Ikulu ya Tanzania
Na Daniel Mbega
TAFSIRI ya
Kiswahili sanifu ya ‘ukahaba’ au ‘malaya’ inaelezwa kwamba ni tendo la kufanya
ngono nje ya ndoa au uhusiano unaokubalika katika jamii, tena na watu
mbalimbali na kwa malipo. Sifa ya umalaya au ukahaba imekuwa ikinasibishwa
zaidi na wanawake hasa kwa vile wanaume wamekuwa wakidai kuwa wao ni wa wake
wengi kwa asili.
Kwa bahati
mbaya katika miaka ya karibuni maana ya maneno hayo imetoka katika asili
kutokana na ama kupanuka kwa lugha ya Kiswahili au jamii kuzalisha maneno
mengine mapya, ndiyo maana hata mwanasiasa ambaye hatulii na chama kimoja,
mwenye kubadili vyama kama ‘nguo za ndani’, amekuwa akiitwa ‘malaya’.
Neno
‘malaya’ ndilo kuntu linaloweza kuelezea tabia za wanasiasa wanaohama vyama
kama nyumba za kupanga ingawaje neno hilo limeanza kupotea taratibu na limebaki
kuwa ni msamiati unaotumiwa zaidi na wazee ambao, kwa sababu zilizo wazi,
hawawezi kutumia lugha za msimu na hapa kwenye lugha za msimu ndiyo tunakuja
kwenye maana ya neno kirukanjia.
Kirukanjia
ni malaya au ukipenda kahaba. Hili limetokana na jina la ndege aitwaye ‘kirukanjia’
au ‘mbarawaji’. Neno ‘njia’ limetumika kumaanisha mtu mwenye kubadilisha njia
kila mara. Ni neno la msimu au la mtaani.
Kwa
maelezo hayo mafupi ni kwamba niko sahihi kabisa kuwaita wanasiasa wanaobadili
vyama kila wakati ni ‘malaya wa siasa’, ambao kimsingi tabia zao hazina tofauti
kabisa na malaya au makahaba wenyewe wanaozungumziwa katika tafsiri halisi.
Wahenga
wanasema, umalaya wa siasa umekuwepo ulimwenguni pengine tangu kuanzishwa kwa
Siasa yenyewe. Umalaya wa kisiasa unaweza kutajwa kwamba ni "hali ya kutoa
huduma au dhamana ya uongozi kwa nia ya rushwa, kwa minajiri ya kupata maslahi
ya kimwili au rasilimali".
Kwa hiyo
basi, wanasiasa wa aina hii ambao wako tayari kuuza ushawishi wao na madaraka
ya kwa nia ya kupata maslahi binafsi wanatambulika kama Malaya wa Kisiasa.
Umalaya
ndiyo fani ya kwanza kabisa duniani, na siasa ndiyo fani ya pili na zote
zinafanana. Siasa na umalaya ndizo kazi pekee ambazo kukosekana kwa uzoefu
kunaonekana kama ndiyo kunaonekana kama ndiyo talanta, na siyo ajabu hata
wanaofanya kazi ya ukahaba wanaweza kudanganya kwamba ni ‘bikira’ ili kuwavutia
wateja wao wakati siyo kweli!
Sikiliza
kisa hiki. Mzee mmoja tajiri alikutana na binti mbichi akamtamani, akamwambia
angempatia Shilingi milioni moja kama angekubali kulala naye kwa usiku mmoja
tu. Binti yule akatafakari kwa muda, halafu akasema “Hakuna taabu”. Sasa mzee
akamwambia, “Unaonaje ikiwa nitakupa Shilingi elfu tano?” Yule binti akamaka,
“Hivi wee babu umenionaje mimi?” Badala yake yule mzee akasema, “Tayari
tumeshajua wewe ni nani. Sasa tunapatana bei.”
Tabia za
wanasiasa malaya hazina tofauti na malaya anayefanya ngono, ambaye daima lazima
amsifie mwanamume aliyenaye sasa kwamba ni bora kuliko yule aliyekuwa naye.
Wanaume nao kwa ulimbukeni wao wa asili, hujiona ufahari wakati tayari
wamekwishaibiwa!
Naam.
Tanzania tunao malaya wa kisiasa, wengi sana, kama ilivyo katika nchi nyingine
ulimwenguni. Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992,
tumeshuhudia wanasiasa wengi wakiondoka kwenye Chama cha Mapinduzi (CCM) na
kwenda upinzani. Hawa walikuwa na kila sababu ya kufanya hivyo, kwani ilikuwa
ni lazima watoke kwenye chama kimoja waende wakaanzishe vyama vingine.
Lakini
kuibuka kwa wanasiasa malaya kumekuwa kukijitokeza kila unapofika mwaka wa
uchaguzi. Tumeshuhudia hayo kwenye uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995
na tunaendelea kushuhudia hata sasa. Wanatoka CCM wanakwenda upinzani,
wanakitukana chama tawala, halafu baadaye wanarejea na kuutukana upinzani!
Wakati
vyama vya siasa vikiendelea kupanga safu za wagombea wao mbalimbali kwa ajili
ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu, tayari wameibuka wanasiasa
malaya ambao wamehama vyama vyao, siyo kwa sababu ya kukerwa na sera za vyama
hivyo, la hasa. Bali kwa sababu wanaamini wakienda kwenye vyama vingine
watapatiwa nafasi ya kugombea uongozi. Yale yale ya makahaba wa kweli!
Ukiwachunguza
wanasiasa wengi, kama siyo wote, ambao wamebadili itikadi zao katika kipindi
hiki, utakubaliana nami kwamba ama walikuwa hawana uhakika kama watapitishwa na
vyama vyao au wamepoteza mvuto wa kisiasa kwa wananchi waliokuwa wakiwaongoza
na sasa wanataka kutumia mwavuli wa nguvu za vyama ‘vipya’ kurejea tena
madarakani.
Wanapokimbilia
upande wa pili, wanasiasa hawa makahaba wamekuwa na tabia zile zile za kukashfu
kule walikotoka, wakijinasibu kwamba walikuwa wanapambana na hiki na kile
lakini hawakusikilizwa, sasa wanaona bora wajiondoe na kwenda upande mwingine
ambako ‘sera zao zinakubalika’.
Madhara ya
wanasiasa wa aina hii yameonekana mara nyingi sana hapa nchini. Wapo ambao huko
walikotoka walionekana kuwa na nguvu, wakapokelewa upande wa pili na kupewa
dhamana, lakini matokeo yake wengi walianguka vibaya na hata wale walioshinda
chaguzi mbalimbali, baadaye wakageuka shubiri kwa madai ya uasi. Tumewaona,
sina haja ya kuwataja hapa.
Ni kwa
mukhtadha huo – sina uwezo wa kuzuia, lakini nina uwezo wa kushauri – naona
kwamba vyama viwe makini na wanasiasa hawa, ambao nalazimika kuwaita ‘ni
makapi’, kwa sababu wanaweza wasiaminike kama wamefuata sera ama wanatafuta
ngazi ya kuendelea kupata neema ya uongozi.
Kuwakumbatia
wanasiasa wa aina hii, japokuwa ni haki yao ya kidemokrasia, ni kuhatarisha
upinzani wa kweli kwa sababu naamini siyo wote wenye mtazamo chanya wa mageuzi
bali wanatafuta maslahi binafsi. Kutoa siri za kule watokako kunamaanisha
kwamba hata wakija kuondoka huko walikokimbilia pia watazitoa siri hizo!
Upinzani
unaimarika nchini, tunapenda uwe na nguvu na ikibidi uongozi halmashauri na
kuwa na sauti kubwa Bungeni, lakini kama mtaji wa vyama vya upinzani utakuwa
kuchukua ‘makapi’, ambayo mengi ni ya CCM, uwezekano wa kutimiza ndoto hizo
utakuwa mdogo.
Hivi tu
niwaulize hao wanasiasa wanaoona muda mzuri wa kuondoka ni kipindi cha
uchaguzi, kwa nini, kama kweli wanataka mabadiliko, hawakuondoka kabla? Kwa
nini, kwa mfano wabunge wanaomaliza muda wao, hawakuondoka katikati kama
tulivyomshuhudia Zitto Kabwe?
Wangu ni
ushauri tu, utekelezaji ni kwa wahusika wenyewe.
Msemea
sikioni, siyo majinuni!
Wasaalam.
0656-331974
IMECHAPWA MARA YA KWANZA NA GAZETI LA WAJIBIKA JULAI 27, 2015
No comments:
Post a Comment