Na Daniel Mbega wa www.brotherdanny.com
MABINGWA
wa soka Tanzania Bara, Yanga, leo wanafungua pazia la michuano ya Kombe la
Kagame dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, pambano ambalo linatarajiwa kuwa la
kusisimua kutokana na ukongwe wa timu hizo katika historia ya kandanda Afrika
Mashariki na Kati.
Hili litakuwa
pambano lao la nane katika mashindano mbalimbali, lakini ni la sita katika
Kombe la Kagame tangu zilipokutana mara ya kwanza mwaka 1975 kule Zanzibar.
Timu hizi
ziliwahi kupambana mara mbili katika raundi ya kwanza ya Klabu Bingwa Afrika
mwaka 1984 ambapo katika mchezo wa kwanza uliofanyika Dar es Salaam Aprili 7,
zilitoshana nguvu kwa kufungana 1-1 na ziliporudiana mjini Nairobi Aprili 28,
Yanga ikalala kwa mabao 2-1.
Hata
hivyo, mechi yao ya kwanza iliiponza Yanga ikafungiwa na Shirikisho la Soka
Afrika (CAF) kutoshiriki mashindano hayo kwa miaka mwili kwa madai ya kutoa
rushwa kwa waamuzi kutoka Ethiopia na viongozi wake wawili, John Ketto na Julius
Rutainurwa, wakafungiwa maisha kutojihusisha na soka.
Gor Mahia
nayo mwaka huo ilifungiwa miaka miwili kutokana na wachezaji wake kumpiga
mwamuzi wakati ilipocheza na Zamalek huko Cairo, Misri katika mchezo wa raundi
ya pili ya Klabu Bingwa Afrika. Pia wachezaji sita wa Gor Mahia walifungiwa kwa
mwaka mmoja, adhabu ambayo ilitambuliwa na CECAFA. Katibu Mkuu wa KFF naye
alifungiwa na CAF kwa miaka miwili kutokana na kutuma teleksi kulikashfu
Shirikisho hilo kwa kuiadhibu Gor Mahia.
Ukiachana na
mechi hizo mbili, Yanga na Gor Mahia zimekutana mara tano kwenye mashindano
haya ya Kagame, ambapo Gor imeshinda mechi tatu, kutoka sare moja na Yanga
imeshinda mechi moja tu.
Zilikutana kwa mara ya kwanza katika nusu
fainali mjini Zanzibar Januari 11, 1975 na Yanga ikashinda kwa mabao 2-0,
ushindi ambao pia iliupata katika mechi ya fainali dhidi ya Simba.
Mwaka 1982 Yanga na Gor Mahia zilikuwa
kwenye Kundi B mjini Kisumu, Kenya ambapo katika mechi ya kundi hilo, Gor
ilishinda 3-1. Zilipokutana katika mechi ya kutafuta mshindi wa tatu, Gor
ikashinda tena 2-1.
Mwaka 1996 timu hizo zilipangwa Kundi B
mjini Mwanza. Katika mechi yao ya kwanza, zilifungana 1-1, lakini katika mechi
ya kutafuta mshindi wa tatu, Gor ikashinda mabao 4-0.
Swali kwamba nani ataibuka mbabe katika
mechi ya leo ndilo linalotawala na litaamuliwa na filimbi ya mwisho uwanjani.

No comments:
Post a Comment