Kikosi cha Pamba cha miaka ya 1980. Nawatambua baadhi kwenye picha (nisahihisheni). Waliosimama kutoka kushoto: Madata Lubigisa, Rajabu Musoma, Beya Simba 'Nissan Patrol', Nteze John, Kitwana Selemani, Philemon 'Fumo' Ferdinand Felician, Paschal Mayala na Paul Rwechungura.
Walioketi kutoka kushoto: George Gole, Khalfan Ngassa, Ally Bushiri, Alphonce Modest Pambamotosapi, Mao Mkami 'Ball Dancer', Selehe Mohammed, Hamis Nyembo na Nico Bambaga 'Machine'. Wachezaji wanne katika kikosi hiki - Musoma, Nteze, Ngassa na Modest - waliichezea Simba na wawili kati yao - Fumo na Bambaga - walichukuliwa na Yanga.
Na Daniel Mbega
KHALID
Bitebo ‘Zembwe’, James Ng’ong’a, Anthony Nyembo, Madata Lubigisa, Ibrahim
Magongo, Joram Mwakatika, Juma Mhina, Beya Simba, Abdallah Bori, Khalfan
Ngassa, John Makelele ‘Zig Zag’, George Magere Masatu, Juma Amir Maftah, David
Mwakalebela, Kitwana Selemani, Mao Mkami, Msonga Rashid, Hamza
Mponda, Raphael Paul, George Gole, Paul Rwechungura, Andrew Godwin, Hussein
Marsha ‘Smart Boy’, Nteze John Lungu, Bitta John, Deo Mkuki, Nico Bambaga
‘Machine’, Philemon ‘Fumo’ Felician… Orodha yao ni ndefu sana, lakini wote ni
miongoni mwa wachezaji waliovuma sana katika soka ya Tanzania kwa miaka mingi.
Wachezaji
wote hao, na wengine wengi, walivuma sana
hasa walipokuwa na klabu ya Pamba FC ya Mwanza, ambayo ilifahamika zaidi kama Tout Puisant Lindanda wana Kawekamo.
Timu
hiyo iliyovuma sana
katika soka ya Tanzania
kuanzia miaka ya 1970 mpaka mwanzoni mwa miaka ya 1990 kabla haijabomolewa na
klabu za Simba na Yanga, ilijivunia kitu kimoja kikubwa; kuwa na uwezo mkubwa
wa kuibua na kuvipika vipaji vya wachezaji wengi, ambao walikuja kutamba hata
kwenye timu ya taifa ya Tanzania ,
Taifa Stars.
Haikuwa
ajabu katika miaka ya 1980 kuona kwamba timu ya mkoa wa Mwanza, Mwanza Heroes,
ilikuwa ikiundwa na wachezaji wengi kutoka Pamba na wachache tu kutoka Toto
African, Co-operetive United na nyinginezo.
Ni
kutokana na kutoa wachezaji wengi nyota ndiyo maana Pamba ikaitwa ‘Chuo cha
Soka Tanzania’, hususan baada ya Yanga kuuvunja mfumo wake wa kuwalea vijana
wadogo ambao awali ulikuwa umeibua vipaji vya akina Juma Pondamali, Mohammed
Adolph Rishard, Juma Matokeo, Sunday Manara, Kassim Manara, Mohammed Mkweche,
Mohammed Yahya ‘Tostao’, na wengineo wengi.
Na
katika kipindi cha uhai wake, Pamba ilikuwa timu ya kuogopwa kutokana na
kandanda yake safi
kiasi cha timu kongwe kama Simba na Yanga
kuihofu kila wakati zilipokutana nayo. Ndio wakati ambao tulikuwa tukishuhudia
‘Big Match’! Yaani mechi kubwa ambayo iliwaweka wapenzi wengi roho juu wakiwa
hawajui nani angeibuka mshindi.
Lakini
unapozungumzia mafanikio ya timu hiyo tangu kuanzishwa kwake miaka ya 1960
mwishoni, basi yalipatikana mwaka 1990 wakati timu hiyo ilipofanikiwa kuunyakua
ubingwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Na ulikuwa ni mwaka huo
huo ambao timu hiyo ilibatizwa jina la utani la Wana Kawekamo, yaani Watoto wa
Kawekamo.
Pamba
ilipewa jina hilo
na wapenzi ake ambao waliunganisha mafanikio hayo ya timu yao na ziara ya Baba Mtakatifu Papa John
Paulo II nchini Tanzania .
Katika
ziara yake nchini Tanzania
mwaka huo, Papa John Paulo II alitembelea pia mkoa wa Mwanza na kutumia viwanja
vya Kawekamo vilivyoko eneo la Nyamanoro kuendesha misa iliyovutia maelfu ya
watu. Sasa mashabiki wakasema kwamba, mafanikio ya Pamba yalitokana na baraka
za Baba Mtakatifu.
Ingawa
Pamba ilitwaa ubingwa huo mwaka 1990, lakini huko nyuma ilikuwa moto wa kuotea
mbali japokuwa haikuwahi kutwaa ubingwa, ikiukosa kwa ncha tu karibu mara
mbili. Na kwa kudhihirisha umahiri wake, mwaka 1991 katika mashindano ya Klabu
Bingwa Afrika timu hiyo iliweza kuiadabisha klabu bingwa ya Madagascar Anser
Baluer kwa jumla ya mabao 13-0 katika raundi ya kwanza, rekodi ambayo ilichukua
miaka mingi kuvunjwa.
Pamba
ilikuwa tishio huko nyuma wakati wa Ligi ya Taifa, kabla ya kuanzishwa kwa ligi
ya Tanzania Bara mwaka 1982. Kwa mfano, mwaka 1978 katika ligi kuu ya taifa,
Pamba, ikiwa na wachezaji mahiri kama James Ng’ong’a, Anthony Nyembo, Madata
Lubigisa, Ibrahim Magongo, Issa Meloo, Khalid Bitebo, na wengineo, ilivisambaratisha
vigogo vya soka na kubebeshwa kila aina ya sifa hadi kunyakua taji la timu bora
yenye nidhamu katika ligi hiyo.
Kituko
kikubwa katika ligi ya mwaka huo 1978 iliyokuwa na timu sita katika hatua ya
mwisho kilitokea kwenye Uwanja wa Taifa wakati Pamba ilipomenyana na Yanga.
Siku hiyo Pamba ilitandaza soka safi na hadi mapumziko ilikuwa mbele kwa mabao
2-0 ambayo yalipachikwa na Anthony Nyembo, lakini wakati timu zikienda
mapumziko shabiki mmoja wa Yanga alishuka kutoka jukwaani na kukimbilia
uwanjani akiwa na kisu mkononi kwa dhamira ya kutaka kumchoma mwamuzi wa mechi
hiyo kwa madai kwamba alikuwa akiipendelea Pamba.
Kwa
bahati nzuri, Shaaban Katwila, mchezaji wa Yanga, alimdaka na kumdhibiti lakini
mkono ulioshika kisu ukateleza na shabiki huyo akataka kumchoma Katwila, na
alipogundua kwamba huyo alikuwa ni mchezaji wa timu yake ya Yanga, nguvu
zikamwishia akakidondosha kisu chini. Baadaye alitiwa nguvuni na wanausalama.
Yanga
walifutika mpira kwapani na kugoma kuendelea na kipindi cha pili kwa madai kwamba
walikuwa wakionewa na mwamuzi. Hata kabla ya mechi hiyo, Yanga walikuwa
wamelalamika kwamba waamuzi walikuwa wakiwaonea. Wakajitoa kwenye ligi na
baadaye wakafungiwa kwa miezi sita.
Baada
ya mwaka huo, Pamba ilipotea kidogo na kuiachia nafasi hiyo Pamba ya Shinyanga,
lakini ikarejea tena mwaka 1984 baada ya kupanda daraja wakati huo ikiwa bado
na baadhi ya wachezaji wake wa mwaka 1978 kama Magongo, Meloo, Bitebo, Lubigisa
na wengine walioongezeka kama Joram Mwakatika, Juma Mhina, Beya Simba 'Nissan
Patrol', Abdallah Bori 'Maalim', Khalfan Ngassa, Edward Hiza, Kitwana Selemani,
Mao Mkami ‘Ball Dancer’, Rwemaho Mkama, na wengineo.
Tangu
wakati huo Pamba haikushuka daraja na ikawa tishio kweli kweli kwa timu za ligi
daraja la kwanza Tanzania Bara. Timu hiyo ilizitambia Simba na Yanga iwe Dar es Salaam au Mwanza
na ndipo mashabiki wake walipoipachika jina jingine la Tout Puisant Lindanda.
Kwa
ujumla, Pamba iliyoanzishwa na Bodi ya Pamba Tanzania mwishoni mwa miaka ya
1960 ikijulikana kama Tanzania Lint, ilileta ushindani mkubwa wa soka katika
mkoa wa Mwanza ambako kulikuwa na timu nyingine kama Co-operative United, timu
kubwa ambayo ilififia baadaye, Toto African ambayo inajulikana kama tawi la
Yanga, Nyamaume ambayo ilijulikana kama tawi la Simba, Mwatex iliyokuwa
ikimilikiwa na kiwanda cha nguo Mwanza, na baadaye RTC Mwanza, miongoni mwa
timu zilizokuwa zikimilikiwa na Kampuni za Biashara za Mikoa.
Lakini
utawala wa timu hii ambayo ilichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo makubwa ya
soka Tanzania kwa kutoa wachezaji wengi kwenye timu ya taifa, ulivurugwa na
Simba, ambayo kuanzia mwaka 1980 iliweza kusajili zaidi ya wachezaji 20, baadhi
yao ni John Makelele ‘Zig Zag’, Raphael Paul ‘RP’, David Mwakalebela ‘MP’, Nico
Bambaga ‘Machine’, Khalfan Ngassa, George Masatu ‘Field Marshal’, Rashid
Abdallah Magongo, Hussein Marsha ‘Smart Boy’, Bitta John, Hussein Bhalo, Juma
Amir Maftah, Nteze John Lungu, Deo Mkuki, na wengineo wengi.
Yanga
nayo ikafuata mkumbo kwa kuwazoa akina David Mwakalebela, Fumo Felician, Nico
Bambaga na wengineo.
Mafanikio
yote hayo sasa yametoweka na Pamba imerejea kwenye uwanja wa Nyamagana, au
tuseme kwenye ligi ya chini tangu iliposhuka daraja mwaka 1999.
Timu
hiyo ilikuwa ishuke daraja tangu mwaka 1996, lakini safari zote mbeleko ya
Waziri wa Elimu na Utamaduni wa wakati huo, Profesa Juma Kapuya, iliinusuru
baada ya kuingilia mara kadhaa siasa za soka na kuvuruga kanuni za ligi kwa
kuibakisha timu hiyo na zingine kama Majimaji
na Milambo Ligi Kuu.
Hata
hivyo, Pamba bado itaendelea kuheshimika kama moja
ya timu zilizokuwa na mafanikio makubwa katika soka ya nchi hii.
WASILIANA
NAMI SIMU/WHATSAPP/TELEGRAM 0656 331974
barua-pepe: brotherdanny5@gmail.com
wavuti: www.brotherdanny.com
No comments:
Post a Comment