Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 14 February 2016

KWA MCHEZO WA LEO, SAFARI YA YANGA LIGI YA MABINGWA AFRIKA INAWEZA KUISHIA KIGALI


Na Daniel Mbega
BAO pekee la dakika ya 17 ya mchezo wa leo mjini Curepipe, Mauritius lililofungwa na Mzimbabwe Donald Ngoma dhidi ya limeisafishia tu Yanga njia dhidi ya Cercle de Joachim kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini bado halijawapa uhakika wa kufanya vizuri kwenye mashindano ya mwaka huu.
Matokeo ya mchezo huo wa kwanza, ambao dhahiri ulikuwa wa ushindani mkubwa kutokana na soka la kasi linalochezwa na mabingwa hao wa Mauritius, hayatoi nuru ya kutosha kwa vijana wa Jangwani ambao wamekuwa na rekodi ya kuzionea timu kutoka Visiwa vya Bahari ya Hindi hususan Mauritius, Comoro na Shelisheli.
Faraja pekee inayoweza kuelezwa na wadau wa soka ni kwamba, timu hiyo ilikuwa inacheza ugenini, hivyo inayo nafasi ya kutosha kujirekebisha na kufanya vizuri kwenye mchezo wa marudiano utakaofanyika Februari 27, 2016 jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, kwa mwenendo ilionao timu hiyo, hata kama itavuka hatua hiyo ya awali, inaweza kurudia raundi ya pili, tena Kigali, mbele ya APR.
APR yenyewe inaanza kampeni zake kesho Jumapili wakati itakapokuwa ugenini mjini Mbambane, Swaziland kucheza na wenyeji Mbambane Swallows, huku wadau wengi wakiipa nafasi kubwa timu hiyo ya Jeshi la Rwanda kufanya vizuri.
Mabingwa wa soka wa Zanzibar, Mafunzo, wamejikuta wakigeuzwa asusa nyumbani kwenye Uwanja wa Amaan baada ya kufungwa mabao 3-0 na Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Timu nyingine ya Afrika Mashariki, Bunamwaya SC maarufu kama Vipers ya Uganda, jana Ijumaa ilifanikiwa kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 nyumbani jijini Kampala dhidi ya mabingwa mara mbili wa Afrika, Enyimba ya Nigeria, hivyo kuufanya mchezo wa marudiano mjini Aba wiki mbili zijazo kuwa mgumu zaidi kwao.
Mabingwa wa Kombe la Washindi wa mwaka 1987, Gor Mahia ya Kenya, wameanza vibaya mashindano hayo baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 nyumbani dhidi ya klabu ya CNaPS Sport ya Madagascar.
Matokeo mengine ya mechi za leo yanaonyesha kwamba, CRD Libolo ya Angola imeichabanga Micomeseng ya Guinea ya Ikweta mabao 5-1, Mangasport ya Gabon imetoshana nguvu na Etoile du Congo ya Congo Brazzaville kwa kutoka suluhu, matokeo ambayo pia yalishuhudiwa kwa mechi baina ya AS Douanes ya Senegal dhidi ya Horoya ya Guinea.
Stade Malien ya Mali imeichapa Bobo-Dioulasso ya Burkina Faso mabao 3-1, mechi ambayo imemalizika usiku huu wakati Chicken Inn ya Zimbabwe imeilaza mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini bao 1-0 mjini Bulawayo.
Katika mechi nyingine ya jana Ijumaa, Olympique Club De Khouribga ya Morocco iliifunga Gamtel FC ya Gambia mabao 2-1 mjini Marrakech.
Katika Kombe la Shirikisho, leo hii Atletico Olympic ya Burundi imechapwa bao 1-0 na Fomboni ya Comoro wakati Bidvest Wits ya Afrika Kusini imeshinda ugenini kwa Lightstars ya Shelisheli kwa mabao 3-0. Bidvest ndiyo inayoweza kupambana na Azam FC ya Tanzania katika raundi ya kwanza.
Defence F.C. ya Ethiopia imekubali kutandikwa nyumbani na Misr Elmagasah ya Misri kwa mabao 3-1 huku Harare City ya Zimbabwe ikishinda nyumbani kwa mabao 3-2 dhidi ya Adema ya Madagascar.
Hali ilikuwa ya neema zaidi kwa timu mbili za Afrika Mashariki. Polisi ya Rwanda imeshinda nyumbani kwa mabao 3-1 dhidi ya Atlabara ya Sudan Kusini wakati Sports Club Villa imeshinda ugenini kwa Al-Khartoum ya Sudan kwa bao 1-0.
Nayo Sporting Gagnoa ya Ivory Coast imeshinda nyumbani kwa mabao 2-0 dhidi ya USFAS Bamako ya Mali katika mchezo mkali na wa kusisimua.
Jana kulikuwa na michezo miwili ya Kombe la Shirikisho, ambapo Bakaridjan ya Mali ilitoka sare ya 1-1 na Stade Gabesien ya Tunisia huku Al-Itihad ya Libya ikiichabanga SONIDEP ya Niger mabao 4-1, mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taieb Mhiri jijini Sfax, Tunisia kutokana na matatizo ya vita nchini Libya.

CREDIT: FIKRAPEVU

No comments:

Post a Comment