Kituo cha Polisi cha Mlandizi, wilayani Kibaha, Pwani.
Na Mwandishi Wetu
ASKARI wa Kikosi cha Polisi cha Usalama barabarani, Kituo cha Polisi Mlandizi wamewasotesha kwa takribani masaa mawili na nusu wanahabari kupata risiti ya malipo ya faini aliyotozwa dereva wao baada ya kudaiwa kufanya kosa la kutaka kulipita gari lingine sehemu isiyoruhusiwa.
Sakata hilo lilianza wakati polisi alipolisimamisha gari hilo katika Kituo cha Visiga, Mlandizi, wilayani Kibaha, Pwani ambapo alimuomba dereva leseni yake na kumuamuru ateremke ili ajieleze akiwa nje ya gari na hatimaye kumlipisha faini ya sh. 30,000 kwa kosa hilo.
Baada ya wanahabari waliokuwa kwenye gari hilo kumsubiri dereva kwa takribani nusu saa, waliamua kuteremka kumfuata kujua kinachoendelea, kwani walikuwa wana haraka ya kufika Dodoma muda waliopangiwa ili waungane na msafara wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwenda Singida kwenye maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa CCM.
Lakini baada ya mmoja wao kuwauliza Trafiki sababu zinazosababisha kutomwachia dereva, walijibu kwa kashfa na kejeli, wakihoji kwani nyie ni akina nani? na dereva wenu asipolipa faini basi watakaa hapo kituoni hadi jioni.
Mmoja wa wanahabari hao alilipa faini ya sh. 30,000 na kuomba risiti.
Hapo ndo songombingo ilianza ambapo Trafiki wa kike alijibu kuwa hawana risti bali kinachofanyika pale ni kuandikiwa tu taarifa ya kosa lao na kwenda Kituo cha Polisi cha Mlandizi kilichopo takribani umbali wa Km 5, na wengine waliokamatwa kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani waliamuliwa kwenda kupata risiti katika kituo hicho.
Mabishano makubwa yalitokea hapo baina ya Trafiki na wanahabari waliokuwa wanahoji ni kwa nini kitabu cha risiti wala mashine za kielekroniki havipo hapo ili kurahisisha kazi. Askari wa kike na mmoja wa kiume walijibu kuwa wasifundishwe kazi.
"Msitupotezee muda hapa, nendeni Mlandizi, mkapate hiyo risiti,"alisema trafiki wa kike. Wakati anasema hivyo kumbe mhasibu wao alikuwepo palepale Visiga, lakini bila kuwaambia ondokeni naye ili akawahudumie."
Pia, mmoja wa Trafiki aliuponda sana utaratibu wa wakosaji kulipia faini kwa kutumia mashine za elekroniki akidai kwamba ni hasara kwa trafiki na madereva ni bora mashine hizo ziishie Dar es Salaam zisipelekwe Mkoa wa Pwani.Trafiki wengine walisikika wakisema kuwa hivi hawa jamaa wanaolazimisha kupewa risiti ni akina nani, waache waende zao, wakafie mbali.
Maneno hayo yalionekana kuwaudhi wanahabari na kuamua kuondoka kwenda Kituo cha Polisi Mlandizi, kufuatilia risiti, lakini walichokikuta huko ni maajabu, hasa ya kuambiwa kuwa Mhasibu hayupo ofisini kwake amekwenda kununua peni.
Baada ya wanahabari hao kusubiri kwa takribani saa moja, waliamua kwenda kaunta kuulizia na kuomba kuzungumza na Mkuu wa Kituo ili awasaidie kupata risiti wawahi kwenda Dodoma, lakini mmoja wa askari aliyekuwa zamu aliwajibu kuwa Mkuu wa Kituo hajafika ofisini amepitia Kibaha Mjini kwenye mkutano.
Alipoombwa awasaidie kumpata mhasibu, askari huyo alitoka nje hadi ofisi ya Mhasibu alipomkosa akaamua kumpigia simu na kuwajibu kuwa ametoka mara moja kwenda kununua peni. Jambo hilo liliwashangaza sana wanahabari na kuanza kuhoji kwamba iweje kitendo cha kununua peni kitumie muda wote huo na kusababisha watu wakiwemo wao kukosa huduma tena asubuhi majira ya saa 3?
Mmoja wa wananchi aliyekwenda kituoni kupata huduma ya risiti, alisikika akilalamika kuwa tabia hiyo ya kuchelewesha kutoa huduma ipo sana kituoni hapo na kwamba wanaoonekana kabisa hawaendani na kasi ya kufanya kazi anayoitaka Rais Dk John Magufuli ya 'Hapa Kazi Tu'.
Mle ndani ya Kituo cha Polisi walisikika wakiulizana kwamba hivi haw watu wanaowasumbua na kutaka kuzungumza na mkuu wa kituo ni akina nani hawa, eti wanataka risiti, ebu tumpigie simu mhasibu aje atuondolee balaa hapa.
Baada ya muda askari mwenye E 3275 alitoka nje na kuwaambia wanahabari kuwa mhasibu amepigiwa simu atakuja muda si mrefu mhudumiwe muondoke, lakini mmoja wa wanahabari hao anayemiliki blogu ya Full Shangwe, John Bukuku, alihoji kuwa hivi ni kwanini polisi wa kituo hicho hawaendani na kasi ya Rais Dk. Magufuli? alijibu kuwa kwani kuna nini?
Baada ya muda Mhasibu aliwasili kwa Bodaboda, na alipofika aliwakebehi wanahabari kwamba anawashangaa kwa yeye kumuacha kule Visiga alikokuwa nao na kuwahi kituoni ndipo wanahabari nao wakashangaa kumuona tena kituoni hapo wakati wlipofika kituoni waliambiwa ameenda kununua peni.
Dereva alimwambia haya twende ukachukue risiti yako muondoke na watu wako. Dereva aliingia na kupatiwa risiti kutoka kwenye kitabu kipya ambacho kwa mujibu wa dereva kilionekana dhahiri kuwa ni kipya. Lakini kwa masaa yote waliyokaa wanahabari kituoni hapo (takribani masaa
mawili), hawakuwaona madereva wa magari waliokamatwa pamoja na gari lao na kuandikiwa makosa na faini pale Visiga, hawakufika Kituo cha Polisi kupatiwa risiti, kitendo ambacho kinaashiria fedha wanazolipishwa madereva kwa kutenda makosa hazitolewi risiti, hivyo mapato ya serikali kupotelea mifukoni mwa baadhi ya askari wa kikosi cha usalama barabarani.
Baada ya wanahabari hao kupata risiti majira ya saa 4:15 waliamua kuondoka kituoni hapo kuanza safari ya kwenda Dodoma kuwahi msafara wa Katibu Mkuu wa CCM, Komredi Abdulrahman Kinana uliokuwa unawasubiri kwenda Singida.
No comments:
Post a Comment