Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inatarajiwa kuingia kambini kesho jumatano katika hoteli ya Tansoma iliyopo eneo la Gerezani jijini Dar es salaam kujiandaa na mchezo dhidi ya Misri kuwania kufuzu kwa AFCON.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars Mart Nooij, amewaita wachezaji 16 kuingia kambini kesho siku ya jumatano kwa ajili ya kupimwa afya zao na kujua maandeleo yao kabla ya kuwajumisha katika kikosi cha pamoja kitakachokua kwenye maandalizi ya mchezo dhidi ya Misri.
Wachezaji walioitwa kuingia kambini kesho ni, Mohamed Hussein, Peter Manyika, Hassan Isihaka, Jonas Mkude (Simba SC), Salum Telela, Juma Abdul, Nadir Haroub (Yanga SC), Aishi Manula, Mudathir Yahya, Frank Domayo, Kelvin Friday (Azam FC), Rashid Mandawa, Atupele Green (Kagera Sugar), Haroun Chanongo (Stand United) Malimi Busungu (Mgambo JKT) na Emmanuel Simwanda (African Lyon).
Mara baada ya kurejea kutoka nchini Afrika Kusini, kocha wa Stars Nooij aliwapa mapumziko ya siku 10, wachezaji waliokua kwenye michuano ya Cosafa mpaka Juni Mosi ambapo ndipo watajumuika na wachezaji wengine waliopo kambini.
Ifikapo Juni Mosi, 2015 Taifa Stars itaanza kambi ya moja kwa moja kujiandaa na mechi dhidi ya Misri itakayochezwa jijini Alexandria katika uwanja wa Borg El Arab Juni 14, 2015 ikiwajumuisha pia wachezaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaocheza soka la kulipwa katika klabu ya TP Mazembe ya Congo DR.
Kabla ya kuelekea nchini Misri, Taifa Stars inatarajiwa kuweka kambi jijini Addis Ababa nchini Ethiopia kuanzia tarehe 4,Juni 2015 kwa muda wa wiki moja kabla ya kuelekea nchini Misri kwenye mchezo huo dhidi ya Mafarao.
Juni 20, 2015 Taifa Stars itawakaribisha Uganda kwenye uwanja wa Aman mjini Zanzibar katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN, zitakazofanyika nchini Rwanda 2016, na mchezo wa marudiano kufanyika baada ya wiki mbili nchini Uganda.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment