
Na Hastin Liumba, BrotherDanny Blog
Sikonge: DIWANI wa Kata ya Kiloli Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, Winston Hamsini, amesema kukosekana kwa miundombinu ya uhakika katika kata yake kumechelewesha upatikanaji wa maendeleo kwa muda unaotakiwa.
Kauli hiyo aliitoa kwenye mkutano wa hadhara wakati akiongea na wananchi wa kata yake akihamasisha wapigakura kukamilisha michango ya ujenzi wa Maabara unaoendelea.
Hamsini alisema licha ya ujenzi wa maabara kuelekea hatua za mwisho, kukamilika kwake kumetokana na hali ya miundombinu ya uhakika katika Kata ya Kiloli.
"Kata hii inakabiliwa na ukosefu wa mawasiliano ya simu kwani hakuna mnara hata mmoja wa kampuni za simu, hivyo wananchi wanalazimika kupanda juu ya milima, miti au vichuguu ili kupata mawasiliano ya simu za kiganjani," alisema.
Alisema miundombinu ya barabara nayo ni kero kubwa kwani vifaa kufika eneo la kata ni kazi pevu kwani kutoka makao makuu ya Wilaya ya Sikonge hadi Kata ya Kiloli ni kilometa 182, hali ambayo inawawia vigumu hata kwenye ujenzi wa maabara.
Anasema usafirishaji bado hali siyo nzuri kwani saruji hadi kufika eneo la ujenzi ni kazi kuwa kutokana na miundombinu ya barabara.
Anasema licha ya changamoto hizo bado wananchi walio wengi wanachelewa uchangiaji wa fedha hasa kutokana na kuchelewa kulipwa fedha za mauzo ya tumbaku.
Alisema fedha ambazo zimepatikana katika uchangiaji kutoka kwa wananchi ni Sh milioni 17 ikiwemo yeye mwenyewe kutoa Sh 400,000.
Hata hivyo, alionya watendaji baadhi kuacha tabia ya kutoza wananchi hasa jamii ya wafugaji kwani wamekuwa wakitoza kaya zenye ng`ombe mara mbili na kutaka tabia ikome huku akiomba wananchi wanaochangia kudai risiti pindi wachangiapo.
No comments:
Post a Comment