TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) linawataka wasanii wote nchini kuhakikisha wamesajiliwa na kuwa na
vibali vya Baraza kwani kufanya vinginevyo ni kuvunja sheria ya Bunge namba 23
ya mwaka 1984 iliyolianzisha BASATA ambayo inamtaka mtu yeyote anayejihusisha
na shughuli za Sanaa kuwa amesajiliwa na kupewa kibali na BASATA.
Aidha, BASATA linawaagiza
Wakuzaji Sanaa wote (Mapromota) wanaoendesha matukio ya Sanaa kama vile matamasha,
mashindano, maonyesho na utoaji tuzo nchini kuhakikisha wanafanya kazi na
Wasanii waliosajiliwa na wenye vibali vya BASATA na si vinginevyo.
Sambamba na hili, BASATA
linawaagiza wamiliki wote wa studio (Production Houses) zinazozalisha kazi za
Sanaa kuzisajili mara moja na kuhakikisha zinakuwa na vibali halali vya Baraza
la Sanaa la Taifa.
Ieleweke kwamba kwa mujibu
wa sheria hii ya BASATA, Baraza limepewa mamlaka ya kutoa vibali na kuratibu
matukio yote ya Sanaa nchini hivyo kuanzia sasa Baraza litaanza udhibiti wa
matukio haya ya Sanaa hasa katika kuongeza sharti la kuwataka waandaaji wote wa
matukio ya Sanaa kuwataka wasanii watakaoshiriki matukio yao kuwa wamesajiliwa
na kupewa vibali na BASATA.
BASATA halitavumilia kwa
namna yoyote kuona Mkuzaji Sanaa (Promota) akitumia wasanii wasiosajiliwa na
kuwa na vibali kutoka BASATA kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi hasa
sheria hiyo namba 23 ya mwaka 1984 inayoelekeza usajili na utoaji vibali kwa
wadau wote wa Sanaa.
Itakumbukwa kwamba mnamo
Mwaka 2013 Serikali kupitia Sheria ya Ushuru wa Forodha ilitangaza rasmi
kuzirasmisha sekta za muziki na filamu. Sheria hii pia inawataka wasanii wote
nchini kusajiliwa na kupewa vibali na BASATA na kinyume chake ni uvunjaji wa
sheria.
Hata hivyo, toka kuanza kwa
mchakato huu wa urasmishaji sekta ya Sanaa ni wasanii wa muziki wa injili pekee
ndiyo wamekuwa wakisajiliwa kwa wingi huku wale wa muziki wa kizazi kipya na
filamu wakisuasua bila kuwepo kwa sababu za msingi.
BASATA limekuwa likichukua hatua
kadhaa kurahisisha mfumo wa usajili wa wasanii ambapo kwa sasa msanii anaweza
kupata fomu ya usajili kupitia mtandaoni www.basata.go.tz au kwa maafisa
Utamaduni wa Wilaya na baadaye kujaza fomu na kutakiwa kuziwasilisha BASATA zikiwa
zimeambatanishwa na wasifu binafsi (CV) wa Msanii husika.
Aidha, gharama za usajili
ni kiasi cha Tsh. 75,000/- pekee ambapo fomu hupatikana kwa Tsh. 5, 000/-,
Usajili 30,000/- na kibali cha kila mwaka 40,000/-
Kwa upande wa studio na wakuzaji
Sanaa (Mapromota) gharama ni sawa na za msanii isipokuwa tofauti huwa kwenye
kibali abapo wao hulipa kiasi cha Tsh. 200.000/- kwa mwaka.
SANAA NI KAZI TUIKUZE,
TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey
L. Mngereza
KATIBU
MTENDAJI, BASATA
No comments:
Post a Comment