Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Wednesday 23 September 2015

TAALUMA YA HABARI IMEBAKWA!


Hivi ndivyo walivyovichora vyombo vya habari vya Marekani wakati vilipogeuka na kuanza kumpamba Barack Obama alipokuwa akiwania urais.


Na Daniel Mbega
WATANZANIA wengi wamepoteza maisha kwenye ajali za magari. Nyingi kati ya ajali hizo zimesababishwa na uzembe wa madereva.
Wakati mwingine uzembe mkubwa ni wa abiria ambao gari linapokimbia wanachekelea, wengine wanasema wanataka kuwahi, lakini gari likipata ajali wao ndio wanakuwa wa kwanza kulalamikia mwendo kasi wa dereva.
Mwaka 1998 nakumbuka nikiwa abiria wa basi moja ambalo nisingependa kulitaja, niliwahi kulisimamisha pale Chalinze baada ya kunusurika ajali mara mbili huku aliyekuwa akiendesha ni mmiliki wake, na dereva halisi akiwa pembeni.
Askari wa usalama barabarani alipolisimamisha basi hilo, ‘dereva’ alishuka haraka na kwenda kuongea naye pembeni, nami nikashuka na kuchukua kwanza namba za askari. Nikamweleza pale pale kwamba dereva huyo, ambaye ndiye mmiliki, alikuwa anataka kutuua kwa ku-overtake lori kwa mwendo kasi bila kuangalia lori jingine lililokuwa linakuja mbele yetu. Salama yetu ni kwamba ilibidi dereva alipeleke basi nje kabisa ya barabara huku abiria wote wakipiga kelele.
Nilimweleza askari kama anashindwa kumuonya dereva, basi ningepiga simu na kumripoti yeye kwa kamanda wake.
Unajua kilichotokea? Nilitukanwa sana na abiria wale wale ambao dakika chache walikuwa wanapiga kelele “Tunakufa! Tunakufa!” Wakasema namsingizia dereva.
Sikujali. Ilisaidia kwa sababu dereva halisi alikaa kwenye usukani na mwendo ukawa wa wastani na kila palipokuwepo na askari gari ‘lilipigwa mkono’. Nakumbuka mmiliki huyo, alisema; “Watu wengine mmezowea kupanda treni, mnakimbilia mabasi ya nini?” nilichotaka ni usalama, maana wanasema ‘Kawia ufike!’
Unyapaa umezidi ndani ya jamii yetu kwa sababu tu jamii iliunyamazia licha ya kuuona. Mauaji ya vikongwe na albino yameshika kasi kwa sababu jamii imeyanyamazia. Hakuna anayezungumza hadharani hata kama amewaona watu waliotenda mauaji hayo.
Naam. Tasnia ya habari tunaaminishwa kwamba ni muhimili wa nne wa Dola kwa sababu ndicho kiungo baina ya mamlaka na wananchi. Binafsi nasema tasnia ya habari ndio MUHIMILI WA KWANZA WA JAMII, kwani wanahabari ndio wanaopaswa kuisemea jamii ili mamlaka husika ziwezi kujua wapi kuna tatizo zichukue hatua.
Lakini tasnia hii ya habari kama chombo, inaoneka kwenda mrama au nasikitika kusema taaluma imebakwa! Na imebakwa kwa sababu manahodha wake ama wamezembea au wanafurahia ubakaji huo na baadhi yao ni sehemu ya kufanikisha ubakaji.
Mniwie radhi wanahabari wenzangu. Nachelea kuona tasnia ikizama nami nimo chomboni wakati ninapaswa kushauri ili chombo kiende katika mwendo unaotakiwa.
Kwa hali ilivyo sasa, vyombo vya habari, na hasa wanahabari wenyewe ambao ndio watendaji wanataaluma, vimepoteza mwelekeo wake upasao kwa misingi ya maadili na sasa vimekuwa vikitumiwa kama vipasaza sauti vya baadhi ya watu ama makundi ya watu. Jamii imesahaulika.
Tukumbushane tu kwamba ziko aina tatu za vyombo vya habari:
Kwanza; kuna mbwa mlinzi (guard dog), ambavyo kazi yake ni kulinda maslahi ya wakubwa wao. Kazi yao kubwa ni kulinda wanasiasa, taasisi za umma na kufumbia macho uchafu wowote uliomo ndani.
Pili; kuna mbwa wa mapajani (lapdog), ambavyo kazi yake kubwa ni kutumiwa na mabwana zao kushambulia mahasimu wao mmoja mmoja, siyo mfumo husika.
Mwisho; kuna mbwa mwangalizi (watch dog), ambavyo kazi yake ni uandishi wa kiharakati bila kuegemea upande wowote kwa lengo la kuwawajibisha wenye dhamana ya kuwatumikia wanajamii ama hata wanajamii wanaokiuka misingi na taratibu zilizowekwa. Hivi ndivyo vyombo vya habari makini ambavyo Watanzania walikuwa wanaamini tunavyo.
Wajibu wa wanahabari ni kuangalia habari zenye maslahi ya umma na kuzindika, nyingi kati ya hizo zikiibuliwa kutoka kwa jamii husika. Sisi ndio tunaopaswa kuanzisha agenda zinazozua mijadala chanya ndani ya jamii. Uandishi wetu unapaswa kuwa wenye kuleta mabadiliko ya umma, siyo kutumika kama kondomu.
Badala yake, tunachoshuhudia hivi sasa ni uandishi wa aina mbili za kwanza, uandishi wa kutumia kalamu kwa maslahi ya tumbo – siyo kwa kutegemea kipato cha mshahara, bali kwa kutegemea kutengeneza fitina dhidi ya mtu mmoja ili upate kitita, au wakati mwingine ‘kuua’ habari ili upate fedha kwa huyo anayetuhumiwa kwenda kinyume na maadili ya uongozi.
Ndiyo maana wakati mwingine naifikiria kauli ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi, aliposema kuna wanaandishi wachumia tumbo. Kauli hii ina mantiki katika mazingira tuliyonayo na mambo yanayotokea.

Waandishi na uchochezi
Mara kadhaa tumelalamikiwa na jamii kwamba waandishi ndio tunaochochea mambo mengi. Nakumbuka hata Baraza la Habari Tanzania (MCT) lilipata kusema kwamba waandishi ndio waliokuwa wakichochea kesi iliyokuwa inamkabili muigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’ kuhusiana na kifo cha mwigizaji mwenzake Steven Kanumba.
Hivi sasa soka la Tanzania linaonekana kwenda kombo, lakini badala ya kuandika na kuelekeza wapi wahusika walipokosea, waandishi ndio wamekuwa mstari wa mbele ‘kushangilia’ kuporomoka kwa soka hilo na matokeo yake, badala ya kurekebisha, ndiyo wanazidi kuchochea liporomoke.
Kwenye siasa, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu tunaendelea kujionea vituko vingi. Jukwaa la Waandishi wa Habari, taasisi ambayo awali ilionekana kama kiunganishi kizuri baina ya wahariri wa vyombo vyote vya habari, ndiyo ambayo sasa inalalamikiwa kwamba imeibananga taaluma kwani wajumbe ama viongozi wake wameingia katika kundi lile la ‘kutumiwa’.
Katika historia ya chaguzi za vyama vingi tangu mwaka 1995, haijapata kutokea kipindi kibaya kama cha mwaka huu wa 2015 ambapo vyombo vya habari vinaonekana kugawanyika, vikiacha kazi yao ya msingi na kueneza propaganda za wanasiasa.
Mifano mizuri ni matukio mawili yanayomhusu Edward Lowassa: Kwanza, wakati ule alipowaita Dodoma. Akawasafirisha na kugharamia chakula, malazi, gharama za mawasiliano na posho zao za kujikimu. Wakati wa kuuliza maswali, ilionekana kama walikuwa wameandaliwa watu, na maswali yaliyoulizwa hayakuweza kukidhi matakwa ya watu. Kwa mfano, wewe kama mhariri au mwandishi mwandamizi, unawezaje kuuliza swali eti "Mheshimiwa kuna watu wanaandika juu ya afya yako kutetereka, lakini sisi tunakuona fit ndio maana umetuita hapa. Je, unalisemeaje hili?" Mwingine akauliza; "Kuna watu wanakuita Eddo badala ya kukuita kwa hadhi yako Mhe. Edward Lowassa. Na wewe umekuwa ukiitika hata unapoitwa Eddo. Je, huoni hii ni kupunguza heshima yako katika jamii?"
Ni waandishi hawa hawa waandamizi ambao wanaketi mezani kuamua habari gani ichapwe na ipi isichapwe. Ndio hawa hawa ambao waandishi wa kawaida hulalamika kwamba ‘wanaua’ habari zao na kwenda ‘kuziuza’ upande wa pili kwa watuhumiwa. Kama siyo kuibaka taaluma nini basi?
Wakati Lowassa alipotangaza rasmi kujiunga na Chadema/Ukawa, tuliwaona wahariri hao hao wakipiga makofi wakati Lowassa akijieleza. Hivi kweli mnapoanza kushangilia na kusahau wajibu wenu, mnaweza kweli kuandika habari makini kama siyo kugeuka ma-guard dog na ma-lapdog?
Tujaribu basi kutanguliza uzalendo pamoja na kuchumia kwetu tumbo, maana tusipokuwa makini kalamu zetu zinaweza kuchochea machafuko halafu hao ‘tunaowatumikia’ wakakimbia nchi na kutuacha tukiteseka.

Siasa na kalamu
Tumeona wimbi kubwa la wanahabari ambao wamekimbilia kwenye siasa wazi wazi kwa kwenda kugombea nafasi za udiwani na ubunge. Wale wale ambao walikuwa vyumba vya habari miaka yote leo hii wamejipambanua uonyesha rangi zao halisi kiitikadi kwamba wako upande upi kisiasa.
Lakini nasema heri yao hao ambao wamejionyesha kuliko hawa waandishi mmoja mmoja ambao bado hawajajipambanua, lakini wameshika madawati na bado wanaendelea kutumiwa na wanasiasa kama vipaza sauti.
Wengi wanaangalia matumbo yao na taaluma, ambayo waliisomea darasani, wameamua kuiweka mgongoni.
Kwa msingi huo, tunawezaje kusimama pamoja kwa sauti moja tukadai Sheria ya Vyombo vya Habari na Sheria ya Kupata Habari ikiwa baadhi yetu ni vibaraka wa wale wale ambao tunasema wanaiminya taaluma?
Tunawezaje kupigania haki zetu za msingi Kikatiba kwa mamlaka husika au hata maslahi yetu kwa waajiri ikiwa kuna unafiki mkubwa miongoni mwetu?
Ndugu zetu kadhaa wamepata majanga, Daudi Mwangosi aliuawa kwa bomu, Richard Masatu aliuawa na watu wasiojulikana, Saed Kubenea alimwagiwa tindikali na Ndimara Tegambwage akacharangwa mapanga, Absalom Kibanda aling’olewa kucha na kutobolewa jicho, sasa tunawezaje kupiga kelele kudai usalama wetu ikiwa hali iko hivi?
Nasikitika kusema kwamba, mara nyingi katika mazingira kama hayo, waandishi hao hao ndio tunaosalitiana. Kwa sababu zile zile za kutumika ili kupata bahasha nono, mwandishi mmoja anaweza kumsaliti mwenzake akadhuriwa ama hata kuuawa.
Badala ya kuchukua hatua madhubuti, sasa baadhi yetu wamebaki kuwa vibaraka wa wakubwa, wengi wakiota ndoto za kuteuliwa serikalini kama ambavyo wameanza kujipendekeza kwa wanasiasa hivi sasa.
Taarifa za rushwa ni ngumu kuthibitika mpaka mtu akamatwe nayo. Lakini katika mukhtadha huo huo, kuna madai kwamba, kuna kundi la wanahabari ambalo limeapa ‘kufa na wagombea fulani’ hadi washinde.
Kundi hili linaelezwa kwamba limeahidiwa mambo mengi, kuanzia madaraka, majumba pamoja na vitita vya fedha visivyopungua Shs. 50 milioni.
Ni aibu kuona kwamba waandishi hawa wenye dhima kubwa kwa jamii, wanabaka haki za jamii kwa wastani wa rushwa ya shilingi moja tu kwa kila Mtanzania! Ndiyo, kama Watanzania tunakaribia milioni 50, basi kwa mwandishi kupewa Shs. 50 milioni maana yake haki ya mwananchi mmoja imeuzwa ama imenunuliwa kwa Shs. 1! What a shame!
Zinaweza kuwa propaganda, lakini kama mwelekeo wa ripoti za vyombo vya habari umegeuka, kuna uwezekano wa wananchi kuamini kwamba yanayosemwa ni ya kweli.
Wanahabari wameacha kupembua, kuchambua, kujadili na kuandika kuhusu sera za wagombea na badala yake vichwa vya habari vinavyotamba ni “CCM nyomi ya nguvu”, “Chadema washusha gharika”, “Magufuli ni mafuriko” na kadhalika huku wakipamba kwa picha nyingi zenye umati wa watu.
Hakuna waandishi wanaochambua kwa kina kuhusu nini ambacho wanasiasa wanaahidi na kama kweli utekelezaji wake unawezekana. Wamebaki kuwa sehemu ya wananchi kupiga makofi wanasiasa wanaponadi sera na kusubiri ni picha gani nzuri ambayo inaweza kupamba magazeti na kadhalika.
Wakitokea baadhi ya wanahabari wakachambua kwa kina kuhusu mambo ya msingi, tayari wanakuwa maadui – si wa wanasiasa tu, bali hata wa waandishi hawa ambao wamekwishaahidiwa madaraka na fedha. Ni aibu!
Siyo ajabu kwamba, waandishi wa aina hii wanaweza wakaibuka na kula njama za kuwadhuru wale wanaoonekana kukwamisha maslahi yao. Na niseme tu, inaweza isiwe ajabu pia kama siku moja mzoga wa mwandishi wa makala haya ukaokotwa porini umeoza au hata akakutwa amenyofolewa viungo vyake kwa sababu tu ya uzalendo kwa taifa na tasnia ya habari.
Tumekuwa mstari wa mbele wa kuwaandika watu wengine kwamba wanafiki na mafisadi, lakini kwa sababu kalamu tunazishika sisi na mara nyingi ‘dereva halipi nauli’, basi imekuwa ni vigumu hata kuthubutu kukosoa kama hivi kwa hofu kinachoelezwa kwamba ‘haifai kuandikana’!
Jamani, gari linakwenda mwendokasi, abiria mmenyamaza, mnasubiri mpaka ajali itokee ndipo mpige kelele?! Tusipokuwa makini, kizazi kijacho kitayachapa bakora makaburi yetu kwa sababu tumeshindwa kuijenga taaluma ya habari ambayo haiwezi tena kutengenezwa upya.
Ni heri uchelewe katika ulimwengu huu kuliko kuwahi katika ulimwengu ujao!

0656-331974 

No comments:

Post a Comment