Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 18 September 2015

UCHAGUZI 2015: NI KURA YA MAAMUZI KUHUSU UMASKINI WA WANANCHI


Na Ananilea Nkya Tanzania  ni  moja  ya nchi  chache barani Afrika ambazo zimejaliwa utajiri  mkubwa wa mali asili yakiwepo  madini, ardhi yenye rutuba iliyosheeni milima mabonde  na wanyama  lakini  mamilioni ya wananchi ni masikini  wa kutisha ingawa  nchi  ilipata uhuru  zaidi ya miaka  50 iliyopita.

Ili nchi iweze kuondokana na umasikini hata kama inazo rasilimali nyingi   inapaswa kuwa na rasilimali nyingine muhimu—rasilimali uongozi –uongozi unaohakikisha kuwa  mali za nchi  zinanufaisha  wananchi wote na siyo kikundi  kidogo cha viongozi.

Uongozi  wa  nchi kwa kawaida hupatikana kupitia vyama vya siasa. Hivyo  ni muhimu wanaotafuta  fursa ya uongozi  katika uchaguzi  wa mwaka huu 2015, kutambua kuwa  mamilioni ya Watanzania  hivi sasa ni maskini ili hali kikundi kidogo cha viongozi  ni matajiri  sana.

Kibaya zaidi  mamilioni ya  Watanzania wanaotaabika kwa umaskini  hivi sasa  wametambua kuwa   umaskini   wao unatokana na  uongozi  unaotoa fursa  kwa  viongozi  kuwa matajiri wa kupindukia  na  mamilioni ya wananchi  kubaki maskini.

Mamimioni hayo ya wananchi  wanateseka kwa umaskini   mwaka huu  wanataka mabadiliko ya uongozi wa nchi yao.

Wanataka mabadiliko hayo baada ya kutambua kuwa  mfumo wa utawala (Katiba)  uliotengenezwa na serikali ya CCM   ndio  unawezesha watawala wachache  kuwa  matajiri wa kutupa kwa kulipana fedha   nyingi  za  umma na kujigawia rasilimali za nchi kujitajirisha wao wenyewe.

Kwa mfano  wananchi wanajua kuwa watawala  walijiuzia kwa  bei  chee  nyumba za umma  zilizojengwa kwa mabilioni ya fedha za  kodi ya Watanzania  wanaoteseka kwa umaskini.
Kadhalika,  wananchi wanafahamu kuwa   viongozi  wa serikali  walijigawina fedha za umma zilizoibiwa kwenye akaunti ya  Tegeta escrow mwaka jana 2014.

Vilevile  wananchi  wanajua  kuwa  watawala  mfano wabunge wanalipwa   mishahara mikubwa na kiinua mgongo kikubwa katika muda wa miaka mitano tu huku watumishi wengine wa umma  mfano walimu, wauguzi na madaktari wakiwa  wanalipwa  mishahara midogo sana.

 Kwa sasa, mtu ambaye haijamuingia akilini kwamba mamilioni ya wananchi wamechoka na umaskini  ambao chanzo chake  ni uongozi  mbovu  katika nchi  yao—uongozi ambao   unatajirisha wachache na hivyo wanataka mabadiliko ya uongozi wa nchi yao,  mtu huyo  atakuwa anajidanganya.

Jambo jema ni kuwa  hata  baadhi ya wagombea Urais  kwa mfano mgombea wa  CCM,  Dr John  Magufuli na mgombea wa  CHADEMA, Edward Lowassa   kwa  niaba ya vyama vinavyounda UKAWA  wamekuwa wakizungumza wazi kwenye  mikutano yao  ya kampeni   kwamba  wananchi wanataka mabadiliko ya uongozi.

Tena wagombea  hawa wanatambua wazi kuwa  mabadiliko watayaleta  hao Watanzania   wenyewe  wanaoteseka kwa  umaskini kwa kutumia sanduku huru la kura hapo tarehe 25 Oktoba  mwaka huu 2015.
Kwa maneno mengine mamilioni ya wapiga kura maskini wanajua kuwa uchaguzi wa mwaka huu 2015 kura yao ni  kura  ya maamuzi  juu ya maisha yao. Ni kura muhimu  ya KUAMUA   KUENDELEA KUWA MASKINI AU KUUKATAA UMASKINI.

Ni kura ya kuamua iwapo  wanataka watawala wachache  wanaotengenezwa na   serikali ya CCM  waendelee kuwa matajiri wa kutisha na mamilioni ya Watanzania waendelee kuumizwa na umaskini ili hali nchi yetu ikiwa ni tajiri mkubwa wa rasilimali za asili za kuwawezesha Watanzania wote kuwa matajiri na kuishi maisha ya furaha na yenye hadhi.

Wananchi wenyewe wanajua kuwa  mabadiliko  wanayoyataka yanawezekana ingawa  kumekuwa na njama za kujaribu  kupunguza nguvu ya umma inayodai mabadiliko kutumia baadhi ya viongozi wa ngazi za juu kwenye vyama vya upinzani vinavyounda UKAWA (CUF, CHADEMA, NCCR Mageuzi na NLD)--vyama vinavyoongoza wananchi katika kutafuta mabadiliko.

Wananchi  wameshuhudia baadhi ya viongozi wa upinzani  wakiamua ghafla kuondoka kwanye uongozi  na kuungana na watawala  ambao mfumo wa uongozi umewafanya kuwa matajiri wa kutisha huku wananchi wengi wakiwa ni maskini wa kutupa.

Lakini  pamoja na viongozi   hao  kuachia ngazi, mamilioni ya wananchi hawajabadilika, hawajayumba,  msimamo wao uko pale pale na wanasonga  mbele  hadi waweze kufanya  mabadiliko wanayoyataka.

Ni kwa nini wananchi wanataka mabadiliko ya uongozi wa nchi yao?
Wanataka nao  wawe matajiri  katika  kipindi cha miaka mitano kama  ambavyo  wananchi wenyewe wameshuhudia  wanaochaguliwa  kuwa viongozi  wakitajirika ghafla  baada ya kuchaguliwa  kuwa viongozi!

Wananchi   wamechoka kuwa mafukara katika nchi yao  yenye utajiri mwingi wa asili  lakini utajiri huo  unatajirisha  makundi mawili tu-- watawala wachache  na wawekezaji wa kigeni.

Tena baadhi ya mamilioni ya Watanzania  wanaotaka mabadiliko wengi wao hawana vyama vya siasa wanavyofungamana navyo maana hata  fedha za kununua kadi ya chama cha siasa hawana.
Baadhi waliobahatika kuwa wanachama wa vyama vya siasa  kikiwepo chama kinachotawala nchi kwa sasa CCM, lakini  wengi wa  wanachama  hao ni mafukara wa kutupa pia wanaohangaika kwa umaskini kama wananchi  wengine.

Kimsingi,  mamilioni  ya watu maskini (nguvu kubwa ya umma) ambayo mfumo wa uongozi wa serikali ya CCM umezalisha, mabadiliko wanayoyataka ya uongozi hayaepukiki maana hakuna anayeweza kuizuia  nguvu ya umma inapoamua kuleta mabadiliko.

Isitoshe, mamilioni ya wananchi   hawa maskini,   ni kama bomu ambalo  serikali ya CCM  imelitengeneza kwa kujua au kwa kutokujua  kwa miaka kadhaa  sasa  na  hivi sasa  linasubiri kulipuka lenyewe kwa  amani  kwenye sanduku huru la kura  tarehe 25  Oktoba  2015.

Jambo la kuzingatia ni kwamba , atakayejaribu kuzuia  kwa mkono bomu hilo lisilipuke kwa amani kwenye sanduku huru la kura---uwanja  wa wazi ambao  ndio pekee bomu hilo linaweza  kulipuka bila kuleta madhara ya kuvuruga amani ya nchi,  mtu huyo  historia  ya taifa hili itamhukumu. Mungu ibariki Tanzania.

NOTE: Naridhia anayetaka kuichapisha au kusambaza makala hii isomwe na Watanzania  wengi afanye hivyo.

Ananilea Nkya
 E-mail:ananilea_nkya@yahoo.com

No comments:

Post a Comment