Profesa Ibrahim Lipumba
Na Robert Kakwesi
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola wanashiriki au kuamini ushirikina na ndiyo maana wanaowafanyia ukatili watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) hawakamatwi.
Akizungumza na wakazi wa mjini Tabora na Urambo katika ziara yake ya kuhamasisha wananchi kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura, Profesa Lipumba alisema tatizo la kukatwa viungo au kuuawa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi linatokana na baadhi ya watu katika vyombo hivyo vya dola kuhusika.
“Haiwezekani matukio yanatokea dhidi ya ndugu zetu na wahusika hawakamatwi, hii ina maana wapo wanaoamini katika ushirikina,” alisema.
Profesa Lipumba aliwaambia wakazi hao kuwa miaka 54 baada ya uhuru, watu wenye ulemavu wa ngozi wanaishi kwa hofu kwa vile baadhi ya watu wanatafuta viungo vyao kwa lengo la kutafuta utajiri.
“Watu wenye ‘albinism’ wenyewe hawana utajiri inakuwaje viungo vyao viweze kuleta utajiri, ” alisema Profesa Lipumba.
Akizungumzia hali mbaya ya maisha, Profesa Lipumba alisema umefikia hatua ya kuzalisha vijana wanaofanya uhalifu Dar es Salaam wanaoitwa Panya Road. Alidai kukata tamaa kwa wananchi na vijana ndiyo kumesababisha wajiingize katika uhalifu.
Aliwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kupiga kura ili wapate fursa ya kuiondoa CCM madarakani katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu na kuweka uongozi mpya wa ukawa.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment