Kukaribishwa kwa Lowassa, ambaye miaka nane iliyopita alitajwa na Chadema kwamba ni fisadi namba saba katika orodha ya mafisadi wanaoitafuna nchi, kunamaanisha kwamba ikiwa ataridhia, basi atagombea urais kupitia umoja huo, hivyo kupambana na mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk. John Pombe Joseph Magufuli katika kinyang'anyiro hicho.
Kwa takriban wiki nzima, Ukawa wamekuwa wakiendesha vikao vya kumpata mgombea atakayesimama kwenye nafasi ya urais, huku jina la Lowassa likitajwa tangu Kamati Kuu ya CCM ilipomtema kwenye mchakato Julai 12, mwaka huu mjini Dodoma.
Ukawa walikuwa wamtangaze mgombea urais jana Jumapili mbele ya waandishi wa habari, lakini kwa sababu zisizofahamika, wakauahirisha mkutano huo ambao ulikuwa ufanyike kwenye Hoteli ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, leo hii umoja huo umeamua kuuvunja ukimya na kumkaribisha rasmi Laigwanan huku ikitafsiriwa kwamba yeye ndiye atakayepeperusha bendera ya Ukawa kwenye mbio za urais.
Muasisi wa Chadema, Edwin Mtei jana alikaririwa na gazeti la MWANANCHI akimkaribisha mwanasiasa huyo na makada wengine wa CCM kujiunga na chama hicho kikuu cha upinzani.
“Nimesikia Lowassa anatajwa kutaka kujiunga na Chadema, mimi namkaribisha aje, si yeye tu, aje na makada wengine wa CCM kwa kuwa tunapaswa kuimarisha nguvu za kuiondoa CCM madarakani,” alisema.
Akaongeza: “Tunawakaribisha Chadema makada wote wa CCM bila masharti na kama wana nia ya uongozi Chadema ina vikao vya kupitia kulingana na sifa zao na vikao vitakuwa na maamuzi ya mwisho.”
No comments:
Post a Comment