Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Wednesday 10 February 2016

WAPINZANI WANA VISA KAMA NDUGU WA MUME!

Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Na Daniel Mbega

GUBU la mawifi na kejeli ni mambo ya kawaida yanayompata mwanamke kutoka kwa ndugu wa mumewe na jamii yetu kamwe haiwezi kuyakanusha.
Tumeshuhudia mara nyingi ndani ya jamii pindi ndugu wa kiume anapoamua kuoa, hasa mwanamke anapokuwa siyo chaguo la wanandugu – wazazi ama dada zake – kwamba mkamwana huyo hupata shida sana kuelewana na ndugu wa mumewe.
Kama hakuambiwa mvivu, basi ataambiwa mchoyo; na kama hakuambiwa ana maringo, ndugu wa mume watamtoa kasoro yoyote kwamba ama ni mbaya, havutii na kadhalika, ilimradi tu hawakosi cha kuongea.
Wanawake wengi wanapoolewa hujiandaa kwa mazingira hayo, wakati mwingine hata waume zao huwatahadharisha kuhusu tabia za ndugu zao.
Hata hivyo, maandalizi hayo huwa hayasaidii kwa sababu kila siku ndugu wanaibuka na mazengwe mapya, hawakosi cha kuongea na ukarimu wa mke huwa si kitu kwao.
Kinachofanywa na wabunge wa upinzani – ambacho kimekuwa kikifanywa kwa muda mrefu sasa – hakina tofauti na visa vya ndugu wa mume kwa mke wa ndugu yao.
Huko nyuma hasa katika Bunge la 10 (maana ndipo mchezo huo ulipoanza) tulishuhudia jinsi wawakilishi hao wa wananchi waliopewa dhamana kubwa ya kuwakilisha changamoto za jamii husika walivyoanza na mchezo wa ‘kususa’ vikao kila walipozidiwa kwa hoja. Wakazusha visa kama vya mwana wa kufikia kususa chakula kila mara kinapowekwa mezani mpaka ‘baba arudi’ hata kama hakuna sababu.
Lakini kila waliposusia vikao, kamwe hawakususa kwenda benki kuangalia kama mishahara yao imeingia ama la! Walikomba kama kawaida huku akiendelea kukaa nje ya Bunge na kuwanyima haki waajiri wao ambao ni wananchi.
Tunafahamu wapinzani kazi yao kubwa ni kuisimamia serikali itekeleze majukumu yake ipasavyo, lakini kususa kwao wala hakukuweza kuizuia serikali isiendelee na majukumu yake – Bunge kwa maana hiyo likawa linaendelea na vikao kama kawaida ilimradi tu akidi inatimia.
Wanasiasa wetu wa upinzani wamekuwa na tabia mbaya ya ‘kujipiga wenyewe na kulia’ halafu wanatoka nje wakitaka wahurumiwe na wananchi, wakati hakuna sababu yoyote kwao kumwaga machozi.
Wengi tulidhani tabia ile imeachwa hasa baada ya serikali ya sasa chini ya Dk. John Magufuli kutekeleza kwa vitendo majukumu yake huku ikiwabana na kuwawajibisha watendaji wazembe na kunyoosha mambo ambayo yamekuwa hayaendi sawa kwa muda mrefu.
Kama walivyo ndugu wa mume wasiokosa sababu, wapinzani hao walianza kwa kubeza, kukejeli na kupinga uamuzi mbalimbali wa serikali tena katika mambo ambayo ni ya msingi kabisa ambayo hata wenyewe walikuwa wakiyanadi kwa wananchi kwamba wangeyatekeleza wakiingia madarakani.
Sasa kabla ya Mkutano wa Pili wa Bunge la 11 haujaanza mjini Dodoma wiki hii, tumeshuhudia walivyozua sababu nyingine na kususia uchaguzi wa wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa maelezo kwamba nao walitaka washirikishwe kwenye uteuzi wa wajumbe wa kamati hizo.
Kambi ya upinzani ikalalama kwamba Chama cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa kinawapangia watu wa kuongoza kamati zinazosimamia mapato ya serikali ambazo kikanuni zipo chini ya wapinzani wenyewe hasa Kamati ya Hesabu za Serikali za (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
“Tumegundua kwamba orodha ya majina yaliyotoka yana matatizo mengi na matatizo hayapo kwenye kamati ya PAC na LAAC tu, kwenye kamati nyingi kuna matatizo kwa hiyo kwa sasa viongozi wa kambi wanakutana kujadili na kuchambua taarifa iliyotolewa baadaye tutakutana na wabunge wote kisha kesho tutatoa msimamo wetu,” alisema Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Mnyika Januari 21, 2016.
Kwa maana nyingine, licha ya kamati hizo mbili kuundwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo wa upinzani, lakini bado wapinzani hawataki kwa madai kwamba wajumbe hao – ingawa ni miongoni mwao wenyewe – ni ‘chaguo la CCM’.
Hili linatia mashaka na kuzusha maswali mengi, kwa sababu wajumbe wa kamati hizo, ambao kwa mujibu wa kanuni miongoni mwao ndimo wanamotoka wenyeviti, ni wabunge wa upinzani, sasa kama leo hii hawawaamini kuingia kwenye kamati hizo, tuhoji basi ni kwanini hata wakawateua kuwania ubunge kupitia vyama vyao kama walikuwa hawastahili?
Kanuni za Kudumu za  Bunge Toleo la Aprili 2013, inasema: “Wenyeviti wa Kamati za Bunge zinazosimamia matumizi ya fedha za Umma ambazo ni Kamati ya Hesabu za Serikali, Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, watachaguliwa kutoka miongoni mwa wajumbe wa kamati hizo ambao wanatoka katika Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.”
Wapinzani ambao wamo katika Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) yenye wajumbe 23 ni Mbunge waSame Mashariki, Naghejwa Kaboyoka (Chadema), Mbunge wa Viti Maalumu, Rais Abdallah Mussa (CUF), Mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbarouk (CUF), Mbunge wa Viti Maalumu, Yosefa Komba (Chadema), Mbunge wa Viti Maalumu, Tunza Issa Malapo (Chadema) na Mbunge wa Mwanakwerekwe, Ali Salim Khamis (CUF).
Kwenye Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) yenye wajumbe 22, wapinzani ni Mbunge wa Mgogoni, Dk. Suleiman Ally Yusuf (CUF), Mbunge wa Viti Maalumu, Rose Kamili (Chadema), Mbunge wa Viti Maalumu, Conchesta Rwamlaza (Chadema), Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Vedasto Ngombale (CUF), Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Kiwelu (Chadema) na Mbunge wa Ukerewe, Joseph Mkundi (Chadema).
Kwangu mimi naamini kwamba, wabunge hawa – wa majimbo na viti maalum – wanafaa ndiyo maana hata wananchi wamewachagua wawawakilishe, lakini kinachoendelezwa na viongozi wa upinzani ni hoja zisizo na mashiko ambazo dhahiri zinaonyesha kwamba walitaka ama walitaka wenyewe wawe kwenye kamati hizo au walitaka maswahiba wao ndio wateuliwe.
Ninaamini kwamba, wabunge wote ni sawa, wana haki sawa na hakuna mbunge aliye bora kuliko mwingine.
Hapa pia naungana na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) Zitto Zuberi Kabwe, aliyesema kupitia ukurasa wake wa facebook, namnukuu; "Kamati zote za Bunge zina hadhi sawa ndani ya Bunge. Kila mbunge ana haki ya kuwa kwenye kamati yeyote ile na hakuna mbunge bora zaidi ya mwingine. Kanuni zimeweka utaratibu wa uteuzi kwenye Kamati ikiwemo maombi ya mbunge, uzoefu na ujuzi wa eneo husika.”
"Wanaolalamika leo upangaji wa Kamati ndio usiku wa kuamkia jana walimshinikiza Spika asiwapange mahasimu wao kisiasa kwenye Kamati wanazoona wao ni nyeti. Ni unafiki uliopitiliza unapojenga hoja ya uzoefu, chaguo la Mbunge na ujuzi wakati huo huo wenye vigezo vyote hivyo unawapiga vita kwa sababu za kisiasa.
"Ni dhahiri kuwa mpangilio wa Kamati unajenga Bunge kibogoyo,  Nilitahadharisha toka Bunge la 11 lilipoanza kwamba, "kuna dalili za Serikali kutaka kulidhibiti Bunge ( kumbukeni sarakasi za Tulia Ackson ambaye sasa ni Naibu Spika) ."
"Kiongozi unapokwenda kwa Spika kusema 'fulani asipangwe Kamati fulani kwa sababu atapata sifa' halafu ukataka 'nyumbu' wako ndio wapangwe huko ujue unaisadia Serikali kudogosha Bunge. Spika anapoamua Nyote, huyo usiyemtaka na nyumbu wako wasiende huko ujue amekudharau sana.
"Unapoona Viongozi wa Serikali wanahangaika kupanga Kamati za Bunge watakavyo wao ujue viongozi hao ni dhaifu, hawana nia njema na hawataki kuwajibishwa.
"Twendeni kwenye hizi hizi Kamati tulizopangiwa kuwafanyia kazi Watanzania. Twendeni tukaonyeshe kuwa Bunge litabaki Bunge tu na Wabunge tusikubali Bunge Kibogoyo. Ni lazima Bunge lidhibiti Serikali hata Serikali hiyo ikiwa inaongozwa na Malaika. Serikali ni chombo cha mabavu lazima idhibitiwe, na ndio kazi ya Bunge kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 63."
Maneno haya ya Zitto Kabwe yana changamoto kubwa kwa serikali, Bunge na wabunge wa upinzani na hapa tunajifunza jambo jingine kwamba, kumbe siku moja kabla ya kususia vikao, wapo viongozi wa upinzani waliojipenyeza hadi kwa Spika ili kutaka ‘watu wao’ waingie kwenye kamati fulani na kuwazibia baadhi ya wabunge eti watapata sifa wakipangwa huko.
Sasa Spika akaamua ‘wote maziganyande’ – wamekosa wote – ndugu zangu wapinzani wanaendeleza visa vya ndugu wa mume na kulalamika bila mpangilio.
Nawaomba waheshimiwa wabunge wote wawe kitu kimoja, wajenge taifa hili si kwa kukomoana, kukamiana au kuchukiana. Wote wanajenga nyumba moja hivyo hawana sababu ya kugombea fito.
Kamati hizi zinapaswa kuwajibika kwa kasi ile ile ya Serikali ya sasa, zijadili mambo ya msingi yenye kuleta maendeleo kwa taifa na siyo ubabaishaji.
Suala la kususa vikao kamwe halitaweza kuwafanya wabunge hawa wa upinzani wakaonekana ni watetezi wa wananchi wao, zaidi vitendo hivyo vinawadhalilisha kwa sababu si vya kiungwana.


No comments:

Post a Comment