Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday, 17 July 2015

KOMBE LA KAGAME: YANGA NDIO WAKONGWE WA MICHUANO HII!

 Yanga wakishangilia ubingwa baada ya kuifunga Simba 1-0 kwenye fainali mwaka 2011.
 Yanga wakiwa na Kombe baada ya kuifunga Azam FC kwenye fainali mwaka 2012.

Na Daniel Mbega wa www.brotherdanny.com

MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Yanga, ndio wazoefu zaidi wa michuano ya Kombe la Kagame kwa mwaka huu kuliko timu nyingine 12 zinazoshiriki.
Mtandao wa www.brotherdanny.com unaendelea kuwaletea uchambuzi wa kihistoria katika mashindano haya ambayo mwaka 2015 yanafanyika jijini Dar es Salaam.

Yanga wanashika nafasi ya pili nyuma ya Simba kwa kucheza mechi 84, wakishinda 45, sare 14 na kupoteza 25, wakati imefunga mabao 121 na kufungwa 89.
Timu hii iliyoanzishwa mwaka 1926 na kusajiliwa rasmi mwaka 1935, mwaka mmoja baada ya kuanzishwa kwa Chama cha Soka Tanzania (FAT – sasa Shirikisho la Soka Tanzania), inashiriki mara ya 22 mashindano haya ambapo imewahi kushiriki katika miaka ya 1975, 1976, 1982, 1984, 1986, 1988, 1992, 1992, 1993, 1994, 1995, 1996, 1997, 1998, 1999, 2003, 2006, 2007, 2008, 2011 na 2012. Hakuna timu kati ya zinazoshiriki inayoifikia rekodi hiyo.
Mara nne haijawahi kushiriki kutokana na sababu mbalimbali. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2000 ikiwa bingwa mtetezi ambapo iligoma kushiriki na kung’ang’ania kombe lake baada ya kushindwa kupata fedha zao za zawadi Dola 10,000 ilizostahili kupata kwa kutwaa ubingwa huo nchini Uganda.
Mwaka 2009 haikushiriki kwa sababu ilikuwa imefungiwa kufuatia kugomea mchezo wake na Simba wa kutafuta mshindi wa tatu mwaka 2008, na mwaka 2013 haikwenda kushiriki mashindano hayo nchini Sudan pamoja na timu ya Kenya na Sudan Kusini kufuatia mgogoro wa kisiasa uliokuwa ukiendelea nchini humo.
Imetwaa ubingwa wa mashindano hayo mara tano kama Tusker FC na AFC Leopards, ambazo mwaka huu hazishiriki. Yanga ilitwaa ubingwa katika miaka ya 1975, 1993, 1999, 2011 na 2012.
Imerudia hatua ya fainali mara tatu katika miaka ya 1976, 1986 na 1992, nusu fainali mara  7, imeshika nafasi ya tatu mara tatu kama rekodi zinavyoonyesha hapa chini:

1975
Yanga ndiyo ilikuwa bingwa wa Tanzania na ilikwenda Zanzibar pamoja na mabingwa watetezi wa Klabu za Afrika Mashariki na Kati, Simba. Vijana hao wa Jangwani walikuwa wakinolewa na Tambwe Leya wa Zaire.
Kikosi chake kiliundwa na wachezaji wengi walioisaidia kutwaa ubingwa wa Tanzania kule Nyamagana, Mwanza mwaka 1974. Miongoni mwao walikuwa Elias Michael, Muhidin Fadhil, Patrick Nyaga, Leogdar Tenga, Omari Kapera, Boi Iddi 'Wickens', Juma Shaban, Jella Mtagwa, Juma Matokeo, Sunday Manara, Kitwana Manara, Gibson Sembuli, Muhaji Mukhi, Ally Yusuf, Ali Selemani, Leonard Chitete, Mohammed Kaburu, Bona Max Mwangu, Ahmed Omari, Athumani Kilambo, Adam Juma, Gilbert Mahinya, Twaha Shaaban ‘Ufunguo’, Abdulrahman Juma (nahodha), Mohammed Rishard ‘Adolf’, Moshi Hussein 'Dayani', Selemani Said Sanga ‘Totmund Wanzuka’, Adam Juma, Omari Kapera na Maulid Dilunga.
Yanga ilipangwa Kundi B pamoja na Express FC ya Uganda na Mufulira Wanderers ya Zambia ambapo katika mechi ya kwanza iliibamiza Express mabao 4-0 kabla ya kutoka sare na Mufulira kwa kufungana bao 1-1 na kuongoza kundi hilo.
Kwenye nusu fainali, Yanga iliichapa Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0 kabla ya kutoa kipigo kama hicho kwa Simba kwenye fainali.

1976
Kulikuwa na mgogoro wa ndani uliokuwa ukifukuta katika klabu hiyo tangu mwaka 1975 ilipotolewa na Enugu Rangers ya Nigeria katika Klabu Bingwa Afrika. Hadi timu hiyo inakwenda Kampala, Uganda kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, hali haikuwa shwari kabisa.
Wakati inakwenda Kampala chini ya kocha Tambwe Leya, Yanga ilikuwa na wachezaji wake wengi wa mwaka uliopita, wakiwemo Patrick Nyaga, Juma Mensah, Juma Shaaban, Selemani Said, Jella Mtagwa, Leodgar Tenga, Omar Kapera, Ezekiel Grayson, Sunday Manara, Kitwana Manara, Gibson Sembuli, Moshi Hussein 'Dayani', Ahmad Omar, Muhaji Mukhi, Twaha Shaaban ‘Ufunguo’, Ramadhan Mwinda, Sam Kampambe, Juma Matokeo, Selemani Jongo, Ali Yussuf na Boi Idd ‘Wickens’.
Ikiwa Kampala kutetea ubingwa wake, Yanga ilipangwa Kundi B pamoja na mabingwa wa Tanzania, Mseto FC ya Morogoro, Bata Bullets ya Malawi na Green Buffaloes ya Zambia.
Yanga iliichapa Mseto 2-1, ikainyuka Bata Bullets 3-1 kabla ya kuitandika Green Buffaloes 2-0. Kwenye nusu fainali iliichapa Express FC 3-0na hatimaye kutinga fainali ambako ilikubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Luo Union ya Kenya na kuutema ubingwa.
Iliporejea tu mgogoro ukaiva. Januari 22, 1976 Katibu Msaidizi wa Yanga Mohammed Misanga alitangaza kufukuzwa kwa wachezaji 21 ambao ni Patrick Nyaga, Juma Mensah, Juma Shaaban, Selemani Said, Jella Mtagwa, Leodgar Tenga, Omar Kapera, Ezekiel Grayson, Sunday Manara, Kitwana Manara, Gibson Sembuli, Moshi Hussein 'Dayani', Ahmad Omar, Muhaji Mukhi, Twaha Shaaban Ufunguo, Ramadhan Mwinda, Sam Kampambe, Juma Matokeo, Selemani Jongo, Ali Yussuf na Boi Idd.
Lakini mnamo Januari 29, 1976 wachezaji saba kati yao wakaandika barua ya kuomba radhi na kusamehewa ambao ni Ramadhan Mwinda, Selemani Said, Ezekiel Greyson 'Jujuman', Twaha Ufunguo, Selemani Jongo, Ahmad Omar na Moshi Hussein 'Dayani', ambao waliungana na wachezaji wengine akina Bernard Madale, Boniface Makomole, Charles Mwanga, Sam Kampambe, Mrisho Karaby, Yanga Fadhil Bwanga (Coastal Union), Rashid Tangale, Habibu Kondo, Charles Boniface (Mseto), Rashid Idd Chama, Ayubu Shaaban, Juma Mkambi, Hashimu Shaaban Kambi 'Ramsey' (Tumbaku), Shaaban Katwila (Mwadui), Gossage Mrisho (Tumbaku), Gondwe, Sudi Pipino, Isega Isindani, Jaffar Abdulrahman, Ibrahim Kiswabi, na Burhani Hemed.

1982
Baada ya kupotea kwa miaka mitano mfululizo, hatimaye mwaka 1982 Yanga ilirejea kwenye mashindano hayo ikiwa bingwa wa Tanzania. Yanga iliundwa na Hamisi Ramadhan Kinye, Joseph Fungo, Juma Mhina, Makumbi Juma, Omari Hussein, Yusuf Ismail Bana, Ahmad Amasha, Athuman Juma 'Chama', Fred Felix ‘Minziro’, Hussein Idd, Juma Mkambi 'Jenerali', Abeid Mziba, Juma Kampala, Charles Boniface, Allan Shomari, Rashid Hanzuruni, Isihaka Hassan 'Chukwu', Shaaban Katwila, Charles Kilinda, Juma Mkambi, Omar Hussein, na Sam Kampambe.
Katika mashindano hayo yaliyofanyika nchini Kenya, Yanga ilipangwa Kundi B ambalo lilikuwa mjini Kisumu pamoja na timu za Gor Mahia (Kenya), Bata Bullets (Malawi) na Kampala City Council ya Uganda.
Yanga ilishika nafasi ya pili nyuma ya Gor Mahia baada ya kuzifunga KCC 2-1 na Bata Bullets 1-0 kabla ya kufungwa 3-1 na Gor.
Kwenye nusu fainai ilitolewa Rio Tinto ya Zimbabwe baada ya kufungwa mabao 2-1 na ikaikosa nafasi ya tatu kwa kufungwa 2-0 na Gor Mahia.

1984
Mashindano ya mwaka 1984 pia yalifanyika Kenya ambapo Yanga iliiwakilisha Tanzania Bara ikiwa inaundwa na wachezaji Hamisi Ramadhani Kinye, Joseph Fungo, Hamisi Kizeruze, Freddy Felix Minziro, Hussein Idd, Athumani Juma Chama 'Jogoo', Ahmed Amasha 'Mathematician', Charles Boniface Mkwasa 'Master', Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’, 'Jenerali' Juma Mkambi, Elisha John 'Super Controller', Abeid Mziba, Omari Hussein ‘Keegan’, Yusuf Ismail Bana, Allan Shomari, Isihaka Hassan ‘Chukwu’, Moshi Majungu, Poisant Moyo, Juma Kampala, Alli Mchumila, na Yusuf Selemani.
Kwa mara nyingine, Yanga ilipangwa Kundi B pamoja na Nkana Red Devils ya Zambia, AFC Leopards ya Kenya, Small Simba ya Zanzibar na Berec Power Pack ya Malawi. Safari Yanga ilirudia kwenye makundi, kwani iliifunga Nkanamabao 2-1, ikafungwa 1-0 na Berec pamoja na AFC Leopards kabla ya kutoka sare ya 2-2 na Small Simba.

1986
Mwaka 1986 mashindano hayo yalifanyika jijini Dar es Salaam. Yanga, wakiwa mabingwa wa Tanzania Bara, walikuwa wananolewa na Joel Nkaya Bendera aliyechukua nafasi ya kocha Mwingereza Geoffrey ‘Jeff’Hudson. Kikosi kiliundwa na Hamisi Kinye, Joseph Fungo, Mkalla Maulid, Yusuf Ismail Bana, Freddy Felix Minziro, Isihaka Hassan, Rashid Idd Chama, Said Mrisho, Edgar Fongo, Lawrence Mwalusako, Allan Shomari, Dotto Lutta Mokili, Mohammed Yahaya ‘Tostao’, Gregory Luanda, Charles Boniface Mkwasa, Muhidini Mohammed 'Cheupe', Hussein Iddi, Juma Kampala, Omari Husseinh, Ali Mchumila, Abeid Mziba, Makumbi Juma 'Homa ya Jiji', na 'Field Marshal' Juma Mkambi.
Yanga ilipangwa Kundi A pamoja na AFC Leopards (Kenya), Silver Strikers (Malawi), Small Simba (Zanzibar) na KCC ya Uganda. Ilianza kwa kufungwa 2-1 na AFC Leopards, lakini ikaichapa Small Simba 2-0, ikaifunga Silver Strikers 3-1 kabla ya kuichapa KCC 1-0 na kushika nafasi ya pili nyuma ya Leopards.
Katika nusu fainali iliitoa Mufulira ya Zambia kwa penati 4-2 baada ya kutoka suluhu katika muda wa kawaida, lakini katika fainali ikatolewa kwa penati 4-2 na El Merreikh ya Sudan baada ya kufunga 2-2 katika dakika 120.

1988
Katika mashindano ya mwaka 1988 nchini Sudan, Yanga iliishia kwenye hatua ya makundi baada ya kushika nafasi ya tatu katika Kundi B lililokuwa mjini Wad Madani ikiwa nyuma ya El Hilal na Nakivubo Villa ya Uganda. Timu nyingine kwenye kundi hilo zilikuwa Red Arrows ya Zambia na CivoUnited ya Malawi.
Ilianza kwa kuifunga Red Arrows 5-3, lakini ikafungwa 2-0 na El Hilal kabla ya kurekebisha makosa na kuichapa Civo United 3-0. Katika mechi ya mwisho, ilifungwa 2-0 na Nakivubo Villa, hivyo ikashindwa kuingia nusu fainali.
Mwaka huo Yanga ilikuwa inanolewa na Joel Bendera na mchezaji wake wa zamani Ramadhan Mwinda ‘Maajabu’ ambaye pia alisajiliwa kwa mechi za kimataifa tu.
Wachezaji waliounda kikosi hicho walikuwa Juma Pondamali, Sahau Kambi (Reli), Mbwana Makatta (Tukuyu Stars), Lawrence Mwalusako, Yussuf Bana, Fred Felix 'Minziro', Kenneth Mkapa (Pan African), Godwin Aswile (Tukuyu), Athumani Juma 'Chama', Leonard Thadeo (Chuo Kikuu DSM), Said Mwaibambe 'Zimbwe', Issa Athumani, Said Mwamba 'Kizota', Abubakar Salum ‘Sure Boy’, Joseph Machella (Pan African), Justine Mtekere (Tukuyu), Athumani China, Abdallah Burhani (Shabana, Kenya), Abeid Mziba 'Tekero', Dennis Mdoe (Nyota Nyekundu), Edgar Fongo, Celestine 'Sikinde' Mbunga (Maji Maji), Lucius Mwanga, na Suleiman Mathew Luwongo (Tukuyu).

1992
Mwaka 1992 mashindano yalifanyikia Zanzibar ambapo Yanga ilikwenda kama bingwa wa Tanzania Bara na Simba ikitetea ubingwa wake.
Yanga ilikuwa inanolewa na Charles Boniface Mkwasa baada ya kutimuliwa kwa Sylersaid Mziray. Timu hiyo iliundwa na Thomas Wembo (Fantastic, Burundi), Steven Nemes, Sahau Kambi, Hatibu Abdallah Kibunda (Fantastic, Burundi), Deogratius Bomboneyehe 'Shundu' (Fantastic, Burundi), Freddy Felix Minzirio, Salum Kabunda, Ramadhani Kilambo, David Mwakalebela (Pamba), Method Mogella (Simba), Stephen Mussa (Tukuyu Stars), Rashid Mandanje (MECCO), Thomas Kipese, Sanifu Lazaro, Hamisi Gaga (Simba), Said Mwamba Kizota, Abeid Mziba, Kenneth Mkapa, Selemani Mkati, John Alex, Joseph Lazaro (Coastal Union), Godwin Aswile, Said Mwaibambe Zimbwe, Athumani China, Willy Mtendawema, Issa Athumani, Jumanne Shango, Abubakar Salum, Justine Mtekere, na Omar Hussein.
Yanga ilikuwa Kundi A pamoja na Rivertex FC Eldoret ya Kenya na Small Simba ya Zanzibar. Iliifunga Rivertex 4-0 lakini kafungwa 2-1 na Small Simba. Hata hivyo iliongoza kundi hilo kwa wingi wa mabao ya kufunga.
Katika nusu fainali ilikutana na El Hilal ya Sudan na ngoma ilipigwa hadi dakika 120 lakini matokeo yakawa suluhu. Yanga ikashinda kwa penati 10-9 na kukutana uso kwa uso na mahasimu wao, Simba. Dakika 120 za mchezo zilishuhudia timu hizo zikifungana 1-1 na katika mikwaju ya penati ndipo Simba ikashinda kwa mikwaju 5-4.

1993
Zamoyoni Mogella 'DHL' alipokuwa akiagizia mipira wakati wa fainali za mwaka 1993 jijini Kampala.

Mwaka 1993 Simba na Yanga ndizo ziliiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati ambayo yalifanyika mjini Kampala, Uganda.
Yanga wakati huo ilikuwa inanolewa na kocha Nzoysaba Tauzany kutoka Burundi. Kikosi cha Yanga kilikuwa na magolikipa- Steven Nemes, Sahau Kambi na Rifat Said. Walinzi- David Mwakalebela, Salum Kabunda, Joseph Lazaro, Mikidadi Jumanne, Fred Felix Minziro, Willy Martin na Selemani Mkati. Viungo - Method Mogella, Steven Mussa, Willy Mtendawema, Issa Athumani, Filotey Mogella na Hamis Gaga. Washambuliaji - Said Mwamba, Mohammed Hussein, Zamoyoni Mogella, Mtwa Kihwelu, Sanifu Lazaro, Aboubakar Salum, John Alex, Said Mrisho na Edibily Lunyamila.
Mwaka 1993 Yanga iliweka historia katika mashindano hayo kwa kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutwaa ubingwa huo katika ardhi ya kigeni, lakini pia iliweza kuwanyanyasa wenyeji itakavyo kiasi kwamba mpaka leo wachezaji kama Edibily Lunyamila na Said Mwamba Kizota bado wanakumbukwa huko.
Ni mwaka huo pia ambapo mchezaji ghali aliyetokea Simba, Zamoyoni Mogella ‘Morgan’, alipachikwa jina la ‘DHL’ akifananishwa na kampuni ya usafirishaji wa vifurushi. Hii ilitokana na umahiri wake wa kutoa pasi za uhakika kwa wenzake pamoja na kuiunganisha vyema timu.
Timu hii kwanza iliondoka kwa mizengwe baada ya kukosa fedha za kuisafirisha hadi Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, alipojitolea kuisafirisha.
Yanga ilisafiri kwa treni mpaka Mwanza, ambako ilipanda meli mpaka Jinja kabla ya kujipakia kwenye basi lililowapeleka Kampala. Wafadhili wa Yanga, Abbas Gulamali, Murtazar Dewji, Muhsin Hassanali, Mohammed Virani 'Babu' na Ramesh Patwa walikuwa wameweka 'ka-mgomo baridi'.
Tofauti na Yanga, Simba wenzao, wakiwa na mfadhili wao mkuu, Azim Dewji, walikwenda Kampala kwa kutumia ndege ya kukodi, ambayo iliwachukua kutoka Mwanza hadi Kampala.
Kichekesho kilikuwa wakati wa kurudi. Simba, ambayo ilitolewa mapema baada ya kufungwa na Express ya Uganda na kuvuliwa ubingwa, iliondoka kwa njia iliyokujia Yanga; yaani ilipanda basi mpaka Jinja kisha ikatumia usafiri wa boti hadi Mwanza kabla ya kukwea gari moshi lililowafikisha Dar es Salaam. Yanga wao walirejea kwa ndege moja kwa moja kutoka Kampala.
Kwa ujumla mashindano ya mwaka huo yalikuwa hayatabiriki kutokana na kushirikisha timu zenye uzoefu mkubwa na mashindano ya kimataifa.
Yanga ilikuwa Kundi A pamoja na Villa na Malindi baada ya Nkana kujitoa. Kwanza ilifungwa 3-1 na Villa, lakini ikailaza Malindi 2-1 na kushika nafasi ya pili kwenye kundi hilo. Katika nusu fainali ikaifunga Express ya Uganda 3-1 na kwenye fainali ikaifunga Villa 2-1 na kutwaa ubingwa.

1994
Mwaka 1994 mashindano yalifanyika nchini Sudan ambapo Yanga ilikwenda kutetea ubingwa wake huku Simba ikiwakilisha Tanzania Bara kama bingwa wa ligi.
Ikiwa inanolewa kwa mara nyingine na Tambwe Leya wa Zaire, Yanga iliundwa na Stephen Nemes, Riffat Said, Ngandou Kazadi Ramadhani (Prince Louis, Burundi), Constantine Kimanda (Vital'O, Burundi), Mikidadi Jumanne (Reli), Kenneth Mkapa, Willy Martin (Ushirika), Willy Mtendawema, Jobe Ayoub ‘Kwasakwasa’ (Pan African), Salum Kabunda, Selemani Mkati, Method Mogella, Nico Bambaga (Pamba), Stephen Mussa, Sekilojo Chambua, David Mjanja, Ally Yusuf 'Tigana', Sinisha Blagojevic (Yugoslavia), James Tungaraza, Issa Athumani, Sanifu Lazaro, Lance Evans Ponera, Said Mwamba 'Kizota', Fumo Felician, Edibily Lunyamila, Mohammed Hussein, Ally Manyanya, na Mohammed Salum.
Yanga ilikuwa Kundi B lililokuwa mjini Port Sudan pamoja na El-Hilal Port Sudan, Mebrat Hail au Electric – ELPA (Ethiopia) na Shangani (Zanzibar).
Yanga ilianza kwa kutoka suluhu na Electric, ikafungana bao 1-1 na El Hilal kabla ya kuifunga Shangani 2-1 na kuongoza kundi hilo. Kwenye nusu fainali, baada ya kufungana 1-1 na Express, Yanga ikajikuta ikitolewa kwa penati 5-4. Hata hivyo, ilifanikiwa kushika nafasi ya tatu baada ya kuifunga tena Shangani mabao 2-1.

1995
Mashindano ya mwaka 1995 yalifanyika Tanzania katika miji ya Dar es Salaam na Mwanza. Yanga ilikuwa Kundi B mjini Mwanza pamoja na Kenya Breweries, Malindi ya Zanzibar na El Mourada ya Sudan.
Ikumbukwe kwamba, timu hiyo ilikuwa imewatimua wachezaji wengi wakongwe kufuatia mgogoro wa mwaka 1994 na sasa chini ya kocha Tambwe Leya, ilisajili wachezaji wengi kutoka Yanga B kiasi cha kupachikwa jina la ‘Yanga Yosso’.
Wachezaji waliotoka Yanga B ni Anwar Awadh Gessan, Silvatus Ibrahim Mwinamumba 'Polisi', Mzee Abdallah Ngauja, Maalim Saleh 'Romario', Ally Jabir Katundu, na Nonda Shaaban 'Papii'. Wachezaji wa zamani waliokuwa wamebakia ni Kenneth Mkapa, Ally Yussuf 'Tigana', David Mjanja, Sekilojo Chambua, Mohammed Hussein, Fumo Felician na James Tungaraza 'Boli Zozo'.
Wachezaji wengine wapya walikuwa Godwin Mashoto (Milambo), Sadiq Kalokola (Pan African), Mahmoud Nyalusi (Sigara), Reuben Mgaza (Coastal Union), Mathias Mulumba (Reli), Bakari Malima 'Jembe Ulaya' (Pan), Kaunda Mmwakitope (Ushirika), Salvatory Edward (Sigara), Willy Martin (Ushirika), Steven Nyenge (Ushirika), Benny Luoga (Sigara), Peter Louis Fwampa (Tukuyu), Dominic Mbawala, Vincent Peter (Lipuli), na Sammi Bitumba Iyela (Burundi).
Katika michuano hiyo, Yanga ilianza kufungwa 2-1 na Kenya Breweries, ikatoka sare ya 1-1 na Mourada pamoja na Malindi, hivyo ikashindwa kuingia nusu fainali baada ya kushika nafasi ya tatu.

1996
Mwaka 1996 mashindano hayo pia yalifanyika nchini Tanzania. Kama ilivyokuwa mwaka 1995, Yanga ilipangwa Kundi B mjini Mwanza, ikiwa na timu za Gor Mahia, Express na Alba ya Somalia. Ilianza kutoka sare ya 1-1 na Gor Mahia, ikazifunga Alba na Express bao 1-0 kila moja na kushika nafasi ya pili nyuma ya Gor.
Katika nusu fainali, ilitolewa na APR ya Rwanda ambayo ilikuwa inashiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza kabisa. Katika dakika 120 timu zilifungana 2-2, lakini kwenye penati Yanga ikafungwa 4-2. Yanga ilikosa hata nafasi ya tatu baada ya kufungwa 4-0 na Gor Mahia.
Wakati huo ilikuwa inafundishwa na Sunday Kayuni na ilikuwa na wachezaji kama Sadiq Kalokola, Mfaume Athumani (CDA), Joseph Katuba (Simba), Baldwin Sinsinawa (Mufulira Wanderers, Zambia), Anwar Awadh, Kenneth Mkapa, Sylvatus Ibrahim, Kaunda Mwakitope, Sekilojo Chambua, Yussuf Macho (Waziri Mkuu), Salvatory Edward, Mohammed Hussein, Edibily Lunyamila (Malindi), Thabit Bushako (Toto African), Idelfonce Amlima (Bandari Mtwara), Sanifu Lazaro (AFC), Abdallah Msheli (CDA), Kenneth Mkapa, Ally Jabir Katundu, Mzee Aballah, Peter Louis, James Tungaraza, Bakari Malima, John Mwansasu (Tukuyu), Reuben Mgaza, Abdul Shaaban (Reli), Stephen Nyenge, Ally Ngaoneka (Tukuyu), na Dominick Mbawala.

1997
Mwaka 1997 Yanga bado ilikuwa chini ya Sunday Kayuni aliyekuwa akisaidiwa na Jella Mtagwa na Juma Pondamali 'Mensah'. Timu hiyo iliundwa na Joseph Katuba, Mfaume Athumani, Sylvatus Ibrahim, Kenneth Mkapa, Anwar Awadh, Kaunda Mwakitope, Nebboh Bukumbi (Tiger FC), Abdilah Ismail, Kazembe Athumani (huru), Akida Makunda (Simba), Paul John Masanja (Shinyanga), Abdallah Msheli, Sekilojo Chambua, Yussuf Macho, Sanifu Lazaro, Said Mwamba, Salvatory Edward, Edibily Lunyamila, Steven Nyenge, Thabit Bushako, Mohammed Hussein, Idelfonce Amlima, Abdul Shaban, James Bwire Tungaraza, Mzee Abdallah, Dominick Mbawala, na Peter Louis.
Mashindano ya mwaka huo yalifanyika nchini Kenya ambapo Yanga ilikuwa Kundi A pamoja na East Coast ya Somalia na JS Saint Pierroise ya Reunion ambayo ndiyo iliyoongoza kundi hilo. Yanga ilifungwa 3-1 na JS kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 na East Coast, hivyo kushika nafasi ya pili.
Katika robo fainali, Yanga iliifunga kwa penati 4-2 Mourada baada ya kutoka suluhu, lakini kwenye nusu fainali ikakubali kipigo cha mabao 2-1 mbele ya AFC Leopards. Hata hivyo, iliambulia nafasi ya tatu baada ya kuifunga Express ya Uganda 3-1.

1998
Mashindano ya mwaka 1998 yalifanyika mwishoni mwa mwaka 1997 huko Zanzibar, hivyo usajili wa Yanga ulikuwa bado vile vile.
Yanga ilitolewa kwenye nusu fainali na wageni wa michuano hiyo, Rayon Sport ya Rwanda baada ya kufungwa mabao 3-1, halafu katika kutafuta mshindi wa tatu, Yanga ikalimwa bao 1-0 na Coffee FC ya Ethiopia.

1999
Pamoja na ukweli kwamba kulikuwa na mgogoro wa uongozi klabuni hapo, lakini Yanga ilikwenda Kampala, Uganda kwenye Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati ikiwa vizuri kwenye kikosi chake. Iliundwa na Manyika Peter, Mfaume Athumani Samatta, Edibily Lunyamila, Idd Moshi, Akida Makunda, Paul John Masanja, Anwar Awadh, Abdallah Msheli, Abdul Maneno Kibavu, Joseph Simon, Bakari Malima, Mohamed Hussein, Sekilojo Chambua, Joseph Katuba, Salvatory Edward, Said Mhando, Banza Tshikala, Kalimangonga Ongala na Raymond Ndunguru (Abajalo ya Sinza, Dar es Salaam), Ally Mayayi (CDA), Said Mwamba Kizota (Kariakoo Lindi), Deogratius Ngassa (Msimbazi Rovers, Dar es Salaam), Ephraim Makoye (Kagera), Sadiq Belanov na Tambwe Patrice (Prince Louis, Burundi), Goliath Mwakipesile (Pan African), Eustace Bajwala, Yussuf Fundi na Sango Baligwa (huru).
Katika mashindano hayo, Yanga ilipangwa Kundi D pamoja na Rayon Sport baada ya Red Sea ya Eritrea kujitoa. Katika mechi ya kwanza Yanga ilifungwa 3-0, lakini nayo ikapata ushindi kama huo huo, hivyo ikabidi kiongozi wa kundi hilo apatikane kwa kurusha shilingi. Rayon ikaongoza.
Kwenye robo fainali, Yanga iliichapa El Hilal ya Sudan kwa mabao 2-1 kabla ya kuitandika Vital’O ya Burundi mabao 3-2 kwenye nusu fainali. Katika fainali, dakika 120 zilishuhudia Yanga na SC Villa zikifungana 1-1, lakini kwenye penati Yanga ikashinda mikwaju 4-1 na kuongeza upinzani wake kwa Villa.

2000
Mashindano ya mwaka 2000 yalifanyika nchini Rwanda, lakini Yanga, kama bingwa mtetezi, iligoma kwenda na ikaling’ang’ania kombe ikitaka ipatiwe zawadi yake ya Dola 10,000 kwa kutwaa kombe hilo mwaka 1999 kule Kampala.
Wadhamini wa mashindano hayo, kampuni ya SmithKline Becham ya Kenya walionyesha ubabaishaji mkubwa, kwani hata washindi wa pili, SC Villa walipewa hundi ya Dola 6,000 lakini walipopeleka benki wakaambiwa hakukuwa na fedha za kutosha.

2003
Mwaka 2003 mashindano yalifanyika nchini Uganda na Yanga ndio walikuwa mabingwa wa Bara. Timu hiyo iliyokuwa inanolewa na beki wa zamani wa kimataifa wa Malawi, Jackson Lloyd Chamangwana, ilikuwa inaundwa na wachezaji Hussein Katandula Thade, Jumanne Mrisho, Abubakar Twaha 'Mtiro', Fred Mbuna, Salum Sued, Ally Mayai, Waziri Mahadhi, Kudra Omar, Salum Athuman, Abuu Ramadhan, Sekilojo Chambua, Herry Morris, Aaron Nyanda, Salvatory Edward, Mwinyi Rajab, Mengi Matunda, Quresh Ufunguo, Omar Changa, na wengineo.
Katika mashindano hayo, Yanga walipangwa Kundi A ambalo mechi zake zilikuwa kwenye Uwanja wa Namboole (Nelson Mandela) yapata kilometa 16 mashariki mwa Kampala. Ilikuwa na timu za Khartoum 3 ya Sudan, Red Sea ya Eritrea, SC Villa ya Uganda na Mlandege ya Zanzibar.
Yanga ilianza kwa kufungwa 2-0 na SC Villa, ikatoka suluhu na Khartoum 3, ikaifunga Mlandege 2-1 kabla ya kufungwa na Red Sea 2-1 na kushindwa kugusa nusu fainali.

2006
Mwaka 2006 mashindano hayo yalifanyika nchini Tanzania ingawa awali yalipangwa kufanyika nchini Uganda. Tanzania iliwakilishwa na timu tatu ambazo ni Yanga, Simba na Moro United.
Yanga iliyokuwa inanolewa na Jackson Lloyd Chamangwa na Sekilojo Chambua, ilikuwa imewatema wachezaji Salum Kidungwe, Samson Mwamanda, Benito John Mwansaga, Athuman Majani, Chesido Mathew, Ngade Chabanga Dyamwale, Noel Pompi, Benson Mungai, Paschal Ochieng (Kenya) na Aaron Nyanda. Nafasi zao zilijazwa na Ahmed Ali ‘Mkweche’ (Zanzibar), Edwin Namiti Mukenya na Bernard Sechange Mwalala (Kenya), Mbarouk Suleiman (Zanzibar), Thomas Maurice (Zanzibar), Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’ (Zanzibar), Hamis Yussuf (APR Rwanda), Lulanga Mapunda (Moro United), Shadrack Nsajigwa (Moro United), Ivo Mapunda (Moro United), Credo Mwaipopo (Twiga), Gaudence Mwaikimba (Ashanti United), Maridadi Bukenya (Uganda), na Waziri Mahadhi (huru). Wachezaji wa zamani walikuwa Benjamin Haule, Kudra Omary, Abubakar Twaha ‘Mtiro’, Fred Mbuna Swale, Amri Kiemba, Herry Morice, John Barasa, Abuu Ramadhan, Mohammed Banka, Deogratius Lucas, Gulla Joshua Mduma, Andrew Carlos, na Said Maulid Kalukula ‘SMG’.
Yanga ilipangwa Kundi A pamoja na Saint George ya Ethiopia, Ulinzi Stars ya Kenya, Polisi ya Zanzibar, na Inter Stars ya Burundi. Ilianza kwa kutoka suluhu na St. George, ikaifunga Polisi 1-0, Ikaifunga Inter Stars 2-1 na kuibamiza Ulinzi 3-1.
Kwenye robo fainali timu hiyo ikatolewa na Polisi FC ya Uganda kwa kufungwa bao 1-0.

2007
Mwaka 2007 mashindano hayo yalifanyika nchini Rwanda ambapo Yanga ilikwenda kama bingwa wa Tanzania Bara. Timu hiyo iliundwa na Ivo Mapunda, Lulanga Andrew Mapunda, Edwin Namiti Mukenya, Waziri Omari Mahadhi, Hamisi Yusuf Shabani, Amri Kiemba Ramadhan, Said Maulid Kalukula, Gaudence Xavery Mwaikimba, Abdubakar Twaha 'Mtiro', Fredy Wilfred Mbuna, Abuu Ramadhan Mauya, Bernard Sechangi Mwalala, Thomas Maurice Mnkay, Benjamin Haule Hellen, Nsajigwa Joel Shadrack, Nadir Haroub Ally 'Cannavaro', Gulla Joshua Mduma, Credo Duncan Mwaipopo, Emmanuel Swita. Wachezaji wapya walikuwa Athuman Idd Chuji (Simba), Wisdom Kihaya Ndhlove (Bakili Bullets, Malawi), James Sebastian Chilapondwa (Bakili Bullets, Malawi), Mrisho Halfan Ngassa (Kagera Sugar), Amir Mrisho Maftah (Mtibwa), Jackson Abraham Chove (Bakili Bullets, Malawi), Hussein Swedi Said (Ashanti United) na Abdi Kassim Abdi (Mtibwa).
Awali Yanga ilipangwa Kundi C pamoja na Bederie ya Eritrea na Banaadir Telecom ya Somalia, lakini timu hizo zikajitoa, hivyo Yanga ikahamishiwa kwenye Kundi A pamoja na CDE ya Djibouti, APR ya Rwanda, URA ya Uganda na Vital’O ya Burundi.
Iliifunga CDE 4-0, ikatoka sare ya 2-2 na URA, ikafungwa 1-0 na APR kabla ya kutoka sare ya 1-1 na Vital’O, hivyo ikaishia kwenye hatua ya makundi.

2008
Mwaka 2008 Yanga ilianza kufundishwa na Jack Chamangwana, baadaye akaja Dusan Kondic wa Serbia.
Wakati inashiriki mashindano ya Kombe la Kagame yaliyofanyika katika miji ya Dar es Salaam na Morogoro nchini Tanzania, Yanga ilikuwa inanolewa na Kondic na iliundwa na Ivo Mapunda, Lulanga Andrew Mapunda, Edwin Namiti Mukenya, Waziri Omari Mahadhi, Hamisi Yusuf Shabani, Laurent Kabanda, Jerson Tegete, Maurice Sunguti, Emmanuel Swita, Aime Lukunku, Said Maulid Kalukula, Gaudence Xavery Mwaikimba, Abdubakar Twaha 'Mtiro', Fredy Wilfred Mbuna Swale, Abuu Ramadhan Mauya, Bernard Sechangi Mwalala, Thomas Maurice Mnkay, Benjamin Haule Hellen, Nsajigwa Joel Shadrack, Nadir Haroub Ally 'Cannavaro', Gulla Joshua Mduma, Credo Duncan Mwaipopo, Athuman Idd Chuji, Wisdom Kihaya Ndhlove, James Sebastian Chilapondwa, Mrisho Halfan Ngassa, Amir Mrisho Maftah, Jackson Abraham Chove, Hussein Swedi Said na Abdi Kassim Abdi.
Timu hiyo ilipangwa Kundi C pamoja na APR na Miembeni na ilianza kwa kutoka sare ya 2-2 na APR kabla ya kuifunga Miembeni 1-0. Katika robo fainali, Yanga iliifunga Vital’O mabao 2-0, lakini ikatolewa kwenye nusu fainali na Tusker FC ya Kenya kwa kufungwa bao 1-0. Siku hiyo Yanga iliwakilishwa na Ivo Mapunda, Shadrack Msajigwa, Wisdom Ndhlovu, George Owino, Nurdin Bakari, Shamte Ally, Geoffrey Bonny, Athman Iddi Chuji/Vincent Barnabas, Kigi Makasi/Abdi Kassim, Boniface Ambani/Gaudence Mwaikimba, na Mrisho Ngassa. Tusker iliyokuwa inanolewa na Jacob ‘Ghost’ Mulee, iliwakilishwa na: Boniface Otieno, Ibrahim Shikanda, John Njoroge, Joseph Shikokoti, Humphrey Okoti, Japhery Oyando/Crispin Odula, Edward Kauka, Osborne Monday, Simon Mburu, John Kio/Robson Ndondo, Justus Anene/Hassan Aden.
Yanga ikagoma kukutana na Simba katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu baada ya Simba nayo kutolewa na URA kwa bao 1-0. Hatua hiyo iliwakasirisha Cecafa ambao waliifungia Yanga kushiriki mashindano hayo kwa misimu mitatu.

2009
Yanga haikushiriki mashindano ya mwaka 2009 huko Sudan kutokana na kutumikia adhabu ya miaka mitatu. Nafasi yake ikachukuliwana Prisons ambayo nayo iliishia kwenye makundi.

2011
Mashindano ya mwaka 2011 awali yalikuwa yafanyike Zanzibar, wakapewa uenyeji Sudan, lakini baadaye nao wakashindwa, hivyo Tanzania ikabidi iwe mwenyeji.
Yanga ilipangwa Kundi B pamoja na El Merreikh ya Sudan, Buanamwaya ya Uganda na Elman ya Somalia. Ilianza kwa kutoka sare ya 2-2 na Merreikh, ikaifunga Elman 2-0 na kuifunga Bunamwaya 3-2, hivyo kuongoza kundi hilo.
Kwenye robo fainali iliitoa Red Sea ya Eritrea kwa penati 6-5 baada ya kutoka suluhu katika muda wa kawaida, na kwenye fainali ikaifunga Simba 1-0 na kutwaa taji hilo kwa mara ya nne.

2012
Kwa mara nyingine tena mashindano ya mwaka 2012 yalifanyika nchini Tanzania, ambapo mabingwa watetezi, Yanga, walipangwa Kundi C pamoja na APR, Al Salaam Wau ya Sudan Kusini na Athletico Olympic ya Burundi. Ilianza kwa kufungwa 2-0 na Athletico, ikaifunga Al Salaam 7-1 na kuifunga APR 2-0.
Kwenye robo fainali ilikutana na Mafunzo ya Zanzibar na kuifunga kwa penati 4-2 baada ya kutoka 1-1 ndani ya dakika 90. Ikaichapa APR 1-0 kwenye nusu fainali na katika fainali ikaifunga Azam FC mabao 2-0.

2013
Mashindano ya mwaka 2013 yalifanyika Sudan, lakini Tanzania, Kenya na Sudan Kusini hazikupeleka wawakilishi wake kutokana na mgogoro uliokuwa ukiendelea nchini humo, hasa kwa kuzingatia kwamba Kenya na Tanzania zilikuwa zikiisaidia Sudan Kusini katika vita vyake na waasi. Kwa hiyo Yanga ikashindwa kwenda kutetea ubingwa wake.

Kikosi cha sasa
Benchi la ufundi la Yanga liko chini ya Mholanzi Hans Van De Pluijm anayesaidiwa na Salvatory Edward na Juma Pondamali. Wachezaji wanaounda kikosi hicho ni Ally Mustapha "Barthez", Salum Telela, Oscar Joshua, Rajab Zahir, Kelvin Yondan "Cotton", Mbuyu Twite, Andrey Coutinho, Kpah Sherman, Jerson Tegete, Said Bahanuzi, Juma Abdul, Omega Seme, Pato Ngonyani, Nizar Khalfan, Mrisho Ngassa, Hamis Thabit, Nadir Haroub "Cannavaro" (nahodha), Deogratius Munishi "Dida" na Simon Msuva.

KUMBUKUMBU HIZI ZIMEANDALIWA NA MTANDAO WA www.brotherdanny.com. Tafadhali ukirejea weka chanzo cha habari.


No comments:

Post a Comment