Mheshimiwa Lowassa akiwa kwenye Kanisa la SCOAN huku Nabii T.B. Joshua akihubiri. Hii ilikuwa Jumapili, Juni 12, 2011
Hii ilikuwa Juni 12, 2011 kama alivyokuwa akionekana ndani ya luninga ya emmanuel.tv
Na Daniel Mbega
MENGI
yamesemwa kuhusu kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Edward Ngoyayi Lowassa,
Mbunge wa Monduli, tangu kashfa ya Richmond/Dowans ilipoibuliwa bungeni.
Yanaendelea
kusemwa kuhusu siri ya utajiri wake na wapi anakopata fedha anazozimwaga kwenye
harambee mbalimbali. Wanasema anataka kununua urais.
Yeye mwenyewe
wakati akitangaza nia ya kuwania urais kupitia CCM Mei 30, 2015 pale kwenye
Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha alisema kwamba anachukia umaskini na
asingependa Watanzania waendelee kuukumbatia umaskini.
Wanaomfananisha
na Oscar Kambona ambaye alipingana na sera za Mwalimu Julius Nyerere za Ujamaa
na Kujitegemea bado wanaendelea kupinga hata uamuzi wake wa kutaka kuwania
urais, ikiwa ni mara ya pili tangu alipoonyesha nia mwaka 1995 (yaani miaka 20
iliyopita).
Hakuna anayepinga
kwamba Lowassa kama binadamu atakuwa amefanya makosa ndani na hata nje ya
uongozi.
Hata hivyo,
lazima tuelewe kwamba makosa yamefanywa na wengi ndani ya CCM na serikali yake
na kama kuna mtu msafi, asiye fisadi wala mla rushwa, basi ajitokeze hadharani
na kumtupia mawe Lowassa.
Lowassa hakuwepo
kwenye maamuzi makubwa zaidi wakati ubinafsishaji ulipoanza mwaka 1994 ambapo
tulishuhudia orodha ndefu ya mashirika ya umma – RTC na hata viwanda
mbalimbali, viliuzwa (waliuziana wenyewe kwa wenyewe) au zilibinafsishwa kwa
bei chee hata yale mashirika na viwanda vilivyokuwa vinazalisha kwa faida.
Ndiyo maana
mwaka 1995 pale Uwanja wa Sokoine, Mbeya wakati wa Mei Mosi, Mwalimu Nyerere
aliwauliza ni kwa nini walikuwa wanabinafsisha hata mashirika yanayozalisha.
Ndiyo. Ufisadi
mwingi umefanyika tangu Azimio la Arusha lilipozikwa Zanzibar mwaka 1991 na
kuingia kwa soko holela. Kila mmoja mwenye tamaa ya mali akatamani
kujilimbikizia. Akala, akashiba, akavimbiwa lakini hakuna aliyekinai.
‘Waliobahatika’
kugundulika wakastaafishwa ‘kwa manufaa ya umma’ lakini hawakushtakiwa. Wakapewa
likizo isiyo na malipo ili waweze kutafuna vyema mali za umma walizozikwapua.
Walipoona ndani
ya CCM wamefukuzwa, ama maovu yao yamebainika, wengi wakakimbilia upinzani na kuwa
vipaza sauti hasa vya kuitukana CCM hiyo hiyo. Wakaficha makosa yao na
kuwaaminisha Watanzania kwamba wao ni wasafi, wameonewa na waliobakia huko ndio
wabaya zaidi!
Leo hii
wanapomwandama Lowassa kwamba ni fisadi, mwizi na kadhalika, binafsi nabaki
nawashangaa.
Mungu mwenyewe
anasema: “Kutoka mbinguni Bwana aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mwenye akili, amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja…”
Sasa nani
ndani ya CCM ama hao walioko upinzani, ambao wengi wao – kama si wote –
wametokea CCM, asiye fisadi na mla rushwa? Yupo mwenye mikono safi? Kama yupo,
basi namwamuru hatua mbili mbeleeee tembea, chukua jiwe na umpige Lowassa!
Ndugu zangu,
mnasahau pia kwamba Mungu yu mwingi wa kusamehe. Anasema, dhambi zenu
zijapokuwa nyekundu kama damu zitakuwa nyeupe seluji, zijapokuwa nyekundu kama
bendera zitakuwa nyeupe kama sufi!
Lowassa amekwishajipambanua
kwamba ametubia makosa yake – kama binadamu na kwa mujibu wa maelekezo ya
Mwenyezi Mungu. Amekwenda ‘kuhiji’ Israel mwezi Februari 2008 mara tu baada ya
kujiuzulu.
Hakuishia hapo,
Juni 12, 2011 alikuwa ndani ya Kanisa la Synagogue Church for All Nations
(SCOAN) jijini Lagos, Nigeria la mhubiri maarufu duniani Temitope Balogun Joshua
maarufu zaidi kama T.B. Joshua ambako inaaminika kwamba wengi huenda kuombewa.
Wakati akiwa
huko wengi wakasambaza taarifa kwamba ‘eti Lowassa ametabiriwa na T.B. Joshua
atakuwa rais wa Tanzania’! Watu bwana!
Jamani eee,
mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Chuki zote hizi zinatokana na yeye kuonyesha
nia ya kuwania urais kupitia CCM, sasa watu wamemua kupiga mishale kila kona. Mara
Nyerere alimkataa, mara fisadi wa kutupwa, mara sijui nini…!
Jamani,
Mfalme Suleiman, ambaye anafahamika kwamba ndiye binadamu pekee aliyekuwa na
hekima duniani kuliko yeyote kabla yake ama baada yake, alikuwa na utajiri usio
kifani. Taifa la Israel lilikuwa limebarikiwa kwa ajili yake. Kuna dhambi gani
tukiwa na rais tajiri?!
Marekani ina
viongozi matajiri wengi, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje, John Kerry. Kuna dhambi
gani hapo?
Kila mmoja
ana namna alivyopata utajiri wake, na hata wewe unayesoma makala haya naamini
una njia zako za kupata kipato. Kinachotakiwa ni kuomba neema ya Mungu
atufunulie tuone kiongozi gani anayefaa.
Tusiwahukumu
watu kwa sababu zetu binafsi, na ndiyo maana Nabii Nathan alikataa kuwatia
mafuta watoto wakubwa wa Yesse mpaka Daudi alipoletwa. Mteule wa Mungu wa
kuliongoza taifa hili katika awamu ya tano atapatikana kwa neema ya Mungu,
lakini si kwa majungu na fitna.
CCM ina
makada zaidi ya 10 waliotangaza nia. Hebu tuwaachie wanachama wenyewe wamchague
wanayeona anafaa kukiwakilisha chama hicho na tusipandikize chuki na siasa za
maji-taka.
Taifa hili
ni letu sote, tusiliharibu kwa sababu binafsi maana kama tutakosa kiongozi bora
taifa litayumba hili.
Ada ya mja
kunena, nimesema yaliyo yakini.
No comments:
Post a Comment