
Na Hastin Liumba, BrotherDanny5 Blog
Tabora: KANDA ya Magharibi ambayo ni mikoa ya Kigoma na Tabora inaongoza kwa vifo vingi vya kinamama na watoto wachanga kutokana na wengi wao kujifungua wakiwa na umri chini ya miaka 18 pamoja na kutozingatia uzazi wa mpango, imefahamika.
Hayo yalisemwa na James Mlali kutoka shirika lisilo la kiserikali la Utetezi wa huduma za uzazi wa mpango wakati akitoa mafunzo kwa wanahabari Mkoani Tabora siku moja kabla ya uzinduzi wa kampeni ya kuzindua upya nyota ya kijani utakaofanyika Desemba 10 mwaka huu.
Mlali alisema asilimia 17 ya vifo vyote vya wanawake vinatokana na wakati wa ujauzito,kujifungua,au katika kipindi cha miezi miwili baada ya kujifungua au kutoa mimba.
“Jukumu la kupata watoto nchini Tanzania linaanza mapema kuanzia miaka 15, na hii ni hatari kwa maana katika umri huu viungo vya uzazi vinakuwa havijakomaa na wastani wa Taifa ni watoto watano ila kwa kanda hii wana watoto kuanzia saba na kuendelea na ambao huzaliwa katika kipindi kifupi kifupi.” alisema.
Alisema kiwango cha uzazi nchini kimepungua ila bado ipo juu kwani mwaka 1991-1992 kilikuwa watoto 6.3 kwa kila mwanamke na katika mwaka 2010 kilishuka hadi kufikia watoto 5.4, na kwa vijijini 6.1.
Alisema katika maeneo ya vijijini kuna kiwango kikubwa cha kuzaliana na elimu haijawafikia walengwa hivyo serikali ina mikakati ya kupeleka elimu pamoja na huduma katika maeneo hayo ili kuzipata kwa karibu na kupandisha wastani wa Taifa wa asilimia 60 ifikapo mwaka 2015.
Nae Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Tabora Dkt Martin Fikiri alisema lengo la kampeni ya uzinduzi wa nyota ya kijani ni kuchangia katika lengo la Taifa la kufikia wastani wa asilimia 60 ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango ifikapo 2015.
Fikiri alisema Mkoa umejipanga kuongeza mahitaji ya huduma za uzazi wa mpango pamoja na upatikanaji wa huduma hiyo katika maeneo yote hasa yale ya vijini ili wenzi kuzipata kwa urahisi na kupanga uzazi ili kupata watoto kwa wakati wanaoutaka na pia kumudu mahitaji yao ya muhimu hasa elimu.
Alisema kwa kutumia uzazi wa mpango unasaidia kuokoa maisha ya mama na watoto wachanga pia kupunguza mimba zisizotarajiwa,kukuza uchumi na maendeleo ya familia pamoja na kumfanya mama kuwa na afya njema.
“Wanawake wengi wanapenda kuachanisha watoto na wengine kuacha kuzaa baada ya idadi kadhaa ya watoto lakini wamekuwa wakipingana kauli na wenza wao mama hataki baba anataka jukumu la kupanga uzazi ni la wote baba na mama,mama kuzaa watoto wengi bila kupumzika ni hatari kwa afya yake,anapaswa kupewa uhuru ”aliongeza Dkt huyo.
*Imeandaliwa na www.brotherdanny5.blogspot.com
No comments:
Post a Comment