Timu ya Mpira wa Miguu ya Taifa ya wanawake wa Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Queens’, inasubiri mchezo wake wa mwisho hatua ya makundi dhidi ya Ethiopia hapo Septemba 16, 2016 ili kujihakikishia nafasi ya kucheza nusu fainali baada ya jana Septemba 12, 2016 kuilaza Rwanda mabao 3-2 katika mchezo wa kuwania Kombe la Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Kwa ushindi huo, Kilimanjaro Queens kwa sasa inasubiri kuona matokeo ya mchezo kati ya Ethiopia na Rwanda unaotarajiwa kufanyika kesho Septemba 14, kwenye Uwanja wa Nambole ulioko jijini Jinja, Uganda. Tanzania iko kundi B ikiwa pamoja na timu za Rwanda na Ethiopia wakati kundi A litakuwa na timu za Kenya, Burundi, Zanzibar pamoja na mwenyeji Uganda.
Nusu fainali itafanyika Septemba 18, kabla ya fainali kufanyika Septemba 20, 2016 ikitanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu na nne.
Mashindano ya CECAFA kwa timu za wanawake yanafanyika kwa mara ya kwanza jambo linaloleta tafsiri kuwa michuano hiyo inaweza kuinua soka la wanawake kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
No comments:
Post a Comment