Edward Lowassa akionyesha kadi yake ya uanachama wa Chadema baada ya kujiunga na chama hicho juzi Jumanne Julai 28, 2015.
Anawaaga CCM? Hapana. Hapa ni wakati wa mikutano yake ya kutafuta wadhamini alipokuwa katikaharakati za kuomba kugombea urais kupitia chama hicho.
Lowassa na mkewe Regina wakionyesha kadi zao za uanachama wa Chadema.
Lowassa akiwa katika mkutano wa ndani wa Chadema Jumatatu Julai 27, 2015 huko Bahari Beach Hotel, siku ambayo Chadema ilitangaza rasmi kumkaribisha.
Lowassa akiwa pamoja na viongozi wa Ukawa Julai 28, 2015 kwenye Hoteli ya Bahari Beach siku aliyotangaza kujiunga rasmi na umoja huo kupitia Chadema.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aiteta jambo la Lowassa katika mkutano huo na waandishi wahabari.
Lowassa akiteta jambo na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba.
Lowassa akifafanua mambo mbalimbali baada ya kukabidhiwa kadi ya uanachama wa Chadema.
Lowassa akikumbatiana na Profesa Lipumba.
Wafuasi wa Chadema wakiwa na bango.
Na Daniel Mbega
KUNA
wahubiri wengine na watoa mawaidha huwa wanajisahau. Wanatumia muda mwingi
kueleza mambo mengi kwa wakati mmoja na kuwafanya watu wasahau yaliyotangulia kusemwa.
Kwa vile siyo busara kuondoka ibadani wakati wa mahubiri, wengine huamua kuketi
lakini mawazo yao yakiwa mbali.
Sasa
sikiliza kisa hiki cha mhubiri aliyetumia muda mwingi kuzungumza mambo mengi
kiasi cha kumchanganya mmoja wa waumini wake. Alipomaliza akawauliza waumini
ambao walikuwa kimya wakati akihubiri:
"Nani
anataka kwenda Mbinguni?" Watu wengi wakanyoosha mikono huku wakipiga
vigelegele "AMEN!".
Akauliza
tena: "Nani anataka kwenda motoni?" hakuna aliyenyoosha mkono.
Lakini
kulikuwa na muumini huyu mmoja ambaye muda wote wa mahubiri alikuwa ametulia
tuli 'akisikiliza' kwa makini. Ajabu ni kwamba, hakunyoosha mkono mahali popote
katika maswali yale mawili yaliyoulizwa.
Mhubiri
akamsogelea akiwa na kipaza sauti akitaka kujua kama huyo bwana amemwelewa ama
alikuwa na mawazo gani.
Akamuuliza:
"Mpendwa, hukunyoosha mkono kati ya wanaotaka kwenda Mbinguni, wala
hukunyoosha mkono kati ya wanaotaka kwenda motoni. Sasa wewe unataka kwenda
wapi?"
Muumini
akajibu, “Nataka kwenda nyumbani, Eboh!”
Naam. Kwa
muda sasa siasa za Tanzania zimekubikwa na agenda moja tu hasa tunapoelekea
kwenye uchaguzi mkuu.
Mjadala mkubwa
kwenye mitandao ya kijamii kama twitter,
whatsapp, facebook au telegram ni
kuhusu kuondoka kwa kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Edward Lowassa na
kujiunga na Chadema, hivyo kuwa na nafasi ya kugombea urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Magazeti
ndiyo usiseme, kwani yameigeuza agenda hiyo mtaji wa biashara tangu
alipoenguliwa na chama chake kule Dodoma wakati wa kuwania uteuzi wa kugombea
urais.
Vyama vya
siasa vya upinzani vilimsubiri muda mrefu ili ‘vimkabidhi mikoba’ ya kuwania
urais kwa matumaini kwamba lazima vitashinda vikimsimamisha.
Hoja
zilizo nyuma ya mijadala mbalimbali ni kwamba, mwanasiasa huyo anakubalika kila
kona ya nchi, watu wa rika zote wanamkubali na wengi waliamini kwamba ndiye
angekuwa rais wa awamu ya tano.
Kuishi kwa
matumaini ni jambo jema, na kuziishi ndoto zako ni vyema pia, lakini wakati
mwingine ni vyema kukubaliana na uhalisia, vinginevyo zitakuwa ni ndoto za
Alinacha kuoa binti wa Sultan huku akipiga teke kapu lake la urembo!
Umati
mkubwa ambao Lowassa alikuwa akiukusanya tangu Mei 30, 2015 alipotangaza nia ya
kuwania urais pale Arusha, na umati ambao ulikuwa ukijitokeza kila mahali
alikokwenda kukusanya saini za wadhamini umewatia kiburi wananchi wengi kwamba
kumbe anaweza kushinda hata kama atasimama upande mwingine.
Kila mmoja
ana mtazamo wake, siwezi kupingana naye na sitegemei kama kuna mtu atapingana
na mtazamo wangu, kwa sababu ni wangu na hauwezi kuwa wa mwingine!
Ninaamini
kwamba Watanzania wengi walikuwa wanapenda Lowassa ateuliwe na CCM siyo kwa
sababu ya busara na uwezo wake wa uongozi, bali walitaka kuleta mabadiliko kwa
kumpata walau kiongozi dikteta kidogo ili awashikishe adabu wale wote ambao
‘wamezowea kazi’ na kuendelea na fungate hata pale shela linapohitaji kufuliwa.
Lowassa,
kama binadamu mwingine yeyote, ana uwezo na udhaifu wake. Katika uwezo, wengi
wanamkubali kwa sababu anaweza kuchukua maamuzi magumu hata kama yataigharimu
serikali. Lakini udhaifu wake ni katika kashfa ambazo anahusishwa za uporaji wa
mabilioni ya shilingi za walipa kodi hata kama hakuhusika moja kwa moja.
Pengine
hiyo ya pili ya udhaifu wake, ikiwa ni pamoja na kujilimbikiza mali nyingi
zisizo na maelezo, ndiyo iliyosababisha Kamati Kuu ya CCM ikamwengua mapema,
hatujui!
Ninachopenda
kumshauri Lowassa, kwa nia njema tu kabisa, ni kutulia badala ya kuendelea kuwa
na ndoto za urais, kwa sababu naamini wapo waliomshauri usiku na mchana aende
upinzani akagombee kwa vile katika umri wa miaka 62, hawezi kusubiri miaka
mingine 10 ndipo ateuliwe na CCM.
Kwa yale
machache ambayo aliyafanya na kumwezesha ‘kupendwa’ na wengi kiasi cha mikutano
yake ya kutafuta wadhamini kufurika, yanatosha na angeweza ama kuendelea na
mbio za ubunge ama kutulia na kuachana na presha hizi zisizo na kikomo.
Kwa hali
ilivyo sasa, nakumbusha tu kwamba, yawezekana hata umati ule mkubwa uliokuwa
ukimfuata kila kona haupo tena na kuna uwezekano mkubwa umati huo ulikuwepo
kutokana na uzito wa pochi! Si wanasema silaha pesa, kisu mzigo bwana?
Kama Mzee
Lowassa anadhani wale waliokuwa wanamfuatilia kila mahali ni dalili ya yeye
kushinda, nachelea kusema kwamba anajidanganya. Wengi waliletwa na njaa zao. Si
tumeelezwa kwamba hata waendesha boda boda nao walikuwa wakijaziwa mafuta ili
kupamba misafara hiyo!?
Ukweli
kwamba siyo kila anayekupigia makofi anakushangilia, ndio ujumbe wangu kwa Mzee
Lowassa. Kumbuka tu hata kisa cha mtoto wa mbu, ambaye kila alikopita alisikia
makofi Pwaa! Pwaa! Aliporudi kwa mamaye akamwambia: “Mama, aisee binadamu wananipenda kweli, kila ninakopita wananishangilia
kwa kunipigia makofi!” Mamaye akamwambia: “Mwanangu jihadhari. Una bahati umenusurika, makofi hayo siyo ya kheri,
wanataka kukuua lakini wamekukosa!”
Wengi
walipiga vigelegele kwa nguvu ili usije ukawasahau katika ufalme wako, au
wengine walishangilia kwa sauti ili hata posho yao iongezeke.
Hata huko
alikokwenda, ni vyema akawa makini zaidi na kuchukua tahadhari, maana jambo
lililo wazi ni kwamba, hao hao waliomwita fisadi, leo hii ndio wanaompigia
nderemo na vifijo, wakiimba nyimbo na mapambio kwamba anafaa.
Ninachokiona
ni kwamba, hao jamaa wanatambua uchu wa madaraka ya urais alionao Lowassa licha
ya kashfa za ufisadi, lakini wenyewe pia wana uchu wa kuongoza Dolan a kuing’oa
CCM madarakani, hivyo wanaona njia rahisi ni kumtumia Lowassa ambaye ‘ana mtaji
wa wafuasi ndani na nje ya CCM’ ili waweze kutimiza ndoto zao.
Hao jamaa,
ikiwa Lowassa ‘atawasaidia’ kuing’oa CCM, baadaye watamtosa kwa kisingizio
kwamba ni mzee na pia mgonjwa!
Kuthubutu
kwenda upinzani kwa dhamira ya kuingia Magogoni kuna mawili – ukibahatika
unaweza ukalamba turufu, lakini ukikosa na kulamba galasa itakuwa mbaya zaidi
hata kwa heshima uliyojijengea.
Wakati
mwingine historia inasaidia. Tulimshuhudia Augustine Mrema mwaka 1995
alipokwenda upinzani baada ya kutimuliwa CCM. Kila kona ilikuwa Mrema! Mrema!
Na yote hiyo ilitokana na juhudi zake alizozifanya akiwa Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi pamoja na kushikilia cheo cha ajabu cha Naibu Waziri Mkuu,
ambacho kilianzishwa na kufutwa katika awamu ya pili.
Huyo bwana
alipamba vichwa vya habari vya magazeti, ambayo wakati huo yalikuwa
yanahesabika kama vidole vya mkono, gari lake likasukumwa bila hata kuwashwa
kwa mwendo mrefu, lakini mwisho wa siku akaangukia pua.
Mzee
Lowassa mshahara bado unao, ulinzi bado unao kwa cheo chako cha uwaziri mkuu.
Bado Mungu amekujaalia amali nyingi ambazo hata utakula kila siku sidhani kama
zitamalizika leo au kesho, kwa nini urais iwe dili kubwa? Kuna nini Ikulu kiasi
cha watu kukushawishi uvae jezi za timu pinzani?
Tafadhali
usiniulize ninataka kwenda wapi, kwa sababu nitakwambia tu “Nataka kwenda
nyumbani!”
Alamsiki.
0656-331974
No comments:
Post a Comment