
IGP Ernest Mangu
Na Mwandishi Wetu, TaboraASKARI polisi watatu wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) mkoani Tabora wamefikishwa mahakamani akiwemo mkuu wa kikosi hicho Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Bhoke Julius Bruno kwa tuhuma za upotevu wa bunduki Nane aina ya SMG, mali ya jeshi la hilo.
Wengine waliopandishwa kizimbani mbele ya Hakimu mkazi Mfawidhi wa mahakama ya mkoa wa Tabora, Issa Magori ni Koplo Idd Abdllah na Mwinyi Gonga,wote wa kikosi cha FFU,Tabora.
Akiwasomea mashitaka,Wakili wa Serikali,Juma Masanja ameiambia mahakama ya Hakamu Mkazi mkoa wa Tabora kwamba watuhumiwa wote watatu wanakabiliwa na shitaka moja la kutochukua tahadhari stahiki katika utunzaji wa silaha.
Alisema kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo kati ya mwezi Aprili mwaka 2014 na mwezi uliopita wakiwa waajiriwa wa jeshi la polisi kikosi cha FFU Tabora.
Wakili Masanja alisema kuwa watuhumiwa wakiwa kikosi cha FFU Tabora kwa pamoja walishindwa kutumia njia za kiusalama katika utunzaji wa silaha na matokeo yake bunduki Nane aina ya SMG zikangia katika mikono ya watu ambayo haijaidhinishwa kwenye umiliki wake.
Watuhumiwa wote watatu wamekana shitaka hilo na wamenyimwa dhamana baada ya Wakili wa Serikali kupinga wasipewe kwa maelezo kwamba kuwepo kwao nje kutaingilia upelelezi wa upatikanaji wa silaha hizo.
Kufuatiwa ombi hilo la serikali, mahakama iliamuru watuhumiwa warudishwe mahabusu hadi tarehe 21 mwezi huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
Kulikuwa na uvumi wa siku nyingi kuhusu upotevu wa silaha katika jeshi la polisi mkoani hapa na askari kadha wakiwemo maafisa wa jeshi hilo walihojiwa kuhusiana na tukio hilo na baadhi yao kuachiliwa kabla ya hawa watatu kufikishwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment