Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 12 December 2014

BUNGE LAIVUTIA PUMZI KAMPUNI YA VIP YA RUGE

Naibu Spika, Job Ndugai

Bunge limeijibu Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited likisema kauli yake ya kuyashutumu maazimio ya Bunge dhidi ya kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuyaita kuwa ni ya kipuuzi, ni dharau kwa serikali.
Limesema litatafakari kwanza kama kweli kauli hiyo imetolewa na kampuni hiyo kabla ya kufikiria hatua za kuchukua.

NDUGAINaye Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema haamini kama mtu, ambaye ni Mtanzania halisi anaweza kusema maamuzi ya Bunge lake ni ya kipuuzi.Ndugai alisema kama kweli kauli hiyo imetolewa na kampuni hiyo, uchunguzi utafanyika kabla ya kuangalia hatua za kuchukua."Tujipe muda kwanza wa kutafakari suala hili. Kama kweli limesemwa, tutaangalia namna ya kuweza kuchukua hatua," alisema Ndugai.

FILIKUNJOMBEMakamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Deo Filikunjombe, alisema kauli ya kampuni hiyo inaweza kutolewa tu na mtu, ambaye pengine ameiweka serikali mfukoni.

“Hayo maneno yanaweza kusemwa na mtu, ambaye ameishika dola mkononi. Lakini Rais ni sehemu ya Bunge. Kwa maana hiyo, kampuni ya VIP inapotoa kauli kama hiyo, inamaanisha hata Rais hana maana,” alisema Filikunjombe.

Filikunjombe, ambaye pia ni Mbunge wa Ludewa (CCM), alisema wakati PAC inawasilisha ripoti yake kwenye mkutano wa Bunge la 126 na 17 ilieleza kuwa suala hili inawezekana serikali ilikuwa na gazi kuliamua au iliganzishwa.

DK. KASHILILLAHKatibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, alipoulizwa kuhusu kauli ya VIP alisema hawezi kujibu lolote.Juzi Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, ilitoa taarifa na kueleza kuwa maamuzi ya Bunge yaliyopendekezwa na PAC ni ya kipuuzi.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana yenye kurasa 19 na orodha ya vielelezo 17, Katibu wa Kampuni hiyo, Respicius Didace, alisema VIP inatuhumiwa kimakosa kwamba, imefanya vitendo vya uvunjifu wa sheria kuhusiana na akaunti ya Tegeta Escrow.

“Tuhuma hizi ni upuuzi kwa sababu VIP ililipwa kwa msingi wa Mkataba wa Uuzaji wa Hisa uliotangazwa na kuridhiwa kwa amri ya Mahakama ya Septemba 5, 2013; na kufuatiwa na amri ya mahakama ya Januari 17, 2014 iliyotolewa katika shauri la wazi; na baada ya kuwa imefanya malipo ya Sh. bilioni 38 (sawa na dola za Marekani milioni 23.6) katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kugharimia malipo yote ya kodi ya VIP,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo, ambayo pia imeishambulia Benki ya Standard Chartered (SCB) kama chimbuko la vurugu zote kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow.

Didace alisema VIP siyo mshirika katika mkataba wa akaunti ya Tegeta Escrow na haikuwa na jukumu lolote katika uanzishwaji wake na ulipwaji wa fedha kutoka katika akaunti hiyo na siyo mwanahisa tena wa IPTL.

Alisema hoja zilizotolewa na PAC wakati wa mjadala bungeni kwamba, fedha zilizopo katika akaunti ya Escrow ni za serikali siyo sahihi, kwani haikusema wazi ni sehemu gani ya fedha hizo ni mali ya umma na kwa misingi gani.

“ Huo siyo msingi wenye mashiko wa kuwatuhumu watu kwamba, wameiba fedha za umma, VIP ina uelewa mpana na wa kina wa historia ya IPTL na msingi wake wa kisheria na imegundua kwamba, taarifa nyingi na tuhuma kuhusu VIP, IPTL na akaunti ya Escrow   zinafanana kwa kutokuwa sahihi,” alisema. Alisema VIP inaamini kwamba, umma na Bunge la Tanzania wamedanganywa kwa kuaminishwa tuhuma zisizokuwa za kweli, ambazo zitafaidisha malengo ya kigeni na kuwafakarisha Watanzania.

Aliongeza kuwa Bunge na PAC zimedharau masuala ya msingi na kushupalia masuala yasiyokuwa na tija kwa taifa na kwamba, mapambano haya yamekuwa na mafanikio na hii ndiyo sababu SCB imesababisha mkanganyiko kwa kuwalisha Watanzania taarifa za uongo. Didace alisema PAC imetoa tuhuma nzito za uvunjifu wa taratibu au jinai dhidi ya watu kadhaa bila ya kutoa ushahidi au sababu: “Hiki ni kiwango cha juu cha kutokuwajibika na ambalo limefanyika kwa maslahi ya muda mfupi ya kisiasa.”

“Ni kiwango cha juu cha kukosa uwajibikaji kwa sababu PAC haiwezi kutoa haki ambazo mahakama ya kisheria lazima itoe kwa watu binafsi wakati wakitoa maamuzi kuhusu migogoro yao,” ilieleza taaifa hiyo.

Alisema hakuna mahitimisho yoyote ya kisiasa yanayoweza kupewa fursa ya kuathiri mwenendo wa utoaji wa haki na mwenendo mzima wa kisheria wa pande zote za ndani ya Tanzania na nchi za ikiwa ni pamoja na kwa VIP.

“Mihimili ya mahakama na watendaji wa serikali wasikimbilie katika kuhukumu na badala yake waheshimu uhuru, mamlaka ya kisheria na madaraka ya muhimili wa mahakama, ambao ndio nguzo za utawala wa sheria katika nchi yoyote ile ya kidemokrasia kama Tanzania,” ilisema taarifa hiyo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment