Kikosi cha Mseto FC
Na Daniel Mbega
TANGU mwaka 1965 ilipoanza Ligi ya soka ya Taifa Tanzania ,
ubingwa umekuwa wa timu za Dar es
Salaam kutokana na timu za mkoa huo kuutwaa kila
mwaka. Hii ni kutokana na uwezo wa kimchezo wa timu hizo, hususan Simba na
Yanga.
Lakini ubingwa wa Muungano, ligi ambayo ilianzishwa rasmi
mwaka 1982 ikizihusisha timu mbili zilizoshiriki Ligi ya Bara na mbili kutoka
Ligi ya Zanzibar, umewahi kutwaliwa na klabu za nje ya mkoa wa Dar es Salaam
mara tisa katika miaka ya 1984, 1985, 1986, 1988, 1989, 1990, 1992, 1998 na
1999, wakati ule wa Tanzania Bara umetwaliwa nje ya Dar es Salaam mara tano
katika miaka ya 1975, 1986, 1988, 1999 na 2000 tangu ligi hiyo ianze mwaka
1965.
Mseto FC ndiyo ilikuwa timu ya kwanza kuupeleka ubingwa wa
taifa nje ya Dar es Salaam mwaka 1975 ikifuatiwa na Tukuyu Stars mwaka 1986,
Coastal Union ya Tanga 1988, na Mtibwa Sugar ya Morogoro 1999 na 2000.
Timu zilizotwaa ubingwa wa Muungano kutoka mikoa mingini ni
KMKM ya Zanzibar
mwaka 1984, Maji Maji ya Songea mwaka 1985, 1986 na 1998, African Sports ya
Tanga 1988, Malindi ya Zanzibar
1989 na 1992, Pamba ya Mwanza 1990, na Prisons ya Mbeya 1999.
Mwaka 1975 Mseto, ambayo ilikuwa bingwa wa mkoa wa Morogoro,
iliwashangaza mashabiki wengi wa soka nchini Tanzania ilipofanikiwa kuwa timu
ya kwanza kuupeleka ubingwa wa Tanzania mikoani na kuvunja utawala wa timu za
Dar es Salaam zilizokuwa zikiumiliki ubingwa huo kwa kuachiana (Sunderland
‘Simba’ 1965, 1966 na 1973, Cosmopolitans 1967, Young Africans ‘Yanga’ 1968,
1969, 1970, 1971, 1972, 1974).
Mashabiki wa soka wa Morogoro waliokuwa kwenye uwanja wa
Taifa Jumamosi Agosti 2, 1975 usiku wakati Mseto ilipotwaa ubingwa kwa kuifunga
Nyota FC ya Mtwara kwa mabao 3-1 katika mchezo wa fainali ya kuwania kombe hilo
lililokuwa likiitwa Karume Cup, waliingia kichaa kwa kushangilia baada ya mechi
huku wakiongozwa na Katibu wa TANU wa mkoa wao, A. Lyander.
Katika mechi hiyo Mseto ilijipatia mabao mawili kupitia kwa
Shiwa Lyambiko na moja kupitia kwa Omar Hussein, wakati ambao Said Dogoa ndiye
aliyefunga bao pekee la Nyota kwa njia ya penati. Mseto iliingia fainali kwa
kuitoa Usalama (Polisi) ya Dar es Salaam kwa mikwaju ya penati 5-3.
Kombe la ubingwa lilikabidhiwa kwao na Kamanda wa Vijana wa
TANU, Rajabu Diwani. Kwa ushindi huo Mseto ilijipatia nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika
mashindano ya Klabu Bingwa ya Soka Afrika Mashariki na Kati pamoja na Klabu
Bingwa Afrika.
Katika kipindi hicho Mseto ilikuwa na wachezaji wazuri kama
Said Gedegela, Charles Boniface Mkwasa, Hamadan, Vincent Mkude, Ramadhan
Matola, Aluu Ally, Shiwa Lyambiko, Hassan Shilingi, Omar Hussein, Spencer na
Jumanne Hassan ‘Masimenti’ waliocheza fainali. Mwingine alikuwa Miraji Salum
ambaye alikuwa na timu ya taifa, Taifa Stars, wakati huo.
Kufuatia mafanikio hayo kwenye ligi ya taifa, Mseto
ilijikuta ikiporwa wachezaji wengi wakiwemo Abdallah Hussein aliyekwenda
Coastal Union ya Tanga, Jumanne Hassan aliyekwenda Simba, Charles Boniface
Mkwasa na Miraji Salum waliokwenda Yanga na Vincent Mkude aliyekwenda Tumbaku
pia ya Morogoro.
Hata hivyo, nayo iliwapata wachezaji kadhaa nyota akiwemo
golikipa Patrick Nyaga aliyetoka Yanga baada ya kukataa kucheza chini ya kocha
Tambwe Leya kufuatia mgogoro mkubwa ulioleta mgawanyiko mwaka 1976.
Baada ya ushindi wao wa mwaka 1975, Mseto ilifanya sherehe
kubwa kuanzia Novemba 7 hadi 9 ikishirikisha maonyesho ya muziki wa dansi,
taarab, mauled na mechi za soka ambapo zilialikwa timu mbalimbali zikiwemo
Simba na Cosmopolitans kutoka Dar es
Salaam . Yanga, ambayo ndiyo ilikuwa imevuliwa ubingwa
mwaka huo, haikualikwa.
Enzi hizo Mseto ilikuwa chini ya kocha Mohammed Hussein
Hassan ‘Msomali’ na baadaye ikaongezewa nguvu na kocha wa timu ya taifa, Taifa
Stars, Bernard ‘bernt’ Trauttmann ilipokuwa ikijiandaa kuiwakilisha Tanzania kwenye
michuano ya kimataifa.
Kwenye Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati kule Mombasa , Kenya
1976, Mseto ilitolewa mapema ikiwa kundi moja na mabingwa watetezi, Yanga,
lakini angalau kwenye Klabu Bingwa Afrika ilifanikiwa kuvuka raundi ya kwanza
kwa kuwatoa mabingwa wa Madagascar Corps Enseignant kwa jumla ya mabao 6-5.
kwenye mechi ya kwanza mjini Antananarivo ,
Mseto ilitandikwa mabao 4-2, jambo lililosababisha kocha Msomali asakamwe mno
kiasi cha kujiuzulu baada ya mechi ya pili ambayo hata hivyo, Mseto ilishinda
kwa mabao 4-1 kwenye uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam .
Kuelekea mwishoni mwa miaka ya 1980, Mseto ikaanza kudorora
hasa baada ya kuwa iemshuka daraja, na baadaye kufa mwaka 1991 kutokana na
viongozi na wachezaji kutawanyika, ama katika harakati za kujitafutia maisha au
kuhama, hali iliyosababisha kukosekana kwa msimamo na umoja.
Isipokuwa mwaka 1983 ikiwa daraja la pili, ilifanikiwa kutwaa
ubingwa wa Kanda ya Mashariki wa ligi hiyo kwa kuifunga Sigara ya Dar es Salaam kwa bao 1-0
kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Mwaka 1982 pia Mseto ilikuwa
imefanikiwa kutwaa Kombe la Jamhuri mjini Morogoro.
Juni 14, 1999 viongozi wa klabu hiyo iliyoanzishwa rasmi
mwaka 1965 mjini Morogoro, walikutana kupanga mikakati ya kuifufua tena. Katibu
wa klabu hiyo, Said Gedegela, ambaye ni mmoja wa waasisi wa Mseto akiwa pia
mchezaji aliyeshiriki kuipatia ubingwa mwaka 1975, ndiye aliyekuwa na jukumu la
kuwakusanya wanachama na baadhi ya viongozi hao ili kuhakikisha wanaifufua
upya. Juhudi hizo zilikwama, lakini huenda zikafanikiwa siku za baadaye.
No comments:
Post a Comment