Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday 8 September 2015

NANI ANAWAFADHILI CCM, UKAWA?


Na Daniel Mbega
KILIO cha muda mrefu cha Watanzania ni kudumaa kwa maendeleo na kukua kwa tabaka la maskini kunakochangiwa na mfumo usio rasmi wa ufisadi uliotamalaki kiasi cha kuua maadili ya utumishi wa umma.
Misingi imara iliyowekwa na waasisi wa taifa hili imevunjwa kwa makusudi na wale waliopewa dhamana ya uongozi, jambo ambalo limefanya pengo kati ya walionacho na wasionacho liwe kubwa zaidi.
Japokuwa ufisadi umekuwepo kwa miaka mingi nchini, lakini kashfa zimewekwa hadharani katika kipindi hiki cha awamu ya nne ya uongozi wa Jakaya Kikwete, ambaye pamoja na kushindwa kutoa maamuzi magumu katika baadhi ya mambo, lakini amethubutu kuweka uwazi na kuacha sheria ichukue mkondo wake kwa baadhi ya watu waliotuhumiwa kwa kashfa mbalimbali.
Tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 25 mwaka huu kuna maswali mengi ya kuwauliza wanasiasa, hususan wa CCM na wale wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwamba fedha wanazofanyia kampeni wamezitoa wapi.
Pamoja na ukweli kwamba ipo Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 na Sheria Namba 1 ya Uchaguzi ya mwaka 1985, lakini kwa hali inavyoonekana sheria hizi hazifuatwi kwani dhahiri gharama zinazotumiwa na vyama hivyo ni kubwa kuliko sheria inavyoelekeza.
Sheria ya Gharama za Uchaguzi inaagiza, gharama za kampeni kwa Mbunge zinapaswa kuwa Shs. 30 milioni na zisizidi Shs. 80 milioni kulingana na ukubwa wa jimbo husika, na kwa upande wa kampeni za urais, zinapaswa zisizidi Shs. 6 bilioni.
Sheria ya Gharama za Uchaguzi madhumuni yake ni kujenga mazingira yatakayowezesha kuwapo kwa uwazi zaidi katika matumizi ya fedha zitakazotengwa kwa ajili ya kampeni, pamoja na kudhibiti vitendo vya rushwa ndani ya vyama vya siasa katika uteuzi wa mgombea na uchaguzi wenyewe kwa ujumla.
Sheria hiyo inaelezea masharti kuhusu fedha zitakazotumika kwa ajili ya uchaguzi, maana ya gharama za uchaguzi, uchaguzi ndani ya Vyama vya Siasa, gharama ambazo vyama vya siasa vinapaswa kutumia wakati wa uchaguzi, masharti kwa Vyama vya Siasa na wagombea kutoa taarifa kuhusu gharama zitakazotumika wakati wa uchaguzi.
Aidha, sheria hiyo inazungumzia kuhusu michango au misaada inayotolewa na kupokewa na vyama vya siasa, kuzuia fedha kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kampeni za uchaguzi, matumizi ya gharama kwa vyama na taasisi za kiserikali wakati wa kutoa elimu ya Kampeni na chaguzi za kisiasa.
Tumeshuhudia jinsi chaguzi za ndani za kura za maoni kwa CCM na Chadema zilivyogubikwa kwa rushwa na kuna baadhi ya wagombea ambao walidakwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), wengine wakaenguliwa na vyama vyao kwa matukio hayo.
Sehemu ya tano ya sheria hii inahusu masharti yanayokataza baadhi ya matumizi ya fedha kama gharama za kampeni na uchaguzi. Matumizi hayo ni yale yanayohusu gharama kwa vitendo vinavyozuiwa au kuwa haramu wakati wa kampeni na uchaguzi.
Sheria inasema kila chama cha siasa kitagharamia kampeni za uchaguzi kwa kutumia gharama za uchaguzi zinazotokana na vyanzo vyake, kwa mujibu wa kifungu cha 8(1) cha sheria hii. Na kifungu cha 8(2) kimezingatia kuwa mgombea anaweza kutumia gharama zake mwenyewe wakati wa kampeni pale inapobidi kulingana na mahitaji ya kampeni zake.
Sheria hii inaweka sharti la uwazi katika mapato na matumizi ya vyama na wagombea kwa ajili ya uchaguzi kabla, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi na katika kifungu cha 9(1), inasema: “Mgombea atatakiwa kutoa taarifa ya fedha alizonazo na anazotarajia kupata na anakusudia kuzitumia kama gharama za uchaguzi ndani ya siku saba (7) baada ya siku ya uteuzi. Taarifa hizo zitawasiliskwa kwa Katibu Mkuu wa chama kwa mgombea wa nafasi ya Urais na kwa mgombea wa nafasi ya Ubunge na Udiwani taarifa zake ataziwasilisha kwa Katibu wa Chama wilaya.”
Kila chama cha siasa kinachoshiriki katika uchaguzi ni lazima ndani ya siku thelathini (30) baada ya siku ya uteuzi wa wagombea kufanywa na Tume ya Uchaguzi kitoe taarifa kwa Msajili juu ya fedha zote ambazo kinakusudia kutumia kama gharama za uchaguzi; na kutumia kwa kuwadhamini wagombea wa chama hicho zikiwa ni kama gharama za uchaguzi.
Pamoja na maelekezo hayo ya Sheria, lakini bado hakuna atakayekuwa na uhakika zilikotoka fedha hizo, zina masharti gani na ni kiasi gani hasa, kwa sababu naamini hakuna anayeweza kueleza kiwango halisi cha bajeti yake – si kwa wagombea wala vyama husika.
Inawezekana pia kwamba, hata kama fedha za mgombea zimepatikana katika nia haramu, lakini kwa ‘kukinusuru chama na kukisaidia kipate ushindi’ taarifa hizo zinaweza kufichwa kwa mamlaka husika na kwa jamii.
Itakumbukwa kwamba, mwaka 2012 CCM iliwahi kuituhumu Chadema kwamba ilikuwa inafanya harambee kwa wanachama wake kama geresha tu ili kuhalalisha mabilioni ya chama hicho yaliyodaiwa kutolewa na wafadhali kutoka mataifa tajiri duniani.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi,  Nape Nnauye alikaririwa akiyasema hayo Agosti 12, 2012, wakati akizungumza na waandishi wa habari, kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba jijijni Dar es salaam.
Alisema: “Itakumbukwa mara kadhaa Chadema wamekuwa wakiitisha harambee za kisanii kwa kujaribu kuwahadaa baadhi ya Watanzania kwa kuwaomba wakichangie chama hicho huku viongozi wa chama hicho wakijua kuwa tayari wameshapata mabilioni toka kwa wafadhili wao. Mfano mzuri wa usanii huu ni juzi siku ya Jumamosi, Agosti 10, 2012, kwenye hoteli ya Serena ambapo walifanyika kiini macho cha harambee na kurushwa moja kwa moja na kituo kimoja cha televisheni."
Katika harambee hiyo, zilikusanywa jumla ya Shs. 500 milioni (taslimu na ahadi) kwa ajili ya kuimarisha na kusaidia shughuli za chama.
Pengine inaweza kusemwa kwamba CCM ilikuwa imechanganyikiwa na zile kampeni za Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) ambazo zilikuwa zinaendelea nchi nzima wakati huo, lakini hata Chadema nao walikuwa wakiwanyooshea vidole viongozi wa serikali, wakiwemo mawaziri, ambao walikuwa wakipita kwenye mataifa mbalimbali ‘kukusanya fedha za uchaguzi’.
Waziri ambaye aliandamwa na kashfa za ukusanyaji wa fedha nje ya nchi ni Bernard Membe, ambaye gazeti la Rai liliwahi kuandika kwamba alikuwa anaomba msaada wa fedha na magari kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kilichoelezwa kwamba ‘ana Baraka za Rais Kikwete’, huku pia akidaiwa kutumia kete ya kuipigania Mahakama ya Kadhi ambayo imeota mbawa.
Haikuishia hapo, akatuhumiwa kwamba ametafuna Dola 20 milioni (takriban Shs. 40 bilioni) za Muamar Ghaddafi. Wengine wakasema alikuwa anazitumia katika harakati zake za kusaka urais ndani ya CCM, wengi wakasema alitaka kuanzisha Benard Membe Foundation na wengine wakasema amezikimbizia Lindi kufungua kiwanda cha saruji.
Kuhusu fedha hizo za Libya ambazo zilikuwa zimehifadhiwa katika akaunti ya Libya No.004-200-0002216-01 iliyokuwa Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), Membe alisema Serikali ya Libya na Tanzania zilitia sahihi mkataba wa nyongeza (Addendum to the Dept Swap Agreement) ambao ulizungumzia, pamoja na mambo mengine, matumizi ya fedha hizo na akasema walikubaliana zikopeshwe kwa mwekezaji aliyeteuliwa na Libya, ambaye ni kampuni ya Meis Industries Limited kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa kiwanda cha Saruji mkoani Lindi.
Lakini CCM kwa upande mwingine imekuwa ikituhumiwa kufadhiliwa na wafanyabiashara wa ndani na nje ambao biashara zao ‘hazieleweki’ na wengine ni wakwepa kodi wakubwa, huku pia kashfa mbalimbali kama za usafirishaji wa meno ya tembo pamoja na zile za uchotaji wa mamilioni ya fedha kama Escrow zikiwa miongoni mwazo.
Inafahamika kwamba, kampeni zozote za uchaguzi kote duniani zinahitaji fedha za kutosha ili kuwafikia wapiga kura. Hii maana yake ni kwamba vyama vinajipanga kuangalia ni namna gani wanatunisha mifuko yao.
Siyo vibaya kupokea fedha za wafadhili isipokuwa zisiwe na masharti ya kuliangamiza taifa letu wala taswira yake.
Ufadhili si jambo geni na hata Chama cha TANU wakati ule wa kupigania uhuru kilikuwa kikifadhili vyama vya siasa vya nchi mbalimbali barani Afrika na vingine vilianzishwa hapa hapa nchini, mfano mmoja wapo ni Frelimo cha Msumbiji.
Katika nchi hizo za Magharibi, wenzetu huwasilisha bajeti zao za kampeni zikiwa na makisio na baada ya uchaguzi ukaguzi hufanyika kuona kama fedha zilizotumika zimezidi, zimepungua ama ziki sawa sawa. Kama zimezidi, zilizoongezeka zimetoka wapi na sababu gani zilizofanya zizidi, zikiwa pungufu ni afadhali.
Ni hivi karibuni tu Rais Barack Obama wa Marekani alieleza namna anavyokusanya fedha kwa ajili ya kampeni ambapo anatumia mtandao wa intaneti.
Hapa Tanzania ukithubutu kuhoji utashambuliwa kwa maneno kwamba ‘umetumwa na nani’? Watu hawaki kuzungumza hoja, hata kama hoja ni za msingi. Na katika kipindi hiki ambapo Ukawa wamepata nguvu kubwa kutokana na ujio wa Edward Lowassa, ukihoji watasema umetumwa na CCM, lakini CCM nao watasema umetumwa na wapinzani!
Hoja yangu ni kwamba tunapaswa kuelewa bila kificho kwamba mabilioni haya ya kampeni yametokana na michango ya aina hii au msaada kutoka taasisi fulani iwe ya ndani au ya nje ya nchi.
Kama ni fedha za wafadhili pia tuelezwe ni wa aina gani na zimetolewa kwa masharti gani. Kama ni mfadhili, katoa kwa madhumuni gani, maana Waingereza wanasema: “There is no free lunch” (Hakuna mlo wa bure).
Kukaa kimya hakuna maana nyingine zaidi ya kuendelea kuzua minong’ono ambayo ingeweza kufutwa kama kila kitu kingewekwa hadharani, kinyume chake ipo siku tutashuhudia wafadhili wa siri wakidai kulipwa fadhila kwa mtindo wa kuliangamiza taifa.  Naogopa wanasiasa wasije wakaliweka taifa letu rehani kwa tamaa yao ya madaraka.
Nawasilisha.
0656-331974


CREDIT: Makala haya yalichapwa kwa mara ya kwanza na gazeti la WAJIBIKA la Septemba 7, 2015.

No comments:

Post a Comment