Kikosi cha Simba cha mwaka 1991. Kutoka kushoto waliosimama: Mackenzie Ramadhan, Issa Kihange, Bakari Idd, Hassan Banda, Jamhuri Kihwelo 'Julio', Itutu Kigi 'Road Master', Zamoyoni Mogella 'Golden Boy', Twaha Hamidu, Mavumbi Omari, ...., Meneja Abdul Yussuf Hazali.
Waliochuchumaa: Ayoub Mzee 'Giant Killer', Hassan Affif, Method Mogella 'Fundi', Ally Machella, Raphael Paul 'RP', Khalfan Ngassa, Idd Pazi 'Father' na mmoja wa wanachama wa klabu hiyo. (Nisahihisheni kama nimekosea).
Na Daniel Mbega
LIGI ya
Tanzania Bara ilianza rasmi Januari 26 na kumalizika Septemba 21, 1991. Kwa
kweli ilikuwa ligi ngumu lakini hatma ya yote ilikuwa Yanga kutwaa ubingwa huo
uliokuwa ukishikiliwa na watani wao wa jadi, Simba, ambayo ndiyo
iliyoinyang'anya Yanga ubingwa mwaka 1990.
Baada ya
kufanya usajili mzuri ambao ulikuwa kama wa kuziba mapengo, Simba ilionekana
kujizatiti huku ikiwa na makocha wanne na meneja mpya wa timu, Azim Dewji.
Simba
ilicheza mechi kadhaa za majaribio, ambapo ilipoteza mechi mbili tu ilipofungwa
na Timu ya Taifa ya Uganda, The Cranes 1-0 na kufungwa na Pilsner 2-1 katika
Kombe la JATA.
Katika
mafanikio yake ya mechi za majaribio, Simba iliweza kushinda mechi zote tatu
ilizocheza katika ziara yake ya Kanda ya Ziwa na ilitoka sare na KCC ya Uganda
1-1, kabla ya kuishindilia Pilsner 4-0 na pia kuzifunga Kikwajuni 2-0 na MECCO
3-0 katika Uwanja wa Karume halafu ikaenda Zanzibar ambako iliichapa tena Kikwajuni
3-0 na kutoka sare ya 1-1 na mabingwa wa zamani wa Muungano, Malindi.
Kwa upande
wa Yanga, nayo ilifanya usajili ambao ulilenga katika kuwa na wachezaji
chipukizi wanaoujua mpira badala ya kufuata majina. Pia ilikuwa imepata uongozi
mpya na Mkurugenzi mpya katika juhudi zake za kutaka kufanya vizuri msimu huo.
Katika
mechi zote za majaribio ambazo Yanga ilicheza, ilifungwa mechi moja tu na
Uganda Cranes kwa magoli 2-1. Baada ya hapo ilianza mtindo wa kushinda na
kutoka sare na kubeba vikombe viwili.
Katika
michezo yake mingine ya kujipima nguvu baada ya kufungwa na Waganda, Yanga
ilifungana 1-1 na Reli na ikafungana pia 1-1 na KCC mjini Dar es Salaam kabla
ya kwenda Tanga ambako iliifunga African Sports 3-1 na kutoka suluhu na Coastal
Union.
Katika
mechi za kugombe Kombe la JATA, Yanga iliitoa Reli na kuingia fainali ambako
iliifunga Pilsner 2-1 na kutwaa kombe hilo. Halafu katika mashindano ya Kombe
la Mfuko wa Pemba ambayo yalifanyika Zanzibar, Yanga iliifunga Small Simba 2-1
na kuingia fainali ambako iliifunga Malindi 1-0 na kutwaa kombe hilo.
Katika
mechi nyingine ambazo Yanga ilicheza mjini Dar es Salaam iliweza kuzifunga
Kikwajuni 2-1, MECCO 4-0 na Small Simba 2-0. Pia iliifunga tena Reli 2-1 mjini
Morogoro.
Sasa Yanga
na Simba walikuwa wanapambana Jumamosi Mei 18, 1991 kuwania pointi tatu za mechi
ya duru la kwanza la Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara kwenye Uwanja wa
Taifa, jijini Dar es Salaam.
Timu ya
Yanga ilikuwa imejichimbia huko Zanzibar kwa wiki nzima, ambako ilicheza mechi
tatu za kirafiki na kupata ushindi mara mbili na kupoteza moja. Simba kwa
upande wake ilikuwa imepiga kambi Jijini Dar es Salaam katika maeneo ya Chuo
Kikuu (Mlimani), ambako ilikumbwa na mkasa wa kuibiwa jezi katika mazingira
yasiyojulikana.
Vinginevyo
pambano hilo lilikuwa likizungumziwa kwa mapana na marefu na hata Waziri
anayehusika na Michezo, Elimu na Utamaduni, Charles Kabeho, alifikia
kushirikishwa katika suala la kiingilio.
Yanga
ilikuwa na wachezaji wapatao saba katika mechi hiyo ambao hawakuwepo katika
mechi ya mwisho na Simba mwaka 1990, nao ni golikipa Stephen Casmir Nemes,
mabeki Selemani Mkati, Willy Mtendawema, na washambuliaji John Mngazija na Said
Sued 'Scud', winga Abubakar Salum 'Sure Boy' na mchezaji wa kiungo Issa
Athumani Mgaya 'Amiri Jeshi', ambaye hata hivyo, alikuwa analalamikiwa na Simba
na kulikuwa na wasiwasi kama angechezeshwa.
Nemes,
Mkati na Mngazija waliwahi kucheza dhidi ya Simba wakiwa katika timu nyingine
msimu wa 1990, wakati Abubakar Salum aliwahi kucheza dhidi ya Simba akiwa na
Yanga kwenye miaka ya nyuma kabla ya kwenda kuichezea AFC Leopards ya Kenya.
Wachezaji
ambao hawakuwepo kwenye kikosi hicho, lakini walikuwepo kwenye kikosi cha
Oktoba 20,1990 kilichoifunga Simba, ni Makumbi Juma Baruani 'Homa ya Jiji'
aliyeachwa kwenye usajili na Joseph Machella aliyezuiwa na FAT kutokana na
usajili wake kuwa na utata.
Kwa upande
wa Simba, wachezaji wapya walikuwa golikipa wa zamani wa timu hiyo Idd Pazi
'Father', Issa Kihange, Bakari Iddi, Jamhuri Kihwelu, Khalfan Ngassa, Gebo
Peter na Azizi Nyoni. Wote hao walikwishacheza dhidi ya Yanga wakiwa katika
timu nyingine msimu wa 1990. Gebo alikuwa mwiba mkali kwa Yanga alipokuwa
akiichezea Sigara, na siku hiyo alitarajiwa kufanya maajabu mengine.
Siku moja
kabla ya mchezo, Kaimu Katibu Mkuu wa FAT, Msafiri Mekelemi, alikuwa amesema
kwamba, mipango yote kuhusu pambano hilo ilikuwa imekamilika na tiketi zilianza
kuuzwa kuanzia saa 3.00 asubuhi pamoja na kuwepo ulinzi wa kutosha.
Wakati
timu hizo zinapambana siku hiyo, Yanga ilikuwa ikiongoza ligi hiyo ikiwa na
pointi 18 kutokana na mechi 14 ilizocheza ikiwa imeshinda sita, kutoka sare
sita na kupoteza mbili. Simba ilikuwa ikishikilia nafasi ya nne ikiwa na pointi
16 nyuma ya Coastal Union na Tukuyu Stars zilizokuwa na pointi 17 kila moja.
Hata hivyo, Simba ilikuwa imecheza mechi 12, kushinda tano, kutoka sare sita na
kupoteza moja.
Mtabiri
mmoja mashuhuri wa Dar es Salaam, Dk. Philip Kajula, alikuwa ametabiri tangu
Mei 15 kwamba, Simba ingeifunga Yanga magoli 3-0. Hivyo, mashabiki wengi wa
Simba walikuwa wamemiminika kushuhudia timu yao ikishinda kama ilivyokuwa
imetabiriwa.
Ilivyokuwa mechi yenyewe Mei 18, 1991
Siku hiyo Yanga
waliruka seng'enge tena na kufaulu kuwalaza wapinzani wao wakubwa wa soka
nchini Tanzania, Simba, ambao wakati huo walikuwa wanajiita 'Taifa Kubwa' tokea
walipotwaa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mapema mwaka huo wa
1991.
Yanga,
ambao wakati huo walikuwa wakijiita 'Umoja wa Mataifa', waliwafunga Simba
karibu kwa muda ule ule ambao mwezi Mei, mwaka 1990 walifungwa. Said Sued,
maarufu kwa jina la Scud, alifunga goli pekee na la ushindi kwa Yanga katika
dakika ya saba, dakika moja zaidi kwa muda ambao Mei 26, 1990 Mavumbi Omari
aliifungia Simba goli la ushindi (katika dakika ya sita). Hilo lilikuwa goli la
tatu kwa Sued msimu huo.
Yanga
ilitokea Zanzibar kwa mazoezi ya wiki moja na kuruka seng'enge na kisha
kutandaza kandanda la hali ya juu ambalo ilikuwa haijapata kulionyesha kwenye
Uwanja wa Taifa katika mechi zake zilizotangulia na kuwazidi Simba katika kila
hali ya uchezaji.
Wakati wa
pambano la mwisho la mwaka 1990, Yanga iliishinda Simba magoli 3-1 baada ya
kupenya kwenye tundu la seng'enge.
Issa
Athumani, akicheza mechi yake ya kwanza baada ya kurejea nyumbani kutokana na
mkataba wake kufutwa huko Uarabuni katika klabu ya Nad Oman SC, ndiye aliyetoa
mchango mkubwa katika goli la ushindi la Yanga.
Issa
alimtoka bega Method Mogella 'Fundi' aliyekuwa amembana na kutoa krosi
iliyomkuta Sued akiwa kwenye nafasi nzuri kushoto mwa goli la kusini, ambaye
aliachia kwa utulivu kiki kali ya chini chini iliyojaa wavuni huku kipa nambari
wani wa Tanzania, Iddi Pazi, akiwa amepotea maboya.
Makosa
yaliyofanywa na mabeki wa Simba mpaka goli hilo likapatikana ni kule kumfuata
Issa wote na kumwacha Sued peke yake. Mpira wa krosi ya Issa uliwapita kwa
karibu mabeki kadhaa wa Simba kabla haujamfikia Sued, ambaye hakuwa na papara
ya kuupiga ovyo.
Yanga
waliutawala kabisa mchezo huo katika dakika zote 45 za kipindi cha kwanza,
ambapo kipa wa pili wa Taifa, Stephen Nemes, hakuwa na kazi kubwa na mara
nyingi alidaka mipira ya kurudishiwa na mabeki wake au mashuti ya mbali ya
washambuliaji wa Simba. Mara nyingi sentahafu wa Yanga, Salum Kabunda 'Ninja',
alikuwa akibakia peke yake nyuma kumlinda Nemes bila madhara ya kutisha.
Issa na
Sued, ambao walikuwa wakicheza kwenye nambari 10 na 9, walikuwa miiba katika
ngome ya Simba, ambayo ilikuwa ikiongozwa na Method pamoja na akina Raphael
Paul 'RP', Twaha Hamidu, Frank Kassanga 'Bwalya' na baadaye Jamhuri Kihwelu
'Mrema'.
Simba
iliingia uwanjani kuanza kipindi cha pili ikiwa na maarifa mapya, ambapo
iliamua kucheza mtindo wa mtu-na-mtu, ambao kwa namna fulani uliwasumbua
wachezaji wa Yanga, ambao walianza kupoteana na kuelekea kuwa Simba ingeweza
kusawazisha goli hilo wakati wowote ule na washambuliaji hatari wawili wa
Simba, Zamoyoni Mogella na Hamisi Gaga 'Gagarino' walicharuka kuelekea kwa
Nemes mara kwa mara, lakini mabeki wa Yanga walikaa imara kuondoa hatari hizo
na kusababisha kona kadhaa ambazo hazikuzaa matunda.
Hata
hivyo, Yanga walifurika tena katika dakika 10 za mwisho na kulitia jamba jamba
lango la Simba hadi dakika ya mwisho, huku giza likiwa limeanza kutanda
uwanjani, kwani mechi ilichelewa kuanza kutokana na Yanga kuchelewa kuingia
uwanjani.
Ingawa
uchezeshaji ulikuwa mzuri kwa ujumla, lakini jambo moja la ajabu lililotokea ni
kwamba, mwamuzi Taji Bakari kutoka Dodoma, na mshika kibendera wake wa mstari
wa kwanza, Joseph Mapunda wa Songea, walikuwa hawaelewani mara kadhaa, licha ya
kuwa walikuwa wakichezesha pamoja mechi za kimataifa kwa miaka mingi nyuma.
Kuna
wakati Mapunda alinyoosha kibendera cha kuotea kwa upande wa Simba, lakini Taji
alimwacha Mogella aelekee golini mpaka Nemes akaunyakua mpira huo. Halafu mara
mbili Taji alimkatisha Mapunda upande wa kutupa mpira; kwanza Mapunda alikuwa
amenyoosha kibendera mpira utupwe kuelekea Simba, lakini Taji akaelekeza Yanga,
halafu wakati mwingine tena kuelekea na mwisho wa mchezo, Mapunda alinyoosha
kiendera mpira utupwe kuelekea Yanga, lakini Taji akaelekeza Simba.
Shaffi Bora aonyesha vidole vitatu, njiwa
ashindwa kuruka
Kama
ilivyo kawaida ya mechi za Simba na Yanga, siku hiyo pia vilikuwepo vituko
vingi kabla ya pambano hilo la watani wa jadi katika Uwanja wa Taifa. Pamoja na
rabsha rabsha zilizojitokeza kuhusu mahali tiketi zilipokuwa zinauzwa, lakini
baadaye watu wengi walijazana katika uwanja huo kuanzia mapema siku hiyo, na
kwa vile watu hukaa muda mrefu uwanjani siku ya mechi hiyo kubwa kabla ya jioni
kufika, basi vituko vingi hutokea hapa na pale.
Lakini
mashabiki waliokuwa na makeke zaidi walikuwa wa Simba, ambao ni kawaida yao
kuwazidi Yanga kwa mbwembwe uwanjani. Mashabiki wa Simba walikuwa na bendera,
ambapo bendera mbili kubwa zilikuwa na maandishi ya SIMBA TAIFA KUBWA.
Timu ya
Simba iliingia uwanjani saa 9.35 katika msafara wa magari nane, ambapo njiwa
aliyekuwa katika gari la wachezaji, alitolewa na kurushwa, lakini njiwa huyo
mweupe alishindwa kuruka mara mbili na kujibanza katika mlingoti wa umeme na
kutoweka baadaye wakati mechi inachezwa huku Yanga ikiongoza kwa goli 1-0.
Kabla ya
timu ya Simba kuingia, Mkurugenzi wa timu hiyo, Shaffi Bora, aliingia uwanjani
kwa makeke akiwa katika gari la kifahari aina ya Mercedes Benz likiendeshwa na
mdogo wake, Ahmed Bora. Shaffi alipokuwa katika gari hilo alionyesha vidole
vitatu na kushangiliwa na mashabiki wa Simba, pengine alikuwa akimaanisha
'magoli matatu' dhidi ya Yanga.
Yanga waliingia
uwanjani saa 10.02 pia kwa mbwembwe, ambapo wachezaji na viongozi waliruka waya
wa seng'enge upande wa kusini. Aliyetangulia kuruka alikuwa Kocha Mkuu wa timu
hiyo, Syllersaid Mziray. Halafu walifuatia wachezaji na viongozi, akiwemo
Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi ya Yanga, Mohammed Fazal Viran 'Babu'.
Wachezaji
wa Yanga walikimbia kuuzunguka uwanja na Mziray alikatisha katikati, ambako
wachezaji wa Simba walikuwa wamekatisha kuja kwenye vyumba vya kukaguliwa.
Wakati wachezaji wa Yanga walipokuwa wakielekea kwenye vyumba vya kukaguliwa
baada ya kukimbia kuzunguka uwanja, wachezaji wa Simba walichomoka kutoka
vyumbani kuelekea uwanjani na lango la kuingilia ndilo lilikuwa njia panda,
ambako walipishania huku mashabiki wakishangilia.
Kajura aeleza utabiri ulivyoharibika
Mtabiri mashuhuri
wa nyota Jijini Dar es Salaam, Dk. Philip Kajura, alisema baada ya mechi kuwa,
utabiri wake aliutoa mapema mno kiasi kwamba watu wengine walianza kutia
changamoto ili aonekane hajui.
Kajura,
aliyetabiri tangu Jumatano, Mei 15 kuwa Simba ingeifunga Yanga Mei 18 kwa
sababu nyota yake ilikuwa kali sana siku hiyo, alisema bila shaka kuna watu
ambao walimwingilia ili kumvurugia utabiri wake.
"Utakumbuka
kwamba, hapa katikati kulikuwa na siku tatu nzima, ndiyo maana wengine nao
walijitokeza kutabiri tofauti ili wanipe changamoto," alisema Kajura
Jumapili, Mei 19 alipokuwa akihojiwa kwenye hoteli ya Internationale ya Mnazi
Mmoja alikokuwa akiishi. Alipoulizwa kama alikuwa anajisikia vibaya kutokana na
utabiri wake kuharibika, Kajura alisema hajisikii vibaya.
Hata
hivyo, mara baada ya mechi hiyo, mashabiki kadhaa wa Simba walimfuata na kutaka
kumpiga kutokana na kuwadanganya, lakini akafanikiwa kuokolewa kwa kujificha
hotelini na walinzi wa hoteli hiyo wakakataza mtu yeyote kuingia ndani.
Timu
zilipangwa kama ifuatavyo: Yanga:
Stephen Nemes, Selemani Mkati/Freddy Felix 'Minziro', Kenneth Mkapa, Godwin
Aswile, Salum Kabunda, Jumanne Shango, Abubakar Salum, Athumani China, Said
Sued 'Scud', Issa Athumani (nahodha), Sanifu Lazaro. Kocha: Syllersaid Mziray.
Simba: Iddi Pazi, Raphael Paul, Twaha Hamidu, Method
Mogella, Frank Kassanga 'Bwalya', Iddi Selemani, Itutu Kigi/Jamhuri Kihwelu,
Khalfan Ngassa, Bakari Iddi/Issa Kihange, Hamisi Gaga, Zamoyoni Mogella. Kocha:
Abdallah Kibadeni.
Orodha nne
Kufungwa
kwa Simba kulikuja kuelezwa baadaye na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdallah
Kibadeni, kwamba kulitokana na kutokuelewana baina ya viongozi wa timu hiyo
katika upangaji wa orodha ya wachezaji ambao wangecheza siku hiyo.
Kwa
kawaida kocha ndiye mwenye jukumu la kupanga wachezaji kwenye mechi kutokana na
kuangalia uwezo wao, lakini kwa Simba siku hiyo ilikuwa tofauti kabisa; kocha
alikuwa na orodha yake, Mwenyekiti Juma Salum alikuja na orodha yake, Katibu
Mkuu Abdul Yusuf Hazali alikuwa na orodha yake na Katibu Mkuu Msaidizi, Hamisi
Mapande alikuwa na orodha yake!!!
Orodha ya
wachezaji 11 wa kwanza iliyopendekezwa na Mwenyekiti ilikuwa kama ifuatavyo: Iddi Pazi, Raphael Paul, Twaha Hamidu,
Method Mogella, Frank Kassanga 'Bwalya', Iddi Selemani, Issa Kihange, Khalfan
Ngassa, Zamoyoni Mogella, Malota Soma na Bakari Iddi. Wachezaji wa akiba ni
Mackenzie Ramadhani, Mavumbi Omari, Jamhuri Kihwelu, Hassan Affif na Hamisi
Gaga au Itutu Kigi.
Orodha
iliyopendekezwa na Katibu Mkuu ilikuwa kama ifuatavyo: Pazi, Mavumbi, Twaha, Method, Bwalya, Iddi Selemani, Kihange, Ngassa,
Gaga, Zamoyoni na Bakari Iddi, na wachezaji wa akiba ni Mackenzie, Raphael
Paul, Jamhuri, Malota na Affif.
Orodha ya
Katibu Mkuu Msaidizi ilikuwa kama ifuatavyo:
Pazi, Raphael Paul, Twaha, Jamhuri, Bwalya, Iddi Selemani, Kihange, Method,
Bakari Iddi, Zamoyoni na Itutu Kigi. Wachezaji wa akiba walikuwa Mackenzie,
Mavumbi, Alli Machella na Ayoub Mzee.
Orodha ya
makocha ilikuwa: Pazi, Raphael, Twaha,
Method, Bwalya, Iddi Selemani, Kihange, Ngassa, Ayoub Mzee, Gaga na Zamoyoni,
na wale wa akiba walikuwa Mackenzie, Aziz Nyoni, Jamhuri, Malota na Affif.
Baada ya
mjadala mrefu baina ya viongozi na makocha huku kila mmoja akitoa sababu zake
za kupanga orodha hiyo hatimaye ikapendekezwa orodha nyingine ya tano, ambapo
wachezaji Hassan Affif, Issa Kihange, Ayoub Mzee na Aziz Nyoni walikatwa katika
orodha ya makocha na kuingizwa Itutu Kigi, Bakari Iddi na Mavumbi Omari kutoka
kwenye orodha ya viongozi, ndipo ikapatikana orodha hiyo hapo juu, ambayo
ilionekana uwanjani.
Pamoja na
kufanya marekebisho makubwa, Simba ilijikuta ikipokea kipigo kama hicho kutoka
kwa Yanga Agosti 31 kwa goli lililofungwa na Said Sued kwa mara nyingine.
WASILIANA
NAMI SIMU/WHATSAPP/TELEGRAM 0656 331974
No comments:
Post a Comment