Na Hastin Liumba, BrotherDanny5 Blog
Nzega: CHAMA cha Mapinduzi CCM wilaya ya Nzega Mkoani Tabora kimesema mradi mkubwa wa maji safi na salama kutoka ziwa Victoria unatarajia kuanza kutekelezwa mapema Januari 2015.
Mradi huo utaanza kutekelezwa ukitokea mkoani Shinyanga kupitia Nzega na Igunga mpaka Tabora.
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni za chama hicho wilaya Amos Majile Kanuda ambaye ni mwenyekiti wa CCM wilaya alisema kuwa wananchi wanapaswa kuamini ahadi hiyo iliyotolewa na serikali kulingana na usimamizi wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010.
Alisema kuwa chama hicho kimewahakikishia wananchi wa mkoa wa Tabora kupata maji safi na salama kupitia mradi mkubwa wa maji safi kutoka Ziwa Victoria.
Alisema kuwa mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa inayokabiliwa na uhaba mkubwa wa maji safi na salama na kuongeza kuwa mpango huo utaweza kutatua kero za wananchi na kuepusha adha mbalimbali walizokuwa wakizipata.
Alisema kuwa ahadi hiyo ya mradi wa maji kutoka ziwa Victoria ni ahadi ya serikali ya awamu ya nne kwa mkoa wa Tabora kupata maji safi na salama kupitia ziwa Victoria.
Kwa upande wake Katibu wa chama hicho wilaya Kajoro Vyohoroka aliwataka wananchi kuaacha kubeza maendeleo yaliyopo badala yakewaangalie kile ambacho kimefanywa na serikali tokea uhuru katika kuwaletea maendeleo kwa wananchi.
Alisema kuwa wananchi wapaswa kuendelea kuiamini serikali yao kikamilifu na sikubadili vyama vya siasa ambavyo haviwezi kuongoza nchi kutokana na kutoaminika kwa wananchi.
Aliwataka wananchi kujitokeza kuchagua wenyeviti wa mitaa pindi ifikapo Dicemba 14 mwaka huu siku ya kuchagua viongozi wa kuongoza mitaa,vitongoji na vijiji.
No comments:
Post a Comment