilabu vya wanawake. Ukiondoa ligi daraja la pili na ligi ya mikoa mashindano yaliyobakia yote yanaonekana moja kwa moja kwenye (live) kwenye Televisheni. Shirikisho liko mbioni kuanzisha mashindano ya vilabu nane bora vya ligi kuu (Super 8). TFF pia huwa inasimamia mechi mbali mbali za kimataifa za mashindano na za kirafiki kwa timu za Taifa za rika mbali mbali za wanawake na wanaume.
3. Masoko na Biashara
Kuendesha mpira ni gharama kubwa. Wastani wa bajeti ya Shirikisho ni shilingi bilioni kumi na tano kwa mwaka.Tunawashukuru FIFA ambao hadi mwaka jana walikuwa wanachangia asilimia 3% ya bajeti hii na kuanzia mwaka huu wanachangia asilimi 6% ya bajeti hii. Jitihada kubwa zimekuwa zikifanyika kuhakikisha shughuli za uendeshaji wa mpira hazikwamishwi na ukosefu wa fedha. Kitengo cha biashara na masoko kinafanya jitihada kubwa kuhakikisha kila shindano letu linakuwa na udhamini hata kama sio wa kukidhi mahitaji yote.
4. Miundombinu
Ni muhimu sana kuwa na miundo mbinu ya kutosha na yenye sifa ya kuchezewa mpira. Kwa kushirikiana na wamiliki mbali mbali wa viwanja vya mpira TFF tumekuwa tukitoa ushauri wa namna ya kuendeleza na kutunza viwanja vyetu vya mpira ili vifae kuchezewa mpira wa kisasa. Aidha tunashukuru Halmashauri ya jiji la Tanga kwa kuiipatia TFF miliki ya eneo la ekari 18 jijini Tanga, kwa kushirikiana na FIFA eneo hilo litajengwa kituo cha kukuza na kuendeleza vipaji vya mpira cha TFF. Michoro yake iko katika hatua za mwisho za maandalizi.
5. Maendeleo ya mpira wa miguu.
TFF tumejiwekea malengo mawili makuu: Kucheza fainali za dunia mpira wa miguu wa wanawake Paris mwaka 2019 na kucheza fainali za kombe la dunia wanaume mwaka 2026.
Kwa upande wa mpira wa wanawake katika kufikia azma hii mwaka huu tunaanzisha ligi kuu ya vilabu vya mpira wa wanawake (Tanzania Women Premier League). Kutokana na ligi hii vipaji vitaibuliwa kwa ajili ya kuimarisha kikosi cha timu yetu ya Taifa Twiga stars. Kikosi hiki mwakani kitakuwa kikikusanywa mara kwa mara, kufanya mazoezi na kucheza mechi za kirafiki za kimataifa ili kujiandaa na hatua za awali za kombe la dunia mwaka 2018.
Kwa upande wa maandalizi ya Taifa stars kuelekea mwaka 2026 tayari program yetu imeanza kwa kuwa na Serengeti Boys ambayo inapambana kucheza fainali za vijana za Afrika mwakani umri chini ya miaka 17. Kwa sasa kikosi hiki kiko kambini Seychelles kujiandaa na mechi dhidi ya Kongo tarehe 18 Septemba . Timu hii pia ndiyo itapambana kucheza fainali za Afrika za vijana umri chini ya miaka 20 mwaka 2019. Aidha kwenye shule ya Alliance huko Mwanza tayari tuna kikosi cha awali cha timu ya Taifa cha vijana umri chini ya miaka 15 ambacho kinaandaliwa kucheza fainali za Afrika umri chini ya miaka 17 mwaka 2019. Tanzania tutakuwa wenyeji wa fainali hizi kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu.
Pia mwaka huu tunaanzisha ligi ya Taifa ya vijana umri chini ya miaka 20. Kutokana na ligi hii mwakani itaundwa timu ya Taifa ya awali ya vijana umri chini ya miaka 23 itakayopambana mwaka 2019 kutafuta fursa ya kucheza fainali za Olimpiki Tokyo mwaka 2020. Kutokana na makundi haya makuu matatu kuanzia mwaka 2021 walimu wetu wa mpira wataweza kuanza kutengeneza kikosi imara cha Taifa stars kuelekea Fainali za Kombe la dunia 2026. Gharama kubwa zinahitajika kugharimia program hizi na tunaomba Serikali na wadau wengine mtushike mkono ili tufikie azma yetu ya kucheza World Cup 2026.
Mheshimiwa Waziri ninaomba nigusie uendeshaji wa ligi yetu kuu na utoaji wa leseni za vilabu.Kama nilivyosema hapo awali Ligi kuu inasimamiwa na bodi ya ligi kwa maelekezo ya kanuni za mashindano kama zinavyopitishwa na kamati ya Utendaji kila mwaka. Mheshimiwa Waziri kinacholiongoza Shirikisho katika uendeshaji wa ligi kuanzia usajili, upangaji wa ratiba,upangaji wa waamuzi na utoaji wa adhabu ni kwa mujibu wa kanuni tulizojiwekea na kauli mbiu ya #fairplay,haki mchezoni.
Ninaomba nieleze pia kuwa kufuatia maagizo ya FIFA sasa tupo hatua za awali za kutoa leseni kwa vilabu zinazohalalisha vilabu kushiriki katika ligi. Mahitaji makuu ya leseni hizi ni klabu kuwa na menejimenti na kumbukumbu za mahesabu yake ya fedha ,kuwa na maeneo ya kufanyia mazoezi na kucheza mechi,kuwa na program za maendeleo ya mpira wa vijana na mwisho kueleza kinagaubaga nani anamiliki na kuendesha shughuli za kila siku za za klabu (ownership and control). Katika hili la umiliki ni marufuku klabu zaidi ya moja katika ligi moja kumilikiwa na mtu au mamlaka moja. Pia kanuni ya leseni za vilabu ina kipengele cha kipimo cha sifa cha nani anaruhusiwa kumiliki au kuendesha klabu ya mpira wa miguu , mipaka ya mamlaka yake na mahusiano na Shirikisho na mamlaka nyingine za juu zikiwemo Serikali,FIFA,CAF na CECAFA.
Mheshimiwa Waziri, ninaomba nimalizie kwa kukushukuru tena kwa kuchukua muda wako kuwa na sisi leo. Familia ya mpira wa miguu Tanzania inafarijika sana unapokuwa karibu na sisi na tunaahidi kuendelea kudumisha nidhamu katika utendaji wetu na kutoa ushirikiano wa karibu kwa Serikali yetu, vyombo na mamlaka nyingine.
Ahsante na ubarikiwe sana.
No comments:
Post a Comment