
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Muimbaji wa nyimbo za injili nchini Edson Mwasabwite
anaetamba kwa sasa na kibao chake kijulikanacho kwa jina la ‘Ni kwa neema na
rehema’ amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi katika Tamasha la Krismas
litakalofanyika katika mikoa ya Mbeya, Iringa na Songea Desemba mwaka huu.
Amesema tayari amejipanga kikamilifu kukonga nyoyo za
mashabiki wake katika tamasha hilo
linalotarajiwa kufanyika tarehe 25, 26 na 28 hivyo mashabiki zake wajitokeze
kwa wingi kupata burudani ya nguvu kutoka kwake.
Ameongeza kuwa kwa mwaka huu watanzania wakae mkao wa kula
kwa kusifu na kuabudu katika Tamasha la Krismas kwani tayari amezindua albamu
yake ya pili ijulikanayo kwa jina la ‘Asilimia mia Mungu amenihurumia’ yenye
nyimbo tisa.
‘Nimejipanga vizuri kutoa burudani kwa mashabiki zangu
katika tamasha la mwaka huu la krismas kwani maandalizi ni mazuri, safari hii itakuwa
zaidi ya mwaka jana kwa sasa nina nyimbo nyingi zitakazowabariki mashabiki
zangu na tayari nimeshazindua albamu mpya’ alisema Mwasabwite.
Aidha amempongeza Mkurugenzi wa Makampuni ya Msama Promotions
kwa kuweza kuandaa tamasha kubwa la kikristo lenye mafanikio makubwa kwa kuweza
kuwakutanisha waimbaji mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania kwa
lengo la kutangaza injili nchini kwetu.
Hata hivyo ameviomba vyombo vya habari kutoa sapoti ya kazi
zao ili waimbaji wa nyimbo za injili waweze kuitangaza injili ulimwenguni kote
na kusisitiza umoja na mshikamano kwa waimbaji wa muziki wa injili.
"Makampuni ya Msama yanaaminika na kukubalika kwa watanzania
na nchi nyingine za jirani ndio maana hata tamasha linafanikiwa, tunaomba
wananchi waendelee kununua kazi zetu, media mtusapoti ili tufike mbali, na kwa waimbaji
wenzangu tuwe na umoja ili tufanikiwe katika kazi zetu’ alisema.
Kwa upande wa Msama Video Production wamesema kwa mwaka huu
wamejipanga vizuri katika Tamasha la Krismas kwani wanavifaa vipya na vya
kisasa vyenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi katika mazingira yoyote yale na
wafanyakazi wakutosha wenye ueledi katika fani hiyo.
Uongozi wa Msama Video Production unawaalika umma wa
watanzania kushiriki katika Tamasha la Krismas la mwaka huu litakalofanyika
nyanda za juu kusini.
No comments:
Post a Comment