Fike Mapugilo wakati anaingia kwenye masumbwi ya kulipwa mwaka 1991
NA DANIEL MBEGA
WENGI
wanamfahamu kama Fike Wilson, lakini wakati anapanda ulingoni kwa mara ya
kwanza kucheza ndondi za kulipwa kwa mara ya kwanza Jumanne Machi 19, 1991
dhidi ya Keith Mwila jijini Dar es Salaam wengi walimfahamu kwa jina la Fike
Mapugilo. Hakuwa akilitumia zaidi jina la katikati la ‘Wilson’.
Lakini jina
la Mapugilo ‘lilipotea’ mwaka 1997 alipoanza mashindano ya ‘Mr Tanzania’ na yeye
akatwaa taji hilo jijini Dar es Salaam.
Fike mwenye bukta nyeusi mbele wakati akishiriki mashindano ya Mr Tanzania mwaka 1997.
Huyu alikuwa
miongoni mwa mabondia wengi kutoka Kinondoni waliotamba enzi hizo na ambao
walishindwa kuendelea na mchezo huo kutokana na ‘siasa’ zilizoingia baadaye
pamoja na ukosefu wa udhamini kwenye masumbwi hayo ya kulipwa.
Unaweza kusema
alicheza ndondi kwa miaka 15, lakini kwa hakika hakuwa akicheza mfululizo
katika kipindi chote hicho, kwani rekodi zilizopo zinaonyesha kwamba alicheza
mapambano 19 tu ya kulipwa akishinda 12 (8 kwa KO), akapoteza matano (matatu
kwa KO) na kutoka sare mawili. Alicheza jumla ya raundi 104 na ushindi wake wa KO
ni asilimia 42.11.
Fike
Wilson mwenye urefu wa futi 5 na inchi 11½ (182 sentimeta), alizaliwa Oktoba
22, 1975 Mbeya na ndiyo maana mapambano yake mengi ya awali aliyechezea huko
kwao.
Pambano lake
la kwanza lilikuwa dhidi ya Keith Mwila kama nilivyoeleza hapo juu ambalo
lilikuwa la raundi 6 na alishinda kwa pointi jijini Dar es Salaam.
Alipanda ulingoni
mara ya pili Juni 15, 1991 kuzichapa na Salum Yazidu, pambano ambalo
lilifanyika mjini Mbeya na akashinda kwa pointi katika raundi 8. Agosti 12,
1991 akapanda tena ulingoni mjini Mbeya kuzipiga na Sunny Mwakasala katika
pambano la raundi sita na kushinda kwa pointi kabla ya kumtwanga kwa pointi
Salum Yazidu kwa mara nyingi katika raundi sita Oktoba 18 mwaka huo huo mjini
Kyela.
Pambano lake
la kwanza dhidi ya bondia kutoka nje ya Tanzania lilifanyika mjini Mbeya
Februari 18, 1992 dhidi ya Ngabo Foreman wa Zaire, ambapo alishinda kwa KO ya
raundi ya 3 tu. Mwezi mmoja baadaye, yaani Machi 19, 1992 alipanda ulingoni
kuzichapa na Abraham Mwitupa huko huko Mbeya na kwa mara nyingine akashinda kwa
KO ya raundi ya 3. Oktoba 20, 1992 alimchapa kwa KO ya raundi ya 5 William
Schula kwenye pambano lililofanyika Kyela.
Mei 12, 1993
alionja kipigo cha kwanza kutoka kwa bondia hatari wa Zambia enzi hizo, Charles
Libondo ‘Mawe’ baada ya kupoteza pambano hilo la raundi 8 kwa pointi huko
Mbeya.
Kwa hasira
tu, alipopanda ulingoni Oktoba 25, 1993 alimchakaza kwa KO ya raundi ya 9 mpinzani
wake Mnatija kwenye pambano lililokuwa la raundi 10. Baada ya hapo akapotea
kwenye ulimwengu wa masumbwi na ndipo alipojikita katika mazoezi ya viungo,
hasa ya utunishaji wa misuli, akiwa amefungua gym yake huko Mwananyamala na
hatimaye kuanzisha mashindano ya utunishaji wa misuli, maarufu kama ‘Mr
Tanzania’.
Miaka sita
na nusu ikapita, hatimaye Fenruari 5, 2000 akarejea ulingoni kuzichapa na
bondia Masoud Kambenga ambaye ndiyo kwanza alikuwa anaingia kwenye ndondi za
kulipwa siku hiyo. Mapugilo alipoteza pambano hilo lililofanyika Dar es Salaam kwa
KO ya raundi ya 3 tu.
Mei 12, 2000
akapanda ulingoni kutwangana na Meddie Serunjogi katika pambano la raundi 10
pale Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, lakini Mapugilo alishinda kwa KO ya
raundi ya 3 na kuurejesha moto wake enzi zake katika uzani wa middle.
Akiwa ameiva
kweli kimazoezi, Agosti 16, 2000 Mapugilo akamwaibisha bondia B Mwakasanga
aliyeingia ngumi za kulipwa siku hiyo kwa kumtwanga kwa KO ya raundi ya 1 tu.
Hatimaye Novemba
5, 2000 akapanda ulingoni kuwania ubingwa wa taifa wa uzito wa middle
unaotambuliwa na shirikisho la ndondi la TPBC akipambana na bondia mkongwe Said
Yazidu, ambapo alishinda kwa pointi katika raundi 10 na kunyakua taji hilo.
Wakati
sasa akiwa na miaka 26, mnamo Juni 11, 2001 Mapugilo alipambana na Abdallah
Nyuki mjini Dar es Salaam katika pambano lisilo la ubingwa la raundi 10 na
akashinda kwa KO ya raundi ya 8
Pambano lake
la kwanza nje ya Tanzania lilifanyika Septemba 21, 2001 kwenye ukumbi wa Blue
Horizon jijini Philadelphia, Pennsylvania, Marekani dhidi ya Ronald Boddie
likiwa na raundi 4, ambapo Mapugilo alipigwa kwa KO katika dakika ya 1:39 ya
raundi ya 3, mwamuzi akiwa Eddie Cotton.
Akarejea
Dar es Salaam kwa hasira na kumtwanga kwa TKO Abdallah Nyuki katika raundi ya 8
kwenye pambano la raundi 10.
Akiwa anataka
kujaribu bahati yake, Mapugilo alikwenda tena Marekani na Januari 12, 2002
alipanda ulingoni kwenye ukumbi wa Cox Pavilion jijini Las Vegas, Nevada kuzitwanga
na Jeff Lacy katika pambano la raundi 6. Hata hivyo, akapoteza pambano hilo kwa
TKO katika sekunde ya 50 ya raundi ya kwanza mbele ya mwamuzi Tony Weeks na
majaji Robert Hoyle, Jerry Roth na Paul Smith.
Desemba 14,
2002 alipambana na Said Yazidu kuwania taji la taifa la uzani wa middle ambapo
katika pambano hilo la raundi 10 lililofanyika kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo
jijini Dar es Salaam aliweza kushinda kwa pointi.
Pambano
lake la mwisho kabisa kabla hajatundika glavu lilifanyika wakati wa Mwaka Mpya
2006 dhidi ya bondia Pascal Ndomba kwenye ukumbi wa New Vijana Social Hall, Dar
es Salaam, likiwa la ubingwa wa super middle linalotambuliwa na TPBC, lakini
mabondia hao walitoka sare.
Amewahi kuishi
jijini Philadelphia, Pennsylvania, Marekani kwa miaka kadhaa kabla ya kurejea
nchini, ambapo ameweza kuendelea kituo cha kuwafundisha vijana masumbwi na
ukakamavu kiitwacho Fike Fitness Gym kilichoko Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Fike Wilson Mapugilo alivyo hivi sasa
Hii ndiyo filamu ya Jamal
Mbali ya
hayo, hivi sasa amejiingiza kwenye uigizaji wa filamu ambao filamu yake ya
kwanza iliyotoka mwaka 2010 iliitwa ‘The Power of God’ na mwaka 2014 akaibuka
na filamu nyingine iitwayo ‘Jamal’ ambayo ameshirikiana na mbabe mwingine Jimmy
Mponda ‘Jay Plus’ na wasanii wengine kama Chrispin Kisinni, Ahmed Ulotu na
wengineo.




No comments:
Post a Comment