Katibu Mtendaji wa Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) Godfrey Mungereza (Kushoto) akizungumza na Msanii Joseph Stanford
ofisini kwake mapema wiki hii. Msanii huyu ametembea kwa miguu kutoka Mwanza
hadi Dar es Salaam kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli.
Katibu Mtendaji wa Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) akimkabidhi cheti cha usajili Msanii Joseph Stanford
aliyetembea kwa miguu kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam kumpongeza Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Kushoto ni
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mitaji na Misaada kwa wasanii Bi. Elineka Ndowo.
NEWS
RELEASE
BASATA
LAMPONGEZA MSANII JOSEPH STANFORD ALIYETEMBEA KWA MIGUU KUTOKA MWANZA HADI DAR
ES SALAAM KUMPONGEZA RAIS MAGUFULI
Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) limempongeza Msanii Joseph Stanford kutoka Mwanza aliyetembea kwa
miguu umbali wa zaidi ya kilometa 1200 kumpongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli
kutokana na utendaji wake pia uundaji wa Idara ya Sanaa iliyo chini ya Wizara
ya Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni.
Aidha, BASATA imempa zawadi
ya usajili bure msanii huyu ili atambuliwe rasmi katika tasnia ya Sanaa na
baadaye kufanya kazi zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za sekta
hii.
Akizungumza ofisini kwake,
Katibu Mtendaji wa BASATA Godfrey Mngereza alisema kuwa Stanford ameonesha
uzalendo wa hali ya juu kwa nchi yake kwani haikuwa kazi rahisi kutembea umbali
mrefu na usiku na mchana kuja kumpongeza Rais Dkt. Magufuli.
“Sisi kama Baraza
tunafarijika sana, tunafurahi kuona wasanii na vijana kwa ujumla mnakuwa
wazalendo na kufurahishwa na kasi ya utendaji wa Serikali ya awamu ya tano. Tunafurahi
zaidi unapopeleka ujumbe wa Wasanii kwamba wamefurahia kuundwa kwa idara ya Sanaa” alisema.
Aliongeza kuwa BASATA
limetambua uzalendo na moyo wake wa kuipenda Sanaa hivyo limeamua kumpa zawadi
ya usajili bure ili iwe chachu ya kujikita kwenye Sanaa na kufanya kazi zake
kwa weledi na kuzingatia maadili ya kitanzania.
Kwa upande wake kijana
Stanford alisema kwamba anafurahia kwa mapokezi aliyopewa na BASATA huku
akisisitiza kuwa ndoto yake ni kumfikishia salamu za pongezi Mheshimiwa Rais
Dkt. John Magufuli lakini pia kupata mafanikio kwenye kazi za Sanaa.
“Nafurahi sana kwa mapokezi
niliyopata, muda wowote nitaenda kumfikishia salamu za pongezi Rais wangu.
Matumaini yangu ni kuona sekta ya Sanaa inazidi kuthaminiwa na kusonga mbele”
alisisitiza Stanford.
Msanii Stanford anatokea
eneo la Mabatini jijini Mwanza na ametembea kwa siku ishirini na tano kutoka
Mwanza hadi Dar es Salaam na ametumia kiasi cha shilingi elfu arobaini na tano
pekee.
No comments:
Post a Comment