Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 12 December 2014

ESCROW YATIKISA MPAKA MAREKANI, TANZANIA KUNYIMWA DOLA MILIONI 700

Rais Barack Obama wa Marekani

Wakati Rais Jakaya Kikwete akisubiriwa kutoa maamuzi ya mapendekezo yaliyofikiwa na Bunge kuhusiana na sakata la uchotwaji fedha zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka kaunti ya Tegeta Escrow wiki ijayo, Marekani imebainisha kuwa  mkataba wa pili wa miradi inayofadhiliwa na shirika lake la Changamoto za Milenia (MCC) utategemea hatua zitakazochukuliwa na serikali ya Tanzania dhidi ya wahusika wa kashfa hiyo.

Uamuzi huo wa Marekani ambayo inafadhili miradi mingi ya mabilioni ya fedha ni mtihani wa pili kwa Rais Kikwete baada ya ule wa maazimio ya Bunge yaliyotaka viongozi wakiwamo mawaziri waliotajwa katika kashfa hiyo kuwajibishwa.

Wanaotakiwa  kuwajibishwa na Rais Kikwete ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa, Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.

Taarifa iliyotolewa jana na Ubalozi wa Marekani nchini ilieleza kuwa wakurugenzi wa MCC waliokutana katika mkutano wao uliofanyika Desemba 10, mwaka huu wamesikitishwa na hali ya rushwa nchini Tanzania.

“Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (MCC) ilikutana katika mkutano wa kila mwaka wa kuchagua nchi zitazopatiwa fedha na MCC, katika mkutano huo Bodi ilielezea hofu na masikitiko yake kuhusu hali ya rushwa nchini Tanzania, ikiwa ni pamoja na yale yaliyojitokeza hivi karibuni katika suala linalohusu kampuni ya kuzalisha umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL),” ilieleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taaarifa hiyo, ingawa bodi hiyo ilipiga kura ya kuiruhusu Tanzania iendelee na maandalizi kwa ajili ya mkataba wa pili wa miradi ya MCC, imehimiza Serikali ya Tanzania kuchukua hatua thabiti na mahsusi za kukabiliana na rushwa ili bodi hiyo iweze kuidhinisha mkataba huo.

Katika tamko hilo kwa umma ambalo limewekwa kwenye tovuti ya MCC, bodi ilieleza kutambua umuhimu wa kusubiri na kuona utekelezaji kamilifu wa tamko lililotolewa na Ikulu ya Tanzania Desemba 9, mwaka huu kwamba itachukua hatua za haraka na kutoa maamuzi dhahiri na thabiti kuhusu maazimio ya Bunge juu la suala la IPTL.
Naye Balozi wa Marekani nchini, Mark Childress, alisema kuwa mapambano dhidi ya rushwa ni muhimu sana kwa mkataba mpya kati ya MCC na Tanzania katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini Tanzania.

“Tumetiwa moyo na tamko lililotolewa na Ikulu hapo tarehe 9, Desemba kwamba hivi karibuni itashughulikia maazimio ya bunge kuhusu IPTL.  Tunatoa wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka kuhusu suala hili hasa kutokana na uzito wake katika masuala muhimu kadhaa ya maendeleo,” ilieleza taarifa hiyo.

Aidha, Bodi iligusia makubaliano kadhaa yaliyofanyika na serikali ya Tanzania iliahidi kufanya mageuzi ya kisera, kimuundo na kitaasisi ili kuongeza ufanisi na uwazi katika taasisi zake pia na katika sekta ya nishati. 

“Tunafurahi kwamba mchakato wa majadiliano ya maandalizi ya mkataba wa pili utaendelea kwa miezi kadhaa ijayo. Tunapenda kusisitiza kuwa ni lazima ahadi hizi zitekelezwe kabla Marekani haijafanya maamuzi ya mwisho kuhusu mkataba wowote mpya na Tanzania,” alisema.

Tanzania ilikuwa mojawapo kati ya nchi kumi zilizojadiliwa na Bodi ya MCC iliyokutana kuangalia kama nchi hizo zimekidhi vigezo vya kuendelea na mchakato wa kuandaa mikataba mipya.

Kama mkataba huu utapistishwa utakuwa ni mkataba wa pili wa MCC kwa Tanzania. Kati ya mwaka 2008 na 2013 MCC ilitekeleza mkataba wa uwekezaji wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 698 uliowezesha utekelezaji wa miradi ya maji, barabara na nishati ya umeme nchini kote.

Chini ya mkataba huo, mtandao wa nyaya za umeme wenye zaidi ya  kilomita 3,000 ulijengwa, jumla ya kilomita 450 za barabara pia zilijengwa, hali kadhalika, mitambo mikubwa miwili ya usafishaji maji na njia ya kurukia ndege katika kiwanja kimoja cha ndege ilijengwa.

Shirika la Changamoto za Milenia ni taasisi ya Serikali ya Marekani inayotoa misaada kwa nchi zinazoendelea. Shughuli za MCC zinajengwa katika msingi kwamba msaada utaleta ufanisi na matokeo makubwa zaidi pale tu unapoimarisha utawala bora, uhuru wa kiuchumi na uwekezaji katika watu ambao unakuza uchumi na kuondoa umasikini.

Novemba mwaka huu, Serikali ya Marekani kwa kupitia MCC, ilikubali kutoa ruzuku ya hadi Dola za Kimarekani milioni 9.78 kwa ajili ya maandalizi ya miradi ya uwekezaji yenye matokeo makubwa katika sekta ya nishati nchini. 

Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo ilifanyika jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Balozi Childress.

Makubaliano yalitiwa saini na Makamu wa Rais wa MCC anayeshughulikia Mikataba na Uendeshaji wake, Kamran Khan, na Waziri wa Fedha wa Tanzania, Saada Mkuya Salum.

Wakati wa mkutano wa 16 na 17 wa Bunge, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), alidokeza kusudio la Marekani kukataa kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya MCC, lakini Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alikanusha taarifa hizo.

Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alikazia akisema makubaliano hayo yalikuwa hayajasainiwa Septemba, bali kikao cha kuyapitisha kingefanyika Desemba na kushangiliwa na wabunge wa CCM.

MBATIA AKOLEZA MOTOKatika hatua nyingine, Mwenyekiti mwenza wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia, amekoleza moto wa sakata Tegeta Escrow, baada ya kuwataka wananchi wa jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, kila mmoja kudai mgao wa Sh. 609, 900 kwa viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

 Akizungumza jana na wakazi wa vijiji vya Mrimbo-Uuwo, Matala, Kondiki, Mwika Lole, Maring’a, Msae-Kinyambuo na Kondeni vilivyopo Kata ya Mwika Kusini  na Kata ya Mwika Kaskazini, Wilaya ya Moshi, Mbatia aliwaambia wananchi hao kwamba hawapaswi kuendelea kuumia kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa maabara na shule za kata kwa sababu wanao uwezo wa kutumia fedha zilizochotwa katika akaunti hiyo kuchangia maendeleo.

 “Si mliona baadhi ya wabunge wa CCM wakiwatetea watuhumiwa wa wizi wa fedha za Escrow, ni hivi; wakija Vunjo kuwaomba muwapigie kura wagombea wao katika uchaguzi wa serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji kesho kutwa, kila mtu adai kwanza hela yake shilingi 609, 000 ndo muwapigie kura…wako vigogo wanaotafuta njia za kujinasua na kashfa hii wakitafuta vijisababu eti zilikuwa za shule na wengine wametafuta watetezi wakati waliwatusi Watanzania wenzao,” alisema Mbatia.

"Katibu Mkuu Kiongozi (Balozi Sefue) anasema Rais atafanya uamuzi kuhusu maazimio ya Bunge baada ya kufanya uchunguzi na kujiridhisha na muda mfupi baadae Ikulu hiyo hiyo, inasema Rais Kikwete atafanya uamuzi wiki ijayo, sasa tuamini kauli ipi hapa…Bunge la Januari mwaka ujao, litakuwa chungu kwa serikali kama kashfa hii itafukiwa fukiwa na kuwaacha baadhi ya watuhimiwa wakiwakejeli watanzania,” alisema Mbatia.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment