Na Hastin Liumba, Tabora
JUMLA ya wajawazito 156,361 katika kipindi cha mwezi Januari hadi Desemba 2014 walisajiliwa katika kliniki za afya ya uzazi na mtoto mkoani Tabora.
Mratibu msaidizi huduma ya afya ya uzazi na mtoto Audrey Bakuza alisema hayo wakati afisa habari na mawasiliano Anna Sawaki toka shirika la EGPAF linalofadhiliwa na mashirika ya CDC na USAID toka Marekani ulipozuru hospitali ya rufaa Kitete.
Bakuza alisema kati ya hao asilimia 16 walikuwa chini ya wiki 12 za ujauzito na asilimia 80 walikuwa zaidi ya wiki 12.
Alisema hali hiyo bado kuna mwamko mdogo katika jamii kuhusiana na wajawazito kuanza kuhudhuria kliniki mapema mara mama anapogundulika ana ujauzito.
Alisema jumla ya wajawazito 61599 ambao ni sawa na asilimia 87 walijifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya na asilimia 89 walihudumiwa na watoa huduma wenye ujuzi.
Aidha alisema wajawazito 5,730 sawa na asilimia 8 walijifungulia nyumbani na kinamama 1,247 sawa na asilimia 2 walizalishwa na wakunga wa jadi.
Bakuza anabainisha zaidi kuwa jumla ya kinamama wajawazito 128,083 walipatiwa ushauri nasaha na kupima afya maambukizi ya VVU kati yao 3,842 sawa na asilimia 3 walikuta na maambukizi na walipatiwa huduma za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto .
Alisema katika kipindi cha wiki sita baada ya kinamama kujifungua jumla ya wajawazito 13,146 walipata huduma na watoto 86,378 sawa na asilimia 84 walipata chanjo.
Akizungumzia changamoto alisema bado kumekuwa na maamuzi ya wajawazito wengi kuchelewa kufanya maamuzi ya kutumia huduma za afya katika jamii zetu kwa kuwa mwanaume pekee ndiye mtoa maamuzi katika familia.
Aidha changamoto nyingine ni upungufu wa watoa huduma wenye ujuzi kwa baadhi ya vituo vya kutolea huduma.
No comments:
Post a Comment