Na Hastin Liumba, Uyui
JAMII wilayani Uyui mkoani Tabora imeaswa kutodharau na kubeza shule za sekondari za kata kwani shule hizo bado ni mkombozi kwa watanzania na serikali haikosea kuanzishwa kwake.
Hayo yalielezwa na Godifrey Madafa wakati akiongea na waalimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Idete ambayo ni shule ya sekondari ya kata ya Isikizya.
Madafa alisema yeye na wenzake saba alioambatana nao wamesoma sekondari hiyo na kuhitimu mwaka 2002 ambapo kwa sasa wanafunzi waliosoma shule hiyo ya kata wameunda kikundi chao chenye watu 50 ambao wana elimu ya digrii.
Alisema wanasikia vibaya kuona jamii inabeza sekondari za kata kwa kuziita yeboyebo wakati wao sasa wana mafanikio makubwa kutokana na mchango wa elimu walioupata toka shule hiyo.
Madafa aliambatana na wenzake waliosoma shule hiyo Omari Ramadhani Kayamba, Ali Issa Mtelela, Kulwa Paschal, Juma Salum Kaweto.
Wengine ni Paschal Poul na Joha Ramadhan Mrisho ambao walihitimu kati ya mwaka 2002 na 2004.
Alisema kwa kuthamini mchango wa maisha yaliyotokana na shule hiyo waliamua kutoa msaada wa kompyuta mpakato nne zenye thamani ya sh milioni 3,600,000 na jezi seti moja na mpira vyenye thamani ya sh 175,000 na kufanya jumla kuu sh milioni 3,775,000.
Kwa upande wake mkuu wa shule hiyo Ndijenyene Luziga alipongeza hatua hiyo ya wanafunzi waliosoma shule kutembelea shule waliyosoma na kutoa misaada.
Luziga alisema wanapongeza kutoa wito kwa wanafunzi wengine huku akipongeza ujumbe huo ambao wengi wao wamefikia hatua ya kuwa na digrii na wengine wameaajiriwa.
Akisoma risala hiyo Luziga alisema shule hiyo ilianzishwa mwaka 1996 ikiwa na wanafunzi 57 na sasa wapo 613 ambapo wavulana wapo 307 na wasichana wapo 306 na walimu wapo 24.
No comments:
Post a Comment