Msanii
mshindi wa shindano la Airtel Trace Music Star Mayunga Malini (Kulia) akiongea
na wadau wa Sanaa (hawako pichani) mapema wiki hii kwenye programu ya Jukwaa la
Sanaa ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA). Wengine katika picha ni Afisa
Habari wa BASATA, Aristides Kwizela (Katikati) na Afisa Sanaa wa Baraza hilo
Augustino Makame.
Msanii
Mayunga Malimi akiimba wimbo wake wa Nice Couple sambamba na mkongwe wa muziki
wa dansi nchini Kassim Mapili kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa la Baraza la
Sanaa la Taifa mapema wiki hii.
Msanii
mkongwe wa Sanaa za Maonesho Nkwama Ballanga akimpongeza Msanii Mayunga kwa
juhudi zake na kujituma katika kazi anazofanya. Wadau wengi wa Sanaa
waliohudhuria kwenye programu ya Jukwaa wiki hii walifurahishwa na juhudi
binafsi za Msanii Mayunga.
Sehemu
ya wadau wa Sanaa waliohudhuria programu ya Jukwaa la Sanaa wakimfuatilia kwa
makini Msanii Mayunga.
Na
Mwandishi Wetu
Wasanii nchini wametakiwa
kujituma na kutengeneza kazi za Sanaa zenye ubora na kuachana na dhana ya
kutegemea rushwa na hongo katika kuyafikia mafanikio yao kisanaa.
Wito huo umetolewa mapema
wiki hii na wadau wa Sanaa kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa ambayo huandaliwa
na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na kufanyika kwa mwezi mara mbili siku ya
Jumatatu kwenye ukumbi wa Baraza hilo.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti wadau hao walisema kwamba kumekuwa na wimbi la wasanii na mameneja wa
wasanii kutegemea rushwa za fedha na wengine kufikia hatua kutoa rushwa za
ngono ili kufanikiwa kisanaa hasa katika kuvishawishi vituo vya radio na
televisheni kucheza nyimbo zao.
“Ukweli ni kuwa rushwa na
hongo zinaendekezwa na wasanii walioshindwa. Msanii anayejitambua hawezi kutoa
rushwa ili wimbo wake uchezwe. Lazima wasanii waachane na dhana hii potofu,
waelewe kwamba kazi ya Sanaa iliyo bora itapendwa tu na kukubalika na jamii”
alisema Nkwama Bhallanga ambaye ni Msanii wa Sanaa za Maonesho.
Kwa upande wake Katibu wa
chama cha wachezesha disko (TDMA) Asanterrabi Mtaki alisema kuwa dhana kwamba
wasanii lazima wahonge watangazaji au ma DJs ili nyimbo zao zichezwe ni potofu
na ni chanzo cha kutangaza muziki au kazi za Sanaa zisizo bora na kuziacha zile
zenye ubora.
“Kama wimbo wako ni mzuri
kwa nini uhonge au utoe rushwa ili uchezwe? Hapa ndipo tatizo la kuendekeza
kazi mbovu za Sanaa linapoanzia. Muziki wa wenye fedha na wanaohonga ndiyo
unasikika, ule mzuri unaondaliwa na wasanii wasiyo na uwezo haupati nafasi”
alisema Mtaki.
Alitoa wito kwa wasanii kufikiria
njia mbadala za kutangaza nyimbo zao hasa kumbi za disko badala ya kutegemea
vituo vya radio pekee.
Awali akizungumza kwenye
Jukwaa la Sanaa, Msanii na mshindi wa shindano la Airtel Trace Music Star
Mayunga Malini alisema kuwa wasanii hawana budi kujituma, kutafuta fursa na
kuzitumia ipasavyo hasa kwa kutumia muda mwingi kubuni kazi zenye ubora.
Aliongeza kuwa, wasanii
hawana budi kuachana na dhana ya utegemezi na kutegemea fedha na hongo katika
kupata mafanikio kwani kazi za Sanaa zikitengenezwa kwa ubora na kwa kuzingatia
vigezo vyote zitapendwa na kutuzwa tu.
No comments:
Post a Comment