Mshauri wa Kimataifa wa Kujitegemea wa Kampuni ya Mabibo Beer Wines and Spirits Ltd, James Rugemalira akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu kupinga uamuzi wa Tume ya Ushindani (FCC) na kuidai fidia hiyo ya Shs. 1 trilioni kutokana na hasara wanayoipata kwa kuruhusu bia ya Windhoek kuingia katika soko la Tanzania kiholela.
Mwenyekiti wa Kampuni ya Mabibo Beer Wines and Spirits Ltd, Benedicta James Rugemalira (katikati), akizungumza katika mkutano huo na kusema bia halali iliyopo kwenye soko ni ile yenye namba MB 66 na inayosambazwa na kampuni hiyo. Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mahusiano ya Mabibo, Anic Kashasha na Wakili, Stephano Kamala.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mahusiano ya Kampuni ya Mabibo, Anic Kashasha (katikati), akizungumza katika mkutano huo. Kushoto ni Wakili wa Kampuni hiyo, Respicious Didace na Mwenyekiti wa Kampuni ya Mabibo Beer Wines and Spirits Ltd, Benedicta James Rugemalira.
Wakili, Stephano Kamala (kulia), akizungumza katika mkutano huo. (PICHA ZOTE KWA HISANI YA BLOG YA HABARI ZA KIJAMII)
Na Daniel Mbega
KAMPUNI ya Mabibo Beer Wines and Spirits Ltd imesema inakusudia kuifikisha mahakamani Tume ya Ushindani (FCC) ikidai fidia ya Shs. 1 trilioni kutokana na kukiuka mkataba baina ya kampuni hiyo na Kampuni ya Bia ya Namibia (NBL - Namibia Breweries Limited) unaoipa Mabibo haki ya kipekee ya kusambaza bia ya Windhoek nchini Tanzania.
Mbali ya kusudio hilo, kampuni hiyo pia imeiomba Mahakama ya Rufaa kutoa uamuzi kuhusu uhalali wa uamuzi uliochukuliwa na Baraza la Ushindani (FCT) mwezi Aprili 2015 kuhusu haki ya Mabibo ya kuagiza na kusambaza bia za Windhoek kipekee katika soko la Tanzania.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam jana, Mshauri wa Kimataifa wa Kujitegemea wa Mabibo Beer Wines and Spirits Ltd, James Rugemalira, alisema anashangazwa ni kwa vipi vyombo hivyo viwili vimekuwa vikikiuka sheria na kuinyima haki kampuni hiyo hata baada ya Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kutoa hukumu.
Rugemalira alisema kwamba, mnamo mwezi Aprili 2015, FCT ilitoa uamuzi unaotafsiriwa kwamba kwamba mkataba baina ya Mabibo NBL ambao ulisajiliwa kwa matakwa ya Sheria ya Alama za Biashara na Huduma, haukuwa halali kisheria.
"Si FCC wala FCT yenye mamlaka yakutengua uamuzi halali wa Mahakama kutafsiri sheria na katiba ya Tanzania. Katika kufungua shauri lake katika Mahakama ya Rufaa tarehe 24 Juni 2015, Mabibo imeiomba Mahakama kuthibitisha kwamba mwenendo wa Mabibo ni sahihi kwa mujibu wa Sheria ya Ushindani ya mwaka 2003, kama Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni ilivyoamua mwaka 2010 na kuwa FCC na FCT walifanya kinyume cha mamlaka zao za kisheria na kikatiba na kujipa uwezo wa kutengua maamuzi ya Mahakama za Tanzania" alisema Rugemalira.
Rugemalira alisema kwamba, Mabibo inataka fidia hiyo kutoka FCC na washirika wake kwa sababu amri isiyo halali ya FCC imeruhusu mwendelezo wa uagizaji wa bia ya Windhoek na wasambazaji wasioruhusiwa hivyo kuharibu biashara ya Mabibo na mkondo wa uadilifu wa bidhaa ya Windhoek katika soko la bia Tanzania.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Mahusiano ya kampuni hiyo, Anic Kashasha, alisema kitendo kilichofanywa na vyombo hivyo viwili vimeitia hasara kubwa kampuni hiyo na kuchelewesha hatua ya ujenzi wa viwanda vitatu vya kuzalisha bia hiyo.
"Tumepanga kujenga viwanda vitatu nchini - Kagera, Kilimanjaro na Tanga - lakini kwa hali ya sasa jitihada hizi zinakwama kwa sababu mauzo ya bia ya Windhoek hapa nchini ni kiasi cha asilimia 0.05 tu ya soko la jumla badala ya asilimia 5 ambayo imekusudiwa katika soko hilo.
"Kwa miaka kadhaa sasa tumeendelea kuumia kutokana na uamuzi huu wa vyombo hivi ambao sasa umefanya waagizaji wengine wasambaze bia ya Windhoek huku sisi wenye haki tukiumia," alisema Kashasha.
Akitoa ufafanuzi wa kisheria, Mwanasheria wa kampuni hiyo Respicious Didace, alisema FCC na FCT hawana haki ya kisheria ya kukiuka hukumu halali ya mahakama kwani, kisheria hakuna chombo chochote kinachoweza kutengua uamuzi wa mahakama isipokuwa mahakama yenyewe kwa kufanya marejeo au mahakama ya juu.
"Mahakama yenyewe inaweza kutengua hukumu hiyo kwa kufanya marejeo (review) au mahakama ya juu yake, lakini hakuna chombo kingine chochote kinachoweza kupinga amri halali ya mahakama," alisema Didace.
Kwa miaka kadhaa sasa Kampuni ya Mabibo imekuwa ikilalamikia hatua ya vyombo hivyo viwili katika biashara kuinyima haki yake ya msingi na kusisitiza kwamba ni vyema kuzingatia dhana ya utii wa sheria bila shuruti.
“Kuna amri ya Mahakama ambayo inazuia mtu yeyote kuingiza na kusambaza Windhoek katika soko hapa nchini bila kuomba na kupata kibali kutoka Mabibo. Amri hii ni halali na inapswa ifuatwe,” alisisitiza Rugemalira.
Rugemalira alisisitiza kuwa bia ya Windhoek inayopaswa kuuzwa katika soko la Tanzania lazima iwe na alama ya MB66 na kwamba inasambazwa na kampuni ya Mabibo Beer Wines and Spirits Limited pekee.
No comments:
Post a Comment