Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 14 February 2016

KIIZA AIPELEKA SIMBA KILELENI KWA MUDA, YASUBIRI MAJALIWA YA COASTAL NA AZAM


USHINDI wa mabao 2-1 yaliyopachikwa kimiani na Mganda Hamisi Kiiza katika mechi dhidi ya Stand United mjini Shinyanga yameipa Simba uongozi wa Ligi Kuu kwa muda huku wakisubiri matokeo ya mechi ya kesho baina ya 'Wana lambalamba' Azam FC na wenyeji wao Coastal Union 'Wagosi wa Kaya' itakayochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Simba, ambayo ilikuwa inasuasua chini ya kocha Mwingereza Dyran Kery, sasa imezinduka na kupata ushindi wa tatu mfululizo tangu mikoba hiyo ilipoanza kushikiliwa na mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Uganda Mayanja Jackson, na ushindi wa leo umeifanya ifikishe jumla ya pointi 45 katika mechi 19, mbili dhidi ya vinara wa Ligi Kuu Yanga.
Hata hivyo, uongozi wake wa ligi unaweza kuwa wa muda ikiwa Azam watashinda mchezo wao na Coastal, kwani nao watafikisha pointi 45 huku wakiwa na mtaji wa mabao mengi ya kufunga, jambo ambalo Simba inaliombea lisitokee ili iendelee kujisimika kileleni kabla ya mechi yake na watani zao wa jadi, Yanga, itakayopigwa Februari 20, 2016.
Katika mchezo wa leo uliopigwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Kiiza alifunga mabao yake dakika za 34 na 47 na sasa ndiye anayeongoza orodha ya wafungaji baada ya kumpiku Mrundi Amissi Tambwe wa Yanga. Kiiza ana mabao 16 dhidi ya 14 ya Tambwe.
Bao la kufutia machozi la Stand United lilipatikana dakika ya 90 mfungaji akiwa David Ossuman. 
Matokeo ya mechi nyingine za leo ni kwamba, African Sports wamewachapa maafande wa Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Mkwakwani, huku kocha Mmalawi, Kinnah Phiri akianza kwa kismati ndani ya Mbeya City baada ya kuiongoza timu hiyo kuikandamiza Toto African ya Mwanza mabao 5-1 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya. 
Mabao ya Mbeya City yamefungwa na Raphael Alfa kwa penalti dakika ya tano, baada kiungo mshambuliaji Ditrim Nchimbi kuchezewa vibaya kwenye boksi, Ramadhani Chombo 'Redondo' dakika ya 35, Haruna Moshi 'Boban' akapachika mawili dakika ya 41 na 43 na Meshack Samuel dakika ya 79, huku bao pekee la Toto likifungwa na Japhet Mkala dakika ya 78.
Ndanda FC imeifunga 1-0 Majimaji Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, wakati JKT Ruvu imelazimishwa sare ya 1-1 na Kagera Sugar Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment