
Rais Pierre Nkurunziza.
Wanajeshi wakipongezwa na wananchi baada ya kupindua serikali ya Burundi.

Kiongozi wa ''Mapinduzi'' ya Burundi, Meja Jenerali Godefroid Niyombare

Apollo Milton Obote

Jenerali Idi Amin Dada
Na Daniel Mbega,
Mwanza
JUMATANO Mei 13, 2015 majira ya saa 9 alasiri, Meja
Jenerali Godefroid Niyombare, aliongoza ‘mapinduzi’
ya kijeshi dhidi ya Rais Pierre Nkurunziza ikiwa ni hatua ya kuunga mkono nguvu
ya umma kupinga kusudio la rais huyo kujiongezea muhula wa tatu wa kuwa madarakani kinyume
cha katiba ya nchi hiyo.
Wakati mapinduzi hayo yakifanyika, Rais
Nkurunziza mwenyewe alikuwa jijini Dar es Salaam katika kikao cha wakuu wa nchi
za Afrika Mashariki waliotaka kutafuta suluhu ya kumaliza mgogoro huo ambao
umeacha majeraha makubwa kwa Warundi, huku baadhi wakiwa wamepoteza maisha
kufuatia kushambuliwa na polisi wakati wakifanya maandamano.
Tukio hili linanikumbusha lile la
Januari 25, 1971 nchini Uganda ambalo liliongozwa na Jenerali Idi Amin Dada likiwa
ni sehemu ya Vita Baridi, ambalo lilifanikiwa kumuondoa madarakani Apolo Milton
Obote na kuuweka utawala wa kidikteta wa Amin.
Jenerali Amin alikuwa anaungwa mkono na
Uingereza na Israel, ingawa Waisraeli nao walionja joto ya jiwe baada ya
kibaraka wao huyo kuwateka raia wa Israel kabla ya vikosi vya kijasusi kutoka
Mossad havijaenda kuwakomboa kwenye Uwanja wa Ndege wa Entebbe.
Kama ilivyotokea Burundi, wakati mapinduzi
yakitokea kule Uganda mwaka huo, Obote alikuwa Singapore akihudhuria mkutano wa
Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Madola, ikabidi akimbilie jijini Dar es Salaam
kupata hifadhi.
Uingereza ilimuunga mkono Amin kwa sababu Obote alitaka
kutaifisha biashara zote zilizokuwa zikifanywa na Waingereza, huku Amin naye
akihofia kufukuzwa kazi mara baada ya Obote kurejea kwani kulikuwa na mtazamo
tofauti kati ya utawala wa serikali kuu na jeshi.
Obote alirejea madarakani mwaka 1980, lakini Julai 27,
1985 akapinduliwa tena katika mapinduzi yaliyoongozwa na Brigedia Bazilio
Olara-Okello. Marais wengine waliokuwa wamepinduliwa Uganda ni Yussuf Lule
aliyetawala kati ya Aprili 13 ha Juni 1979 (siku 70) baada ya majeshi ya
Tanzania kuung’oa utawala wa Nduli Idi Amin; Godfrey Binaisa akatawala kati ya
Juni 20 1979 hadi Mei 12, 1980 (siku 327); Paulo Muwanga akatawala kwa siku 10 tu
kati ya Mei 12 na Mei 22, 1980 kabla ya kujiuzulu na kuipisha Tume Maalum ya
Urais kuongoza kwa siku 207 na hatimaye kumkabidhi Obote madaraka.
Kihistoria, hali ya kisiasa ya Burundi haina nafuu wala
afadhali kwani kumekuwepo na Vita vya Wenyewe kwa Wenyewe kwa miaka mingi na
hasa baada ya uhuru uliopatikana mwaka 1962. Hii yote ni kwa sababu ya migogoro
ya kikabila baina ya Watutsi walio wachache wanaotawala na Wahutu walio wengi
wanaokataa kutawaliwa.
Rekodi zinaonyesha kwamba vita vya wenyewe kwa wenyewe
nchini humo vilipamba moto kati ya mwaka 1993 hadi 2005. Mgogoro ulianza mara
baada ya uchaguzi mkuu wa vyama vingi nchini humo tangu ilipopata uhuru kutoka
kwa Wabelgiji, na wengi walitarajia kwamba, baada ya kuapishwa kwa Pierre
Nkurunziza Agosti 2005, huenda ndio ungekuwa mwisho wa yote, lakini hali
imekuwa tofauti.
Kabla ya ukoloni, Burundi iliongozwa na utawala wa
kifalme wa Kitutsi kama ilivyokuwa kwa Rwanda. Wabelgiji na Wajerumani waliona
ni afadhali kuongoza kupitia utawala uliokuwepo ambao tayari Watutsi walikuwa
wanawakandamiza Wahutu. Hii iliwajengea kiburi Watutsi na kujiona kwamba wana
haki ya kutawala na siyo kutawaliwa!
Tofauti na Rwanda, Burundi iliamua kuendelea na utawala
wa kifalme mara baada ya kupata uhuru, ingawa kwa miaka takriban 25 jeshi
lililoongozwa na Watutsi ndilo limekuwa likitawala kwa nguvu kabla ya uchaguzi
wa kidemokrasia wa Juni 27, 1993. Uchaguzi huo ulirejesha kumbukumbu za miaka
25 nyuma wakati Michel Micombero alipoongoza mapinduzi mwaka 1966 na kuuondoa
ufalme na badala yake akaifanya Burundi kuwa Jamhuri.
Chini ya utawala wa Micombero, Watutsi wachache walijaa
kwenye vyeo karibu vyote muhimu vya serikali. Mwaka 1972 kundi la Wahutu lililofahamika
kama Umugambwe w'Abakozi b'Uburundi au Chama cha Wafanyakazi Burundi (UBU) kiliandaa
na kufanya mashambulizi kadhaa dhidi ya Watutsi, kwa lengo la kulimaliza kabisa
kabila hilo. Lakini jeshi la Watutsi likawashambulia Wahutu kwa silaha kali na
hakuna idadi kamili ya Wahutu waliouawa iliyopata kurekodiwa ingawa makadirio
yanaonyesha kwamba Warundi wote waliokufa walikuwa takriban 100,000. Warundi wengi
wakakimbilia Tanzania na Rwanda, ambapo baadhi yao tayari wamekwishapewa uraia
wa Tanzania.
Mapinduzi ya mwisho kabla haya ya sasa yalifanyika mwaka
1987 na kumuweka madarakani ofisa wa jeshi wa Kitutsi Meja Pierre Buyoya ambaye
alijaribu kubadilisha baadhi ya mambo na kuweka mjadala wa kitaifa, lakini
badala yake hali hiyo ikachochea mgogoro wa kikabila.
Mapigano yakaibuka sehemu mbalimbali ambapo makundi ya Wahuti
yaliwashambulia na kuua mamia ya Watutsi, Buyoya akatuma jeshi kuwaua maelfu ya
Wahutu.
Oktoba 21, 1993, rais wa kwanza wa Burundi aliyechaguliwa
kidemokrasia akitokea kabila la Wahutu, Melchior Ndadaye, aliuawa na waasi wa
Kitutsi na kuzusha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ambayo yalisababisha watu
kati ya 50,000 hadi 100,000 kuuawa ndani ya mwaka mmoja. Rais aliyefuata
baadaye, Cyprien Ntaryamira, ambaye naye alikuwa Mhutu, aliuawa kwenye ajali ya
ndege pamoja na Rais wa Rwanda, Mhutu Juvenal Habyarimana, wakati wakitokea Dar
es Salaam.
Hata alipoteuliwa Sylvestre Ntibantunganya Aprili 8,
1994, hali haikuweza kutulia Burundi. Nakumbuka Mwalimu Julius Nyerere ndiye
aliyeteuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa msuluhishi wa mgogoro wa Burundi na
alijitahidi sana ambapo matokeo yake ni Wahutu na Watutsi kufikia muafaka wa
kuwa na serikali ya mseto mwaka 1996.
Mwaka 1996, Mtutsi Meja Pierre Buyoya akachukua madaraka akimpindua
Mhutu Ndibantunganya. Mwaka 1998, Buyoya na Bunge lililoongozwa na Wahutu
walikubaliana kusaini katiba ya mpito na Buyoya akaapishwa kuwa rais. Mazungumzo
ya amani ya Burundi yakaanza rasmi mjini Arusha Juni 15, 1998.
Baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere, Mzee Nelson Mandela
ndiye aliyeshika mikoba ya upatanishi wa Burundi na mwaka 2000 mazungumzo
yakafanyika nchini Tanzania na kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya mpito
ambapo rais na makamu wa rais wangebadilisha vyeo kila baada ya miezi 18.
Wakati ambapo serikali na vyama vitatu vya Kitutsi
vilisaini makubaliano hayo, vyama viwili vikuu vya Kihutu viligoma kushiriki,
na mapigano yakaendelea. Mkutano wa amani mjini Arusha Novemba 30, 2000
ulifungwa bila mafanikio.
Aprili 18, 2001, jaribu la mapinduzi lilishindika. Hata hivyo,
mnamo Aprili 9, 2003 makao makuu ya Jeshi la Umoja wa Afrika nchini Burundi
yalifunguliwa jijini Bujumbura chini ya Meja Jenerali Sipho Binda wa Afrika
Kusini. Hadi kufikia Oktoba 18, 2003, ilielezwa kwamba jeshi hilo lilikuwa
limejiimarisha zaidi likiwa na wanajeshi 1,483 kutoka Afrika Kusini, Waethiopia
820, na 232 kutoka Msumbiji.
Mnamo Julai 2003, mashambulio ya waasi yaliua watu 300 na
kuwaacha watu 15,000 wakiwa hawana makazi. Lakini ni mwezi huo ambao Mhutu
Domitien Ndayizeye alipotwaa madaraka ya urais katika serikali ya mpito, na
Buyoya akang’atuka. Pamoja na kikundi kikuu cha waasi cha Wahutu - National
Council for the Defense of Democracy–Forces for the Defense of Democracy (FDD)
- Rais Ndayizeye akasaini makubaliano ya kumaliza mapigano kwenye Mkutano wa
Wakuu wa Nchi za Afrika uliofanyika jijini Arusha, Tanzania mwezi Novemba 2003.
Chini ya makubaliano hayo, FDD kikawa chama cha siasa, na ikaamuliwa kwamba,
wanamgambo wote wa Kihutu waingizwe kwenye jeshi la nchi hiyo lililokuwa
limesheheni Watutsi watupu.
HISTORIA YA
MATUKIO KATIKA BURUNDI
Wakati wa
ukoloni
1890: Wajerumani waliitwaa Ruanda na Urundi (Burundi) pamoja na Tanganyika na
kuifanya koloni lao waliloliita German East Africa chini ya Carl Peters.
1919: Wajerumani walipotea Ruanda-Urundi kwa Ubelgiji chini ya Udhamini wa
Ligi ya Mataifa. Wajerumani na Wabelgiji wote walitawala kupitia mfumo wa
kijadi wa Watutsi ulioongozwa na Mwami.
1950: Ubelgiji iliunda serikali ya ndani kuwaandaa Wanyarwanda na Warundi kwa
ajili ya kujitawala.
1950: Mtutsi Prince Louis Rwagasore alianzisha chama cha siasa katika mfumo
wa vyama vingi, kilichoitwa Union for National Progress (UPRONA).
Uhuru
1962: Prince Rwagasore aliuawa, lakini chama chake cha UPRONA kiliongoza
serikali ya kwanza kwa ushirikiano wa Mfalme Mwambutsa IV.
1965: Utawala wa kijadili ulianguka katika uchaguzi wa kwanza baada ya
wanasiasa wa Kihutu kushinda kwa wingi na kuongoza mabunge yote. Mfalme
Mwambutsa alivunja bunge kabla halijakutana na jeshi lililojaa Wahutu likaasi. Jaribu
la mapinduzi la jeshi hilo lilizuiliwa na maofisa wa jeshi wa Kitutsi
wakiongozwa na Michel Micombero. Mfalme Mwambutsa IV akakimbia nchi na mwanawe Ntare
V akatawazwa. Micombero alimwondoa Ntare maarakani na kuamrisha mashambulizi
yaliyosababisha vifo vya Wahutu 5,000.
1969: Kulikuwa na harakati nyingi za Wahutu wasomi.
1972: Idi Amin wa Uganda alimsaidia Micombero kumkamata Ntare V (ambaye
baadaye alikufa akiwa gerezani nchini Burundi. Akihusisha machafuko
yaliyosababisha vifo vya maofisa 2,000 wa jeshi wa Kitutsi, Micombero akaanzisha
utawala wa mkono wa chuma (martial law). Wahutu wasomi ndio waliokuwa walengwa
na kati ya 80,000 na 500,000 waliuawa, wakati zaidi ya Wahutu 100,000
walikimbia nchi na hawakurudi tena. Wakati huo, Ufaransa, China na Libya
ziliongeza msaada wa kijeshi kwa serikali ya Burundi, na ripoti ya kadhaa
zinasema kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kwa raia wa Kihutu.
1974: Micombero aliifanyia marekebisho katiba na kuifanya nchi ya chama
kimoja chini ya UPRONA.
1975: Japokuwa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilifungua
mashtaka dhidi ya viongozi wa Burundi kuhusu unyanyasaji dhidi ya Wahutu,
baadaye kesi hiyo ilitupiliwa mbali.
1976: Micombero alipinduliwa katika mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na
Kanali Jean-Baptiste Bagaza, lakini madaraka yakaendelea kubaki wa Watutsi
waliojaa kwenye vyeo vya juu vya jeshi, watumishi wa umma na UPRONA.
1985: Bagaza alipanua wigo dhidi ya wapinzani wa serikali na kuliongeza
Kanisa Katoliki kwenye mamlaka.
1987: Bagaza alipinduliwa na Pierre Buyoya katika mapinduzi mengine ya
kijeshi.
1988: Kulikuwa na machafuko makubwa wakati jeshi lilipowaua Wahutu 25,000
kama kisasi kwa mauaji ya baadhi ya Watutsi kaskazini mwa nchi hiyo. Takriban Wahutu
60,000 walikimbilia Rwanda na wengine 100,000 wakakosa mahali pa kuishi nchini Burundi.
1991: Chama cha Mapinduzi ya Ukombozi wa Wahutu – The Revolutionary Party for
the Liberation of the Hutu People (PALIPEHUTU) – kilianzisha mashambulizi
zaidi, na kuanzisha mapambano mapya.
1991: Buyoya aliongeza ushiriki wa Wahutu kwenye serikali. Japokuwa Wahutu
walijaa kwenye nafasi za uwaziri, mamlaka ya mwisho yalibaki kwa Kamati ya
Kijeshi ya Wokovu ya Taifa iliyokuwa na Watutsi.
1992: Katiba mpya ikafungua milango kwa uchaguzi wa vyama vingi.
1993: Uchaguzi ulishindwa kufanyika wakati machafuko makubwa yalipoibuka. Karibu
wakimbizi 175,000 walikimbilia Rwanda.
Februari 1995: Mkutano wa OAU kufanyika kwa mara ya kwanza kabisa jijini Bujumbura
kuzungumzia hali ya wakimbizi walioko Rwanda.
1995/09/09: Mkutano wa pilia wa OAU kufanyika Bujumbura kuzungumzia tatizo la
wakimbizi walioko Rwanda.
*Imeandaliwa na www.brotherdanny.com (Ukiichota usiache kuonyesha chanzo).
No comments:
Post a Comment