Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 26 July 2015

MAJANGA, BVR YASABABISHA KIFO DAR, MASHINE YAKUTWA NYUMBANI KWA MTU



NA BEATRICE SHAYO
Mtu mmoja mkazi wa Yombo Vituka jijini  Dar es Salaam, anadaiwa kuanguka na kufariki dunia kwenye foleni ya zoezi la uandikishwaji wa daftari la kudumu la wapiga, jijini Dar es Salaam.

 Marehemu huyo aliyetambuliwa kwa jina la Baba Abi, alidondoka wakati akisubiri kusajiliwa juzi saa 11 jioni kwenye daftari hilo linalotumia mashine za kielektroniki (BVR), akiwa kwenye msururu wa kituo cha Kwa Ali Mboa huko Yombo Vituka. 
 
Kwa mujibu wa mpangaji wa Baba Abi, Mwalami Dirunga marehemu alizikwa jana huko Chanika Kinyamwezi, baada ya kufariki alfajiri.
 
Dirunga alisema kuwa alipigiwa simu kujulishwa kuwa baba huyo ameanguka akiwa kwenye foleni saa 11 jioni na aliwahi kwenye tukio kumpeleka hospitali.
 
Wakati zoezi hilo likisababisha kifo, mapya yamezidi kuibuka baada ya mashinye moja kukutwa mafichoni nyumbani kwa mkazi wa Yombo aliyetajwa kwa jina moja la Baba Furaha.
 
Mashine hiyo ilikuwa imehifadhiwa nyumbani kwake kinyemela ambapo taarifa ilizopata NIPASHE ilikuwa ni mkakati wa kuandikisha wanachama wa CCM kwa siri nyakati za usiku.
 
Gazeti hili lilifika nyumbani kwa mtuhumiwa ambaye hata hivyo hakuwepo na kuthibitishiwa kuwa uandikishaji huo ulikuwa ukifanyika kwa wana-CCM wachache.
 
Hata hivyo, baada ya kutokea mgogoro, mashine hiyo iliondolewa na kupelekwa kituo cha uandikishaji  cha  Yombo kwa Kilakala.
 
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema), Edson Joel, akizungumzia tukio hilo, alisema aliiona mashine hiyo nyumbani kwa mhusika ikiandikisha wapiga kura.
 
Alisema kuhifadhiwa kwa mashine hiyo nyumbani kwa mtu binafsi ni kinyume cha taratibu na kwamba ulikuwa ni mpango ulioandaliwa wa kuandikisha vijana wa CCM.
 
Joel alisema waliungana na wenzao kupinga zoezi hilo kufanyika nyumbani kwa mtuhumiwa na kuhakikisha mashine hiyo inaondolewa na kupelekwa kwenye kituo cha usajili ilipopangiwa na baadaye ilirejeshwa ofisi ya serikali ya mtaa wa Kilakala.
 
Alisema kituo hicho kimeanzishwa kinyemela huko Mazegere kata ya Kilakala na kwamba hakipo katika orodha zilizotajwa hivyo waliingilia kati na kuiondoa.
 
Alisema hata kama nia ni njema ilitakiwa vyama vyote wakubaliane na sio CCM kujichukulia majukumu bila kushirikisha wadau.
 
“Inaonyesha dhahiri hawakuwa na nia njema ndiyo maana hawajatushirikisha lakini kwanini BVR ihamishiwe nyumbani kwa Baba Furaha ambako kuna vijana wanachama wa CCM… walitaka kuwaandikisha haraka haraka,” alikosoa. Joel alisema kutokana na tukio hilo, vijana hao wa CCM wamemtishia na tayari ameripoti kituo cha polisi Kilakala kulinda usalama wake.
 
Mtendaji wa Kata ya Kilakala, Peter Makoye, ambaye awali alikanusha kuhusu kuanzishwa kwa kituo hicho, baadaye alikiri kupelekwa kwa mashine hiyo kwa lengo la kuondoa msongamano katika kituo cha Shule ya Msingi ya Kilakala iliyopo Yombo. Alisema shuleni hapo kuna vituo vinne, hivyo waliamua kuihamisha BVR hiyo.
 
Katika kituo cha Shule ya Sekondari ya Barabara ya Mwinyi, kulitokea vurugu baada ya kudaiwa kuingizwa watu kupitia mlango wa nyuma bila kukaa kwenye foleni hali ambayo ilisababisha polisi kuitwa ili kutuliza vurugu.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Barabara ya Mwinyi, Waziri Enosi, alisema ilichotokea ni kuandaliwa kwa watu wao na kupatiwa kitambulisho bila kukaa foleni.
 
Alisema zoezi hilo ni haki ya kila mtu lakini matokeo yake wanashangazwa ni kwa nini siasa zinaingizwa na kusababisha ugumu kwa wengine.
 
 “Hili suala lipo huru lakini wanaingiza maslahi yao watu wapo kwenye foleni tangu saa 11 alfajiri lakini wanaandikishwa wengine ambao wanapitishiwa mlango wa nyuma ndiyo maana watu wamefanya vurugu,” alisema
Aidha baadhi ya wananchi waliopo vituoni walilalamikia watendaji wa mtaa kupewa rushwa huku wengine wakiandikiwa memo ili wasajiliwe haraka.
 
“Mimi nimeandikiwa hata wewe ukitoa hela utapata kitambulisho fasta nenda kamuone mtendaji,” alisema mmoja wa wananchi aliyekuwa kituoni hapo.
 
Katika kituo cha Kiembe Samaki B kilichopo Yombo Bakwata wananchi walilala kituoni bila kusajiliwa.
 
William Mabaranga aliyekesha kituoni ili kuwahi namba moja alizidiwa na wajanja waliotumia mbinu chafu kama vimemo na kupitia milango ya nyuma.
 
“Tangu usiku sasa sijui hao ambao wanaandikishwa namba zao zinatoka wapi wakati mimi ndiyo wa kwanza kinachofanyika ni ufisadi,” alisema. Alisema BVR zinaharibika kila wakati lakini wanashangaa wenzao wakiandikishwa.
 
Mwandikishaji Ally Uweso alisema wana kompyuta mbili lakini moja ndiyo inayofanya kazi kwani nyingine ina matatizo ya  kamera.
 
Ofisi ya serikali ya mtaa wa Kimbunga , ilikuwa na tatizo la kukosa mashine kwani ilikuwapo moja huku wakielemewa na idadi kubwa ya wananchi.
 
Kituo cha Tabata Shule walilalamikia kukaa kwa zaidi ya siku tatu bila kupata kitambulisho kutokana na mashine hiyo kudaiwa kuharibika kila wakati.
 
Wakati huo huo, uandikishaji wapiga kura umeingia siku ya nne lakini ndiyo kwanza vioja vimeeendelea kujitokeza vituoni, huku wananchi wakilalamikia utaratibu uliowekwa wa uandikishaji ambao wamedai umeangalia maslahi ya kichama zaidi.
 
Mkazi wa Mzimuni, Abubakar Ali , alisema Jumatano ya wiki hii alipewa namba sita ya kujiandikisha lakini hadi jana hajapata fursa hiyo huku wenye namba za juu yake wakiwa tayari.
 
“Kila siku nakuja hapa saa 11:00 alfajiri lakini ninapouliza kwa nini sipewi fursa naambiwa namba yangu haijafikiwa, hivi inawezekana vipi namba sita kwa muda wa siku tatu haijafika,” alisema.
 
Alilalamikia utaratibu unaendelea kituoni hapo na kueleza kuwa, kila siku umekuwa ukibadilishwa na kuwafanya wananchi kukata tamaa.
 
Bakari Kombo mkazi wa Kawe, alisema kuwa, uandikishaji kituoni hapo siyo mzuri na kusababisha kuwepo kwa vurugu baina ya wananchi na waandikishaji.
 
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ilitakiwa iwe na watu ambao wanawaongoza wananchi kwa utaratibu unaoeleweka, lakini sasa tunajikuta kila mmoja anagombania kwenda pale kujiandikisha kwa madai namba zao zimefika,” alisema.
 
Kutokana na kuwepo kwa utaratibu usioeleweka, NIPASHE Jumamosi ilishuhudia baadhi ya wananchi wakigombania zamu ya kujiandikisha huku vijana waliojitambulisha kwa gazeti hili kuwa ni wa kujitolea, wakiliambia gazeti hili kuwa, wameamua kuchukua nafasi ya NEC kusimamia kazi hiyo ili iende vizuri.
 
Charles Fabian mkazi wa Mzimuni, alisema kuwa yeye na wenzake baada ya kuona vurugu zinatokea kutokana na kila mtu kudai namba zao zimefika, waliamua kujitolea kuwaelekeza wananchi utaratibu mzuri wa kujiandikisha.
 
Pia alisema tatizo linaloendelea kujitokeza ni ubovu wa mashine za kusajili ambazo zinasababisha wananchi kuwa na hasira kutokana na kushinda kituoni muda mrefu bila kupata haki yao ya kujiandikisha.
 
Rose Maganga mkazi wa Kawe Mzimuni, alisema kuwa yupo kituoni hapo si kwa sababu anataka kitambulisho bali ili apate fursa ya kumchagua kiongozi amtakaye mara baada ya kukabidhiwa kitambulisho hicho.
 
“Tatizo lingine kwenye mashine hizi ni kitendo cha kuchukua dakika zaidi ya 20 kumwandikisha mtu mmoja, nafikiri serikali haikufanya utafiti kabla ya kuruhusu mfumo huu kuingia nchini, tunateseka bila hatia na tunajikuta tunatumia muda mrefu hapa na kuacha kufanya shughuli nyingine,” alisema.
 
Pia alisema tatizo lingine aliloliona kutoka afike kituoni hapo ni watu kupewa namba kinyemela huku wale waliopata kihalali wakikosa fursa ya kujiandikisha.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment