Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday 13 February 2016

YANGA NA WAKONGWE WENGINE 13 WAANZIA MTOANO

Wachezaji wa Yanga wakishangilia

Na Daniel Mbega

MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga, leo hii wanaanza kampeni yao kuwania taji la ubingwa wa Afrika kwa kucheza ugenini na Cercle de Joachim ya Mauritius, lakini ikiwa ni miongoni mwa klabu kongwe 14 barani Afrika ambazo zinaanzia raundi ya mtoano.
Klabu nyingine kongwe zinazoanzia kwenye hatua hiyo ya mtoano kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ni mabingwa mara mbili wa Afrika, Enyimba FC ya Nigeria, Mangasport ya Gabon, Ferroviario de Maputo ya Msumbiji, Gor Mahia ya Kenya, AS Vita Club ya Jamuri ya Kidemokrasia ya Congo, AS Douanes ya Senegal, Horoya A.C ya Guinea, Stade Malien ya Mali, Club Africain ya Tunisia, Wydad Casabanca ya Morocco, Asec Mimosas ya Ivory Coast, St. George ya Ethiopia na US Douala ya Camroon.

Kama zilivyo timu nyingine, Yanga – ingawa haijawahi kutwaa ubingwa wowote wa Afrika – lakini ni moja ya timu kongwe barani Afrika ikiwa inawania ubingwa wa Afrika kwa mwaka wa 20 sasa tangu ilipoanza kushiriki mashindano hayo mwaka 1969 na kufika robo fainali kabla ya kutolewa kwa shilingi na Asante Kotoko ya Ghana, ambayo pia iliitoa katika hatua kama hiyo mwaka 1970, safari hiyo kwa kucheza ugenini Ethiopia baada ya mechi za Kumasi na Dar es Salaam kushindwa kutoa mshindi.
Yanga watacheza na wenyeji wao katika Kisiwa kidogo cha Curepipe, mchezo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani licha ya rekodi kuonyesha kwamba timu za Mauritius zimekuwa hazitambi mbele ya Yanga.
Lakini mabingwa hao wa Mauritius siyo wa kuwabeza, kwani wametwaa ubingwa wa nchi hiyo mara mbili mfululizo kwa mwaka 2014 na 2015 na ndiyo timu inayoongoza kwa kuwa na mashabiki wengi nchini humo ikisifika kwa soka safi huku ikiwa inamiliki uwanja wake wenye uwezo wa kuingiza watazamaji 6,200 walioketi.
Waamuzi katika mechi kati ya Cercle de Joachim na Yanga watakuwa Hubert Marie Bruno Andriamihasisoa wa Madagascar atakayesimama katikati akiasaidiwa na Randrianarivelo Ravonirina Harizo na Augustin Gabriel Herinirina wote kutoka Madagascar.
Mabingwa wa Zanzibar, Mafunzo F.C, wanawakabili wakongwe wa soka Afrika ya Kati japo hawajawahi kutwaa ubingwa, AS Vita Club ya Congo DR, mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Amaan na utachezeshwa na Warundi Eric Gasinzigwa, Hervé Kakunze na Pascal Ndimunzigo.
Enyimba jana walikaribishwa na Vipers SC (Bunamwaya) kwenye Uwanja wa Nakivubo, Kampala huku wenyeji wakimkosa mshambuliaji wao hatari Farouk Miya ambaye ametua kwenye klabu ya Standard Liege ya Ubelgiji kwa kitita cha Dola 400,000 mara tu baada ya mashindano ya Ubingwa wa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) kumalizika nchini Rwanda.
Vipers wanafundishwa na kocha wa zamani wa Kampala City Council Authority (KCCA), George Nsimbe na wanataka kuvuka raundi ya mtoano kwa mara ya pili tangu walipofanikiwa kufanya hivyo mwaka 1972.
Gor Mahia FC wao wanawakaribisha CNaPS Sport ya Madagascar, mchezo ambao utachezeshwa na waamuzi kutoka Tanzania wakiongozwa na Mfaume Ali Nassoro atakayesimama katikati akisaidiwa na Ferdinand Chacha na John Longino Kanyenye.
Mangasport inawakaribisha wakongwe wengine, Etoile du Congo kutoka Congo-Brazzaville kwenye Uwanja wa Henri Sylvoz jijini Libreville wakati Ferroviario de Maputo wamepita baada ya wapinzani wao Mochudi Center Chiefs ya Botswana kujitoa.
AS Douanes na Horoya A.C zitakabiliana kwenye Uwanja wa Mbour – Caroline Faye mjini Mbour wakati Stade Malien ikipepetana na Racing Club de Bobo ya Burkina Faso.
Kesho Jumapili, Club Africain itaikaribisha AS Tanda ya Ivory Coast, As Cotontchad SN ya Chad itaikabili Asec Mimosas ya Ivory Coast pia, Mbabane Swallows ya Swaziland itakuwa mwenyeji wa APR ya Rwanda, Lioli ya Lesotho itakuwa mwenyeji wa Vital’O ya Burundi, St. Michel ya Shelisheli itakuwa ugenini Addis Ababa kucheza na St. George, Wari Wolves ya Nigeria itaikaribisha CS Praia Cruz ya Cape Verde, US Douala watakuwa ugenini kwa Nimba United FC nchini Liberia na Wydad Casablanca watawakaribisha AS Douanes ya Niger.
Kwa upande wa Kombe la Shirikisho, wawakilishi wa Tanzania, Azam FC wataanzia kwenye raundi ya kwanza ambapo watacheza na Bidvest Wits ya Afrika Kusini.
Lakini katika kombe hilo pia kuna timu kongwe zinazoanzia raundi ya awali ambazo ni Africa Sports ya Ivory Coast iliyotwaa Kombe la Washindi Afrika mara mbili na kunyakua ubingwa wa nchi hiyo mara 17, Sports Club Villa ya Uganda, Al Ittihad ya Libya.
Al Ittihad ya Tripoli imeshiriki kwenye mashindano mbalimbali ya Afrika tangu mwaka 1967, ikirudia nusu fainali ya Kombe la Shirikisho mwaka 2010.
Al Ittihad imecheza mechi yake ya nyumbani jana Ijumaa dhidi ya Sonidep ya Niger nchini Tunisia kutokana na vita vinavyoendelea Libya, lakini mabingwa mara mbili wa Afrika, Esperance ya Tunisia na FUS Rabat ya Morocco wamepita raundi ya kwanza ambayo itaanza Machi.
JKU ya Zanzibar na Mouloudia d’Oran ya Algeria zimepita hadi raundi ya kwanza baada ya wapinzani wao Gaborone United ya Botswana na Wallidan ya Gambia kujitoa.
Ajax Cape Town ya Afrika Kusini ilisitisha uamuzi wake wa kujitoa kucheza dhidi ya Sagrada Esperanca ya Angola baada ya Chama cha Soka Afrika Kusini (SAFA) kuichimba mkwara timu hiyo kwamba ingeifungia endapo ingejitoa.
Timu mbili za Congo, Diables Noire na V Mokanda, zote ziko nyumbani wikiendi hii kucheza na Africa Sports ya Ivory Coast na mabingwa watetezi Awka United.
Wakongwe wengine wenye kibarua kigumu wikiendi hii ni Kawkab Marrakesh ya Morocco itakayocheza na USFA ya Burundi, Saint Eloi Lupopo ya DR Congo itacheza na Bandari ya Kenya na El Khartoum ya Sudan itapepetana na SC Villa ya Uganda.
Mechi zote za marudiano zitafanyika kati ya Februari 26-28 wakati raundi ya kwanza itaanza kati ya Machi 11-13, 2016.

CREDIT: FIKRA PEVU




No comments:

Post a Comment