Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Wednesday 9 September 2015

LIPUMBA AMEHONGWA, SLAA AMENUNULIWA... UKAWA WAMETEKWA!

Profesa Ibrahim Lipumba akitetea jambo na Edward Lowassa siku kada huyo wa Chama cha Mapinduzi alipojiunga na Chadema/Ukawa Julai 28, 2015. 
Lowassa akiwa na viongozi wa Chadema siku chama hicho kilipotangaza kumpokea Julai 27, 2015. Dk. Slaa anaonekana kushoto. 

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akimkabidhi kadi ya uanachama Edward Lowassa baada ya kujiunga Julai 28, 2015.

Na Daniel Mbega
TAFSIRI ya haraka ya neno ‘Propaganda’ ni taarifa, mawazo au uvumi unaosambazwa kwa makusudi kumsaidia au kumharibia mtu, kundi la watu, harakati, taasisi, taifa na kadhalika.
Propaganda pia inatafsiriwa kama namna ya mawasiliano yanayolenga kuwashawishi baadhi ya watu waunge mkono jambo fulani.
Lakini tafsiri nyingine ya Propaganda ni taarifa ambazo siyo sahihi zinazotumika kwa msingi wa kushawishi hadhira na kuchochea agenda, mara nyingi kwa kuwasilisha taarifa zilizopangwa ama kutengenezwa (pengine kudanganya hapa na pale) ili kuhamasisha kundi linalolengwa liamini kinachoelezwa na liunge mkono.
Neno hili kwa sasa limebebeshwa mtazamo hasi kwa kulihusisha na harakati za kurubuni kwa maslahi ya kundi linaloendesha harakati hizo na kwamba wanaofanya propaganda wanaweza kuwaaminisha watu kwamba ile rangi ‘nyeusi’ ni ‘nyeupe’ na kinyume chake.
Hata hivyo, asili yake ilikuwa ni ya usawa na ilikuwa na malengo chanya, kama kuhamasisha masuala ya afya ya jamii, mabango kuhamasisha jamii ishiriki kwenye sensa na uchaguzi, ama ujumbe kuwahamasisha wanajamii kuripoti matukio ya uhalifu.
Pengine hakuna mtu katika historia aliyetumia nguvu ya propaganda kwa mafanikio ya kutisha kama alivyofanya Paul Joseph Goebbels, ambaye alikuwa Waziri wa Propaganda wa chama cha Nazi cha Ujerumani kati ya mwaka 1933 hadi 1945 wakati wa Hitler. Wakati wote wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, yeye ndiye aliyedhibiti mawasiliano yote nchini Ujerumani na kufanikiwa kulibadilisha taifa lote kuwa kakamavu na la kijeshi.
Inaelezwa kwamba, isingekuwa mbinu za Goebbels, chama cha Nazi kisingeweza kutawala Ujerumani kwani licha ya kuhamasisha magwaride ya kijeshi, ndiye aliyewafanya Wajerumani wawe makatili hata wakati wa vita kiasi cha kufanya mauaji ya kutisha, ikiwa ni pamoja na kuwateketeza Wayahudi.
Goebbels ndiye aliyehamasisha hadi kuanzishwa kwa somo la propaganda shuleni, ambapo watoto walianza kuaminishwa mambo mbalimbali tangu wakiwa wadogo, hata kama yalikuwa ya uongo.
Watoto walifundishwa na kulishwa uzalendo kwamba Ujerumani ilikuwa ni ya Wajerumani tu, hivyo Wayahudi na watu wengine hawakutakiwa kuishi humo!

Propaganda za Ukawa
Kiongozi wa chama cha National Socialism (au kwa Kijerumani: Nationalsozialismus), ambacho ni maarufu zaidi kama Nazi, Adolf Hitler, alitenga sura tatu za kitabu chake cha Mein Kampf kilichochapishwa 1925/26, ambacho chenyewe ni silaha ya propaganda, katika somo na mafundisho ya propaganda. Alidai alijifunza faida za propaganda wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kwamba propaganda za Waingereza zilikuwa na nguvu kuliko za Wajerumani. Mjadala kwamba Ujerumani ilipoteza vita hivyo kwa sababu ya nguvu za propaganda za Waingereza umeelezwa kwa kina kwenye kitabu cha Mein Kampf, na ndio ulioakisi harakati za Ujerumani kupigania utaifa wao. Ingawa madai hayo ni ya uongo – propaganda za Wajerumani zilikuwa na nguvu sana kwenye vita hivyo kuliko za Waingereza – mjadala huyo ukawa ndio ukweli wa chama cha Nazi na kupandikiza ‘imani’ kwa Wajerumani kwa msaada wa Hitler.
Hitler anasema katika kitabu cha Mein Kampf Sura ya VI (nanukuu kwa tafsiri ya Kiswahili): "Daima propaganda lazima ijidhihirishe kwa watu wengi. (...) Propaganda zote lazima ziwasilishwe katika mfumo maalumu na lazima zijikite kwanza kwa wasomi ili zisiwe juu ya vichwa vya watu wenye uelewa mdogo ambao ndio walengwa. (...) Sanaa ya propaganda hasa inahusisha uwezo wa kuamsha matamanio ya watu kwa ushawishi wa kutumia hisia zao, ili kutafuta mfumo mzuri wa kisaikolojia ambao unaweza kuteka umakini na kuchochea msukumo mioyoni mwa wananchi wengi. Makundi makubwa ya wananchi hayaundwi na wanadiplomasia au maprofesa wala hayahusishi watu wenye uwezo wa kufanya maamuzi sahihi baada ya tafakuri katika kadhia husika, bali ni makundi ya vijana ambao wanayumbishwa na wazo moja baada ya jingine. (...) Kundi kubwa la wananchi katika taifa lina tabia za kike na mtazamo ambao mawazo na mwitikio wao unatawaliwa na huruma badala ya tafakuri makini. Halitofautiani sana, lakini lina mtazamo hasi na chanya wa kupenda na kuchukia, sahihi na isiyo sahihi, ukweli na uongo." Mwisho wa kunukuu.
Hapa Tanzania, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) – Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD – vinaendesha propaganda kubwa ya kisiasa ambayo haijapata kutokea tangu mfumo wa vyama vya siasa ulipoanzishwa mwaka 1992.
Vyama hivyo vya upinzani, ambavyo Jumamosi ya Septemba 15, 2007 pale kwenye Viwanja vya Mwembeyanga, Temeke jijini Dar es Salaam – wakati huo vikiwa chini ya Umoja wa Vyama vya Upinzani – ndivyo vilivyofichua orodha ya kutisha ya watu 11 mafisadi wanaolitafuna taifa.
Orodha hiyo ilitajwa na Dk. Willibrod Slaa kwa niaba ya wenzake iliwataja Gavana wa zamani wa Benki Kuu Dk. Daudi Balali, Rostam Aziz, Nimrod Mkono, Andrew Chenge, Basil Mramba, Gray Mgonja, Patrick Rutabanzibwa, Nazir Karamagi, Edward Lowassa, Benjamin William Mkapa na Rais Jakaya Kikwete. Lowassa akalazimishwa kujiuzulu Uwaziri Mkuu.
Hapo ndipo propaganda za ‘Vita dhidi ya Ufisadi’ nchini zilipoanza na Chadema wakatumia harakati mbalimbali wakizunguka kote nchini kuelezea kwamba Chama cha Mapinduzi (CCM) kinawalinda mafisadi. Kila mahali walikokwenda waliita tafsiri ya CCM kuwa ni ‘chama cha mafisadi’.
Propaganda hizi zimesaidia kuinyoosha Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Kikwete, na tuliweza kushuhudia vigogo wengi – mawaziri na wafanyabishara wakubwa wasioguswa (the untouchables) – wakifikishwa mahakamani na baadhi yao hivi sasa wako jela wanatumikia vifungo mbalimbali.
Mbali ya kuendelea kufichua maovu ya watendaji wa serikali na kuilazimu kubadili Baraza la Mawaziri mara kadhaa, lakini wapinzani wamesaidia – kwa propaganda hizo – kuwahamasisha Watanzania kuielewa elimu ya uraia, haki zao za msingi na wapi ambako serikali haitekelezi waibu wake. Haya ni mambo muhimu sana na ndiyo majukumu ya upinzani kokote ulimwenguni. Kama wapinzani watashindwa kuyafanya haya, basi hawajui wajibu wao.
Ni kwa mtaji huo ndiyo maana Chadema iliweza kujiimarisha vyema hata uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, ambapo mbali ya mgombea wake wa urais, Dk. Slaa, kushika nafasi ya pili, lakini kwa mara ya kwanza iliweza kushinda majimbo 23 ya ubunge na kwa hivyo kikawa ndicho chama kikuu cha upinzani bungeni. Lakini pia kilishinda madiwani wengi na kuongoza baadhi ya halmashauri.

Ujio wa Lowassa Chadema
Ujio wa Lowassa kutoka CCM kwenda Chadema baada ya mwasiasa huyo kuenguliwa katika mbio za kuwania urais umeleta tetemeko katika siasa za Tanzania, maana ndiye mwanasiasa pekee aliyepata kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano kuweza kuthubutu kwenda upinzani. Huko Zanzibar ilitokea kitambo wakati aliyepata kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi (SMZ), Maalim Seif Sharif Hamad, alipojitosa mapema kwenye vyama vingi mwaka 1992.
Tetemeko la Lowassa limekuwa na mafanikio makubwa kwa Chadema na Ukawa kwa ujumla, kwani ameondoka na wanaCCM wengi waliokuwa wakimuunga mkono tangu mwanzo, hivyo kuongeza idadi ya wanachama katika upinzani lakini pia imesaidia kulainisha harakati za upinzani kuiondoa CCM madarakani.
Hata hivyo, propaganda ambazo zimetumika tangu wakati huo zimewaacha watu wengi midomo wazi. Chadema na Ukawa kwa ujumla hawataki tena kuzungumzia kuhusu ufisadi wa Lowassa na kauli mbiu yao kubwa ni kwamba ‘Heri kuwa na fisadi mmoja kuliko kundi la mafisadi’.
Yule yule ambaye walimwita fisadi, leo hii ni ‘mtakatifu’ na kipenzi cha wengi. Kauli mbiu ya ‘Vita dhidi ya Ufisadi’ ilikwisha muda wake kitambo na hakuna mpinzani yeyote kati ya wanaounda Ukawa ambaye anathubutu kuitamka.
Ukawa wanachukua jukumu la ‘kukanusha’ uhusika wa Lowassa kwenye mkataba tata wa kifisadi wa kampuni za kufua umeme za Richmond na baadaye Dowans, kwamba hakuhusika bali alitumwa. Hawazami kwa undani kuhusu nafasi ya Lowassa katika Serikali kabla hajajiuzulu. Hawazungumzia kwamba, kama Lowassa alilazimishwa, na kama kweli alikuwa mzalendo na hakupenda kulazimishwa, kwa nini hakujiuzulu kama alivyofanya Ali Hassan Mwinyi!
Hakuna anayehoji kwamba Lowassa amtaje basi mtu aliyemlazimisha, na ikibidi amtaje hata mmiliki wa Richmond na hata Dowans.
Ukawa hawazungumzii kabisa uadilifu wa Lowassa tangu akiwa Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) na hata alipoingia kwenye Baraza la Mawaziri wakati wa Awamu ya Pili ya Alhaj Mwinyi. Hawazungumzii mikataba mbalimbali ya kifisadi iliyosainiwa kwa maazimio ya Baraza la Mawaziri wakati wa Awamu ya Tatu ya Benjamin Mkapa huku Lowassa akiwa mmoja wa mawaziri hao.
Hata baada ya waziri mkuu mwingine wa zamani, Frederick Sumaye, kujiunga na Chadema, hakuna anayethubutu kuelezea maovu ya Sumaye ambaye amekuwepo kwenye Baraza la Mawaziri tangu mwaka 1985 hadi 2005.
Hakuna anayejisumbua kuhoji ni kwa nini kilimo kiliyumba na vyama vya ushirika vilikufa wakati Sumaye alipokuwa Naibu Waziri wa Kilimo na Ushirika katika ya 1985 na 1994 kabla ya kuwa waziri kamili katika wizara hiyo mwaka 1994 hadi 1995 alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu.
Hakuna anayehoji ni kwa vipi yeye akiwa mtendaji mkuu wa serikali waliuza mashirika ya umma, wakaua viwanda, wakajilimbikizia ardhi, mambo ambayo huyo huyo leo hii anasimama kwenye majukwaa kuahidi kwamba Chadema ikiingia Ikulu itarejesha viwanda hivyo. Ni propaganda.
Leo hii yeyote atakayemsema vibaya Lowassa, Sumaye ama Ukawa, ndiye anayeshambuliwa kwa maneno kwamba ama ametumwa au hataki mabadiliko, bila kuali kama mabadiliko yanayozungumza na kushabikiwa ni ‘mabadiliko bora’ au ‘bora mabadiliko’.
Hapa pia naikumbuka kauli ya Adolf Hitler katika kitabu hicho cha Mein Kampf kuhusu mbinu zinazotumika kwenye propaganda, ambapo anasema (namnukuu):  "Propaganda haihitaji kufanya uchunguzi wa ukweli wa jambo (objectively) na, kwa namna inavyotamaniwa na upande na upande mwingine, inatakiwa kuwasilishwa kwa mujibu wa nadharia ya utawala wa haki; lakini lazima iwasilishwe kwa misingi ya ukweli ambao upande husika unataka. (...) Uwezo wa wananchi wengi umedumaa, na uelewa wao ni mdogo. Kwa upande mwingine, ni wepesi sana wa kusahau. Kwa msingi huo, propaganda zote zinatakiwa kujikita katika mambo machache muhimu na hayo yanapaswa kuhubiriwa katika fomula nyepesi inayofanana. Kauli mbiu hizo zinatakiwa kurudiwa kila wakati ili kumfanya mpaka mtu wa mwisho aweze kuelewa na kushawishika na yanayosemwa. (...) Kila badiliko linalofanywa kuhusu hoja fulani ya propaganda lazima kila wakati iwe na suluhisho moja. Kauli mbiu kubwa lazima iwekwe katika njia tofauti na kwa namna mbalimbali, lakini mwisho wa siku lazima kurejea kwenye fomula ile ile."
Agosti 6, 2015 Profesa Ibrahim Lipumba alijivua uenyekiti wa CUF na kusema kwamba hawezi kuendelea kuwemo kwenye chama hicho na umoja huo baada ya kumkaribisha Lowassa kwa kuwa dhamira yake inamsuta.
Awali kabla ya ujio wa Lowassa, CUF walikuwa wamejitenga kinyemela na ndiyo maana hata kikao cha Ukawa kilichofanyika tarehe Julai 14, 2015 pale Collesium Hotel jijini Dar es Salaam, wao hawakushiriki.
Lipumba alisema ameamua kujiuzulu kwa sababu ya mambo makuu mawili; moja ni Ukawa kukubali kupokea waliotoka CCM ambao walikuwa kikwazo kwenye Bunge la Katiba, na pili ni CUF kutothamini mchango wake na hivyo kuonekana yeye ni kikwazo.
“Nimeamua kwa ridhaa yangu kuachia madaraka rasmi ndani ya CUF, nitabaki mwanachama wa kawaida, dhamira yangu inanisuta. Tumechukua watu waliotoka CCM ambao waliipinga Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Jaji Warioba… mimi ndiye mwanzilishi wa Ukawa, sasa tumewapokea wanasiasa waliotoka CCM, tumeshindwa kuenzi na kuzingatia maamuzi yetu kwenye vikao vya Ukawa,” aliongeza.
Lakini mara tu baada ya kujiuzulu kwake, propaganda nyingine za nguvu zikaanza kuenezwa, kwamba Profesa Lipumba amehongwa na kwamba alifanya hivyo ili kulinda ajira ya mmoja wa maswahiba wake wakubwa serikalini.
Mwandishi na mwanasiasa (mgombea ubunge Jimbo la Ubungo – Chadema), Saed Kubenea, aliandika kupitia MwanahalisiOnline (http://mwanahalisionline.com/siri-za-prof-lipumba-kujiuzulu-zafichuka/) kwamba, taarifa kutoka serikalini, ofisi kuu ya CCM, Lumumba, Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) na kwa watu waliokaribu na Prof. Lipumba mwenyewe zinasema, kiongozi huyo alijiuzulu baada ya wakubwa ‘kufika bei’ ili kulinda kibarua cha mmoja wa vigogo kutoka idara nyeti serikalini, ambaye ni swahiba wake wa karibu. Akaandika kwamba, haifahamiki ni kiasi gani cha fedha alicholipwa ili kumshawishi kujiondoa katika wadhifa wake, ingawa kuna taarifa kuwa zaidi ya Shs. 3.7 bilioni zimetumika kwa kazi hiyo.
Taarifa hizo (propaganda) zikasema, miongoni mwa vyeo ambavyo Prof. Lipumba ameambiwa atakabidhiwa baada ya CCM kushika Dola, ni kufanywa kuwa waziri wa fedha katika serikali ya John Magufuli au kuwa mshauri mkuu wa uchumi wa serikali hiyo, ahadi ambazo zimefanya asaliti mageuzi.
Wakati hayo yakiendelea, Septemba Mosi, 2015, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Slaa aliibuka ghafla na kueleza uamuzi wake wa kujiuzulu, huku akitoa tuhuma nyingi kwa Chadema, Ukawa, Lowassa na Sumaye, pamoja na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ambaye anadaiwa kwamba ndiye ‘mshenga’ aliyefanikisha ‘uhamisho’ wa Lowassa kutoka CCM kwenda Chadema.
Zile propaganda zilizotolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kwamba Dk. Slaa alikuwa mapumzikoni (likizo) zikakanushwa vikali na Slaa mwenyewe, ambaye alisema alijiuzulu tangu Julai 18, 2015.
Kama kawaida, propaganda zinaendelea, ambapo imeelezwa kwamba Dk. Slaa amenunuliwa ndiyo maana ameamua kuyasema hayo wakati huu.
Wengine wanasema ni shinikizo la mkewe, Josephine Mushumbuzi, ambaye alitarajia kwamba Dk. Slaa atagombea urais kupitia Ukawa na yeye atakuwa ‘Mke wa Kwanza’ (First Lady) wa Tanzania.

Ukawa wametekwa
Propaganda, kama tulivyoona hapo juu, ni mbaya kama zinatumiwa na kikundi cha watu kueneza uongo na kupindisha ukweli. Anayeendesha propaganda yuko tayari kuliita jiwe kwamba ni mkate.
Propaganda za mabadiliko ya nguvu ndizo zinazoenezwa Tanzania, na kitendo cha wapinzani sasa kumwita kila anayewanyooshea kidole kwamba wamekosea kuwa ni ‘msaliti’, ‘amenunuliwa’, ‘amehongwa’ na mambo kama hayo, kinaondoa dhana halisi ya mabadiliko hayo tarajiwa.
Ukawa, na kwa maana halisi Chadema, kuwasema wote wanaotoa hoja za kupinga mwenendo wao wa sasa wa kuifunika hoja ya ufisadi kwamba wamenunuliwa ni kuupindisha ukweli huo.
Au pengine, kama wanataka Watanzania waamini propaganda hizo za Profesa Lipumba na Dk. Slaa kuhongwa ama kununuliwa, basi Watanzania pia waamini kwamba Ukawa nao wametekwa.
Tena basi watakuwa wametekwa na mambo mawili: Kwanza; ni kwa wingi wa watu wanaomshabiki Lowassa kwamba ndio utakaofanikisha kukaa Ikulu. Inafahamika kwamba, hivi sasa Chadema haitaki jambo lolote lile isipokuwa kuingia Ikulu tu bila kujali itaingia na watu wasafi ama wachafu. Kuiondoa CCM Magogoni ni agenda yao kubwa na haihitaji mjadala wa ufisadi wala nini.
Nilipata kusema wakati fulani, Lowassa anautaka urais, lakini wapambe wake – na sasa Chadema na Ukawa – ndio wanaoutaka zaidi. Imani ya madaraka watakayoyapata baadaye ndiyo kubwa zaidi.
Pili; Chadema watakuwa wametekwa na fedha za Lowassa. Ni ukweli ulio wazi kwamba, hakuna mgombea urais wa mwaka huu anayeweza kumfikia Lowassa kwa umaarufu na pia utajiri. Kwa fedha alizojilimbikizia kwa kujinyima – iwe za mfukoni mwake ama kutoka kwa rafiki zake – Lowassa anaweza kufanya kampeni nchi nzima bila hata kutegemea ruzuku ya serikali.
Imeelezwa mara kadhaa kwenye duru za siasa na katika mitandao ya kijamii, kwamba Chadema wamelambishwa Shs. 10 bilioni na Lowassa na ndiyo maana wengine wanalalamika kwamba chama kimeuzwa!
Kwamba makubaliano ya Chadema kumuuzia Lowassa chama hicho yalifanywa Jumapili Julai 26, 2015 kati ya Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe na Lowassa, ambaye anadaiwa kukubali kutoa kiasi hicho cha fedha ili aweze kutimiza safari yake ya matumaini ya kugombea urais baada ya kuenguliwa na CCM.
Pengine fedha hizo ndizo ‘zilizofuta’ hata ile Orodha ya Mafisadi (List of Shame) kwenye mtandao wa Chadema (link: http://www.chadema.or.tz/tamko/tamko.php?id=16&pg=110) kwa kuogopa wadaku na wadakuzi wasije wakaishikia bango! Lakini wameshindwa kutambua kwamba hawawezi kufuta kumbukumbu kwenye vichwa vya watu.
Wakati Zitto Kabwe alipofukuzwa Chadema, baadaye ilielezwa kwamba mwanasiasa huyo alikuwa amepewa rushwa na Nimrod Mkono, mmoja wa watuhumiwa 11 wa ufisadi.
Tuhuma hizo zilitolewa na Mwanasheria machachari wa Chadema, Tundu Lissu mwaka 2014, ambaye alisema ulikuwepo mkakati wa kuwachafua viongozi wa chama ulioendeshwa na Zitto baada ya kuyanasa mawasiliano yake na aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Denis Msacky (sasa Mhariri Mtendaji wa Mtanzania) tangu mwaka 2009.
Lissu akasema Zitto wakati huo alikuwa na magari mawili ya Nimrod Mkono, na kwamba Mkono mwenyewe ndiye amewaambia taarifa hizo.
Lakini Zitto akauanika ufisadi wa Mbowe, akisema: “Lissu anasema nimepewa magari 2 na Mzee Mkono. Anasema kaambiwa na Mkono. Naamini Mkono alimwambia pia mwaka 2005 alimpa Freeman Aikaeli Mbowe Shs. 40 milioni ili Mbowe asifanye kampeni Musoma Vijijini.
“Nadhani (Mkono) alimwambia pia mwaka 2008 (baada ya orodha ya mafisadi kutangazwa 2007) alimpa Freeman Shs. 20 milioni za uchaguzi (mdogo) wa Tarime na Freeman akasema kwenye chama ametoa mkopo na akalipwa.”
Zitto akaendelea: “Nadhani alimwambia pia kuwa mwaka 2010 Mkono alimpa Mbowe Shs. 200 milioni za kampeni ya Slaa. Pia hakusahau kumwambia kuwa Rostam Aziz alimpa Mbowe Shs. 100 milioni za kampeni. Lissu anajua kuwa gazeti la Tanzania Daima limeanzishwa na fedha za chama kutoka Conservative Party?
“Nimefanya internship yangu kwa Mkono and Company Advocates kuhusu masuala ya mikataba. Mzee Mkono ni Mzee wangu na alisaini petition ya kumtoa Waziri Mkuu Pinda. Lissu awaambie waliomtuma wamwambie ukweli wote. Lissu ajue yeye ni kifaranga tu, mimi namtaka mama wa kifaranga ajitokeze. Aeleze aliingia deal gani na Kinana na Sumaye mwaka 2005 kufuatia deni lake NSSF. Aweke wazi mkataba kati yake na NHC kuhusu nyumba ya umma ilipo Club Bilicanas. They must know I am not a push over. Chacha died, I won't (Lazima watambue kwamba mimi siyo mjinga. Chacha alikufa, mimi siwezi). Mtu ambaye hawezi kuheshimu mke wake aliyemzalia watoto hawezi kunyooshea mtu kidole kuhusu maadili,” alisema Zitto.
Nakubaliana na maneno ya Mwalimu Ndimara Tegambwage anayesema: “Siasa haijawahi kuwa mchezo mchafu… Bali kuna watu wachafu kwenye siasa – na vyama vya siasa.”
Naam. Fedha inaweza kununua kila kitu: inaweza kununua nafasi katika Ukawa na mwenye tuhuma za ufisadi akateuliwa kugombea nafasi yoyote bila hata kufuata utaratibu.
Hizo ndizo propaganda na hiyo ndiyo michezo inayoendelea ndani yake. Sishangai kuona leo Chadema wamemuona yule yule waliyemwita fisadi, amekuwa muadilifu na ‘mtakatifu’.

0656-331974
Kumbuka: Haya ni maoni ya mwandishi, hayana uhusiano na msimamo wa blogu hii. 

No comments:

Post a Comment