Supreme Freddie Ndala Kasheba akiwa na swahiba wake enzi hizo Kikumbi Mwanza Pango 'King Kiki'.
Sikiliza kibao cha 'Dunia Msongamano'
Na Daniel Mbega
HABARI za leo wanabaraza wenzangu popote pale mlipo. Natumaini kila mmoja wetu yu bukheri wa afya kwa uwezo wa Jehova.
HABARI za leo wanabaraza wenzangu popote pale mlipo. Natumaini kila mmoja wetu yu bukheri wa afya kwa uwezo wa Jehova.
Maradhi humpata mtu yeyote yule, na kwa hakika kuugua
siyo kufa! Lakini inashangaza baadhi ya walimwengu, tena wakati mwingine wale
ambao ni watu wa karibu yetu kabisa, hutokea kuombea kwamba fulani afe. Wengi
hugeuka watabiri kila wanaposikia fulani anaumwa, na moja kwa moja mawazo yao
huwapelekea kuamini kwamba watu hao hawatapona bali watakufa!
Fikiria mtu anasikia kwamba unaumwa, lakini bila kujua
kinachokusibu, anapokuja kukujulia hali badala ya kukufariji anakwambia; “Mimi
na mke wangu tumekubaliana kuzikwa hapa hapa Dar, wewe umepanga kuzikwa wapi?!”
Labda pengine, kama ni ninyi mngemjibu vipi mtu huyu,
ambaye kwa vyovyote vile mnamtegemea kama mmoja wa wazazi ama ndugu wa karibu anayeweza
kuwa wa msaada kwako.
Lakini watu wa aina hii ni wengi sana ndani ya jamii yetu
na inaonekana wamepitiwa hata na maneno ya wimbo wa Salamu kwa wagonjwa ulioimbwa na Omar Kungubaya miaka ile ya 1970
yasemayo; “…Ajuaye Bwana Mungu kwa mzima
kuwa mfu, mgonjwa kuwa salama…”
Binafsi naamini kwamba kila nafsi itaonja mauti, kwa
sababu sisi sote ni mavumbi na mavumbini hatuna budi kurejea. Hivyo, mwenzenu siogopi
kufa bali nahofia kuishi! Nafsi iliyokufa ina heri kuliko inayoishi.
Ninachokihofia zaidi ni kwamba nitakuwa katika kundi
gani baada ya kufa. Daima wenye hekima humuomba Mungu awaongoze katika haki na
kuwaombea wengine washike mwenendo mwema, si ndivyo jamani?
Hii ndiyo sababu iliyonifanya nikikumbuke kibao cha
al-marhum Freddie Ndala Kasheba ‘Supreme’ alichokiimba mwaka 1982 akiwa na
Orchestra Safari Sound ‘wana-Dukuduku’ kisemacho Dunia Msongamano; “…Mawazo
yamenijia leo, Ya Mzee wangu alokuwa akisema, Dunia ni msongamano wa watu wenye
akili tofauti, Ukitaka kuishi vema lazima uwe na utulivu, Ukitaka kuishi vema
fikiri kabla ya kujibu, Jifunze kwa walimwengu, na walimwengu wajifunze kwako,
Dunia ni kuona mambo, Na halafu kuyasahau…”
Ni kweli kabisa, dunia ni msongamano kwa sababu imejaa
watu wengi wenye mawazo tofauti kama hawa waheshimiwa, ambao wanadhani kwamba
mtu akiugua basi atakufa tu, tena yawezekana kabisa wakawa wamempangia siku,
saa na namna kifo chake kitakavyokuwa.
Watu wa aina hii tunawashuhudia jamani, hawaendi kuwaona
wagonjwa mpaka kwanza waulizie; “Anaumwa nini?” “Vipi amekonda?” “Sijui kama atapona,
hivi umemuona Danny alivyo? Na ule wembamba wake kabaki kama chelewa?” Basi
hukumu hizi na nyingine nyingi ndizo hutawala mawazo ya watu hawa, na hata pale
wanapokuwa wanakwenda kuwatazama wagonjwa huwa ni kama maigizo fulani tu kwao,
yaani kana kwamba wamekwenda kuthibitisha hisia zao kwamba watu hao hawatapona!
Utadhani wao ni maswahiba wa Mungu na wanajua mipango yake!
Kweli naamini maneno ya Kasheba; “…Dunia msongamano, Kasema baba, Nimeyaona leo nakubali mie, Wengine
hupendelea kufurahia, Wanaposiikia fulani kafa, Kufa kwa binadamu hupangwa na
Mungu, Namuomba Mwenye Enzi anipe maisha eeh.”
Wapo watu mabingwa wa kupima homa kwa viganja! Wakatimwingine
joto la mwili linaweza kuwa kwa sababu ya jua, lakini watasema ‘unaumwa malaria’!
Wanatumia darubini za macho!
Hebu burudikeni na kibao hiki, lakini kusema kweli nahitaji
sana mchango wenu katika mada hii.
AAhhhh DUNIA MSONGAMANO
Mawazo yamenijia leo,
Ya Mzee wangu alokuwa akisema,
Dunia ni msongamano wa watu wenye akili
tofauti,
Ukitaka kuishi vema lazima uwe na utulivu,
Ukitaka kuishi vema fikiri kabla ya kujibu,
Jifunze kwa walimwengu, na walimwengu
wajifunze kwako,
Dunia ni kuona mambo,
Na halafu kuyasahau
Kibwagizo:
Dunia msongamano,
Kasema baba,
Nimeyaona leo nakubali mie,
Wengine hupendelea kufurahia,
Wanaposiikia fulani kafa,
Kufa kwa binadamu hupangwa na Mungu,
Namuomba Mwenye Enzi anipe maisha eeh
NI KILA JUMAPILI USIKOSE KUPITIA WAVUTI HII YA www.brotherdanny.com
KWA UCHAMBUZI WA MUZIKI. LAKINI TEMBELEA WAVUTI HII KILA SIKU KWA HABARI
MBALIMBALI ZA KISIASA, KIJAMII NA MICHEZO ZIKIWEMO KUMBUKUMBU MBALIMBALI.
UNAWEZA KUWASILIANA NAMI KWA SIMU/WHATSAPP/TELEGRAM 0656 331 974.
No comments:
Post a Comment